Na
Daniel Mbega, Iringa
MFUKO wa Kimataifa wa Kuhifadhi Mazingira (WWF)
mkoani Iringa umetoa mafunzo na vifaa kwa wakulima wa mpunga wa Kata za Pawaga
na Idodi wilayani Iringa katika kuhamasisha kilimo shadidi.
Vifaa 12 vilivyotolewa, ambavyo vinatarajiwa
kukabidhiwa kesho Jumamosi vitakavyosaidia kupalilia pamoja na kuvunia ambavyo
vina thamani ya Shs. 960,000, vitawanufaisha wakulima wa mpunga wa Skimu ya
Umwagiliaji ya Mlenge, Pawaga kutoka vijiji vya Kinyika, Isele, Kisanga na
Magombwe.
Vijiji vya Kata ya Idodi vitakavyonufaika ni Idodi,
Tungamalenga, Mapogoro na Makifu ambavyo vipo katika Skimu ya Magozi.
Mbali ya vifaa hivyo, WWF pia imegharamia mafunzo
hasa katika vijiji vya Kata ya Pawaga, mafunzo ambayo yanaendeshwa na Shirika
lisilo la kiserikali la Rural Urban Development Initiative (RUDI) la mjini
Iringa.
Ofisa wa WWF mkoani Iringa, Bi. Martha Sanga,
amesema wanashirikiana na Idara ya Kilimo ya Wilaya ya Iringa katika mpango huo
ili kuwawezesha wakulima wapate tija katika shughuli zao na kuwakomboa katika
umaskini.
Mafunzo na vifaa hivyo, pamoja na gharama nyingine
za uendeshaji, vimegharimu Shs. 8 milioni, ambazo ndizo zilizoombwa na Idara ya
Kilimo kufanikisha zoezi hilo.
“Tuliwafuata Idara ya Kilimo Wilaya na kuwaambia
kwamba tunataka kuwasaidia wakulima wa mpunga, lakini wilaya ikatuambia kwamba
kwa kuwa nao wanafanya kazi katika maeneo hayo, basi ni vyema watueleza wapi
walipopungukiwa ili tuwasaidie.
“Walisema wanahitaji kusaidiwa katika mafunzo na
vifaa vya palizi, jambo ambalo nasi tumeona linafaa hasa kwa kuzingatia kwamba
tulikuwa tumechelewa msimu wa kupanda, lakini mafunzo waliyoyapata yatawasadia
wakulima kwa msimu ujao,” alisema Bi. Martha.
Katika mafunzo hayo, wakulima wanaelekezwa namna ya
kushiriki katika kilimo bora chenye tija kwa uchaua mbegu bora kwa kuzingatia
kanuni bora za kilimo shadidi na kupanda kwa nafasi ya 25sm mstari kwa mstari
na mche kwa mche.
Mbegu zinazopendekezwa kwa kilimo chenye tija ni
aina ya Saro 5 (TXD 306) ambayo imeonekana bora zaidi, hairefuki, inatoa
machipukizi mengi, ina uwezo wa kutoa mavuno mengi kutoka magunia 30 hadi 40
kwa ekari moja ambazo zina ujazo wa 80kg.
Inaelezwa kwamba, mbegu hiyo tayari imeanza
kuonyesha matunda mazuri hasa kwa wakulima wa Skimu ya Tungamalenga ambao
tayari wamekwishapatiwa mafunzo na shirika hilo la RUDI tangu mwaka 2013.
Shirika la WWF limejikita katika kuhamasisha
shughuli za utunzaji wa mazingira pamoja na maendeleo ya jamii, ikiwemo kilimo,
ambapo limekuwa likishiriki kikamilifu katika utoaji wa elimu na vifaa kwa
wanajamii.
Mwaka 2013 lilianzisha kampeni ya utunzaji wa
mazingira katika ngazi ya shule kwa kutoa mafunzo kwa washiriki zaidi ya 60
kwenye Kijiji cha Ifunda mkoani Iringa ambapo pia walitoa vifaa mbalimbali
vilivyogharimu Shs. 1.2 milioni kwa shule za Kibaoni, Ifunda Tech, Ifunda Girls
na Lyandembera sekondari katika harakati za kuuokoa Mto Ruaha Mkuu ambao
unakabiliwa na hatari ya kutoweka kutokana na shughuli za kibinadamu.
“Hii ni kampeni ya kuhifadhi mazingira, hasa katika
eneo bonde la Mto Mbarali na Ndembera inayomwaga maji yao kwenye Mto Ruaha,”
alisema wakati huo Ofisa Elimu ya Mazingira wa WWF, Mwamini Masanja.
Mto Ruaha unamwaga maji katika mabwawa ya Mtera,
Kihansi na Kidatu ambayo yanategemewa sana katika uzalishaji wa umeme, hivyo
kukauka kwake kunamaanisha kwamba uzalishaji huo utapungua na kuwa janga kwa
taifa.
Hali ya baadaye ya Mto Ruaha Mkuu inaonekana kuwa
mashakani huku jitihada za serikali na wadau wa uhifadhi mazingira zikionekana
kugonga mwamba baada ya mto huo kukauka kwa kasi hivyo kutishia maisha ya
binadamu, wanyama na viumbehai vingine hasa katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Pamoja na serikali kuwafukuza wafugaji waliokuwa
wamevamia mabonde ya Usangu na Ihefu na kuwahamishia Kilombero, lakini shughuli
za kilimo cha umwagiliaji katika mashamba makubwa ya mpunga huko Mbarali,
Kapunga, Madibira, Pawaga na Idodi yamefanya maji mengi kuishia mashambani na
hivyo kutishia pia uwepo wa Bwawa la Mtera ambalo nalo linakauka.
Imetulia hii kwa maendeleo ya wakulima
ReplyDelete