Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba, akiteta jambo la Rais Dk. Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Wakati mchakato wa Katiba mpya unaendelea mjini Dodoma na suala la theluthi mbili likisumbua vichwa vya wengi, mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ameeleza kuwa kura za wajumbe 14 kutoka Zanzibar ndizo zitauokoa au kuukwamisha mchakato huo.
Dar es Salaam. Wakati mchakato wa Katiba mpya unaendelea mjini Dodoma na suala la theluthi mbili likisumbua vichwa vya wengi, mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ameeleza kuwa kura za wajumbe 14 kutoka Zanzibar ndizo zitauokoa au kuukwamisha mchakato huo.
Profesa Lipumba alikuwa kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi
nyumbani kwake, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam kuhusu mustakabali wa
mchakato wa Katiba baada ya kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kususia kuhudhuria vikao.
Kundi hilo lilisusia vikao Aprili 16 kwa madai kuwa Bunge lilipoteza
mwelekeo kwa kuacha kujadili Rasimu ya Katiba, hasa katika suala la
muundo wa serikali ya Muungano na kwamba chama tawala, CCM kiliingiza
suala la serikali mbili ambalo halimo kwenye rasimu hiyo badala ya
serikali tatu.
Kutokana na uamuzi wa Ukawa, ambayo inaundwa na wajumbe kutoka CUF,
Chadema, NCCR Mageuzi na baadhi wa kundi la 201 kutoka taasisi
mbalimbali za kijamii, kuna shaka kwamba mchakato huo huenda usifanikiwe
kutokana na ukweli kuwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inataka uamuzi
upitishwe na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Bara na idadi kama hiyo
kutoka Zanzibar.
Kutokana na utashi huo wa kisheria, Profesa Lipumba alisema wana
uhakika kuwa Katiba haitapita kwa kuwa wanao wajumbe 14 kutoka kundi la
201 ambao ndiyo tegemeo lao.
“Sisi tunao wabunge na wawakilishi kutoka Zanzibar wa vyama vyetu
ambao hawakwenda hata kwenye vikao. Tukiwajumlisha, tunahitaji watu 14
kutokana na wale wajumbe 77 (wa Zanzibar) wa Kundi la 201 na kule tuna
uhakika wa watu kama 21,” alisema.
“Wapo baadhi waliokwenda kuhudhuria vikao, lakini tunajua misimamo
yao. Tunajua kuna mbinu zinafanyika kuwarubuni, lakini tunawafuatilia
kwa karibu.”
Alisema kuwa Ukawa wana uhakika pia wa kuungwa mkono na wabunge na
wawakilishi wa CCM kutoka Zanzibar katika kutetea mamlaka ya Zanzibar.
“Kama mnafuatilia mazungumzo ya Baraza la Wawakilishi, katika
malalamiko ya suala la Muungano, mazungumzo ya CUF na CCM yalikuwa
yanafanana na hata ule waraka uliopelekwa bungeni kutoka CCM Zanzibar
ambao sasa wanaukana, unataka mamlaka tatu. Maana yake nini? Mamlaka ni
Serikali,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
“Hata kura zitakapopigwa, CCM hawawezi kupata theluthi mbili za upande wa Zanzibar. Suala la Katiba ni suala la maridhiano.”
Aitetea Tume ya Jaji Warioba
Huku akitetea uamuzi wa Ukawa kutoka nje ya Bunge la Katiba, Profesa
Lipumba ametaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na rasimu iheshimiwe
kwa kuwa imefanya kazi kubwa.
Utata Bunge la Katiba, NEC
“Pamoja na kwamba kila kundi lilikuwa na mambo yake katika Katiba,
yale mambo ya msingi yaliyoletwa na Jaji (mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Joseph)Warioba na Tume yake tuyasimamie na
yaongoze mchakato wa Katiba. Ukiisoma rasimu ile kwa kweli utaona Tume
hiyo imefanya kazi kubwa,” alisema Profesa Lipumba.
Amewataja makamishna wa iliyokuwa Tume hiyo ya Mabadiliko ya Katiba
akisema kuwa utaalamu wao ndiyo umezingatia umuhimu wa muundo wa
serikali tatu.
“Kati ya wataalamu waliobobea katika Katiba ni pamoja na marehemu Dk
Sengondo Mvungi na Profesa Palamagamba Kabudi. Siyo Profesa Issa Shivji
(namheshimu sana huyo, kwani ameandika mengi kuhusu Zanzibar kwamba
imebanwa sana),” alisema.
“Lakini, utaalamu wa Profesa Shivji ni sheria za kazi. Ni msomi
mwenye uelewa mpana… lakini wanafunzi wake ni wataalamu wa masuala ya
Katiba ambao ni Dk Mvungi na Profesa Kabudi ndiyo wameona hivyo.
“Hawa ni wazalendo. Huwezi ukahoji uzalendo wa Jaji Warioba, Jaji
Augustino Ramadhani, Joseph Butiku, Dk Salim Ahmed Salim na wengineo.”
Utata Bunge la Katiba, NEC
Lipumba amesisitiza kuwa hata Bunge hilo likiendelea na vikao vyake,
bado Katiba ya wananchi haitapatikana kwani haitakuwa na maridhiano ya
kisiasa.
“Waziri wa Sheria na Katiba wa Zanzibar, Abubakar Bakari hayumo
katika Bunge Maalumu, unajadili vipi Katiba? Huwezi kupata Katiba bila
maridhiano ya kisiasa ya Wazanzibari, hakuna maridhiano ya kisiasa. Kwa
hiyo, tunataka mchakato usitishwe,” alisema.
Kwa upande mwingine, Profesa Lipumba alisema kuna mikanganyiko mingi
katika Bunge hilo pia kukiwa na utata wa kufanyika kwa kura ya maoni
kutokana na maandalizi hafifu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
“Tume ya Uchaguzi ilivyo sasa, hata Daftari la Wapigakura wanasema
hawana, wameshafuta vitambulisho vya kupigia kura. Wanasema wataliandaa
ifikapo Septemba wakati hadi tufikie kwenye Uchaguzi Mkuu 2015 tuna
mwaka mmoja,” alisema.
Aliongeza: “Halafu wanachanganya mambo, leo utasikia mwenyekiti wa
Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta anakutana na jamii ya wafugaji.
Kwamba wafugaji hawamo kwenye rasimu?
“Tunafahamu Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeeleza katika ripoti zao
kwamba mambo hayo yote walikuwa nayo, lakini hawakuyaweka kwa kuwa hii
ni Katiba ya Muungano.
Rais Kikwete msahaulifu
“Mambo ya ardhi, serikali za mitaa hayakuwekwa. Sasa, utaletaje mambo
ya Tanzania Bara yaamuliwe na Wazanzibari wakati wana Katiba yao? Hata
ile mantiki iko wazi tu,” alisema Profesa Lipumba.
Rais Kikwete msahaulifu
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba alisema Rais Jakaya Kikwete
ameshindwa kusimamia ahadi zake, hali inayochangia kupwaya kwa utawala
wake.
Akifafanua hoja yake, mwanasiasa hiyo alisema, “Katika hotuba yake ya
mwisho wa mwaka 2011 ambapo pia alianzisha mchakato wa Katiba, alisema
kutakuwa na kituo cha kufua umeme cha megawati 300, kutakuwa na
Kinyerezi (I) ya megawati 200, megawati nyingine 200 za makaa ya mawe
na uzalishaji wa umeme kwa upepo.
“Hadi sasa imeshapita miezi 36, hakuna hata kimoja alichomaliza
kukitekeleza, kituo cha kufua umeme cha Kinyerezi (I) kinaendelea
kujengwa.”
“Kwa jumla, Kikwete ameshapoteza dira ya maendeleo kwa kipindi cha
miaka tisa alichokaa madarakani, hivyo sioni cha kumshauri. Alisema
tangu Kikwete aingie madarakani, hakuwa na ajenda maalumu ya maendeleo,
ndiyo maana nchi imeendelea kuwa maskini.
“Kwa sasa, Rais Kikwete amebakiza muda wa mwaka mmoja, hakuna la
kutegemea. Kwanza, hakuwa na mtazamo au dira ya kufanikisha mambo, kwa
hiyo kwa mwaka huu mmoja huwezi kutegemea kuwa ataleta mabadiliko
makubwa,” alisema Profesa Lipumba.
Profesa Lipumba, akirejea utawala wa kiongozi wa serikali ya awamu ya
tatu, Benjamin Mkapa, alisema kuwa utawala wa Kikwete umeshindwa kuwa
na nidhamu ya fedha kiasi cha kuzorotesha uchumi.
“Ili uweze kusimamia maendeleo ya nchi yetu, ni lazima uwe na
matumizi mazuri ya fedha za umma na uwe na Serikali inayosimamia vizuri
matumizi na malengo yaliyowekwa,” alisema msomi huyo wa nyanja ya
uchumi.
“Rais Mkapa alikuwa na nidhamu ya utendaji wa Serikali kibajeti, kwa
sababu alikuwa akitumia bajeti ya fedha taslimu. Ilitumika kuleta
nidhamu kwa kuwa fedha zilizokuwapo, ndizo zilizotumiwa.
“Tatizo kubwa ambalo limejitokeza katika kipindi hiki… Bajeti kwa
ujumla wake, ule mgawanyo wa kila wizara haukuwa na mwongozo mzuri wa
nini Serikali itatekeleza. Tatizo hilo lilikuwa ni muhimu kwa awamu ya
mwanzo kuleta nidhamu katika matumizi ya ujumla yalingane na mapato,
lakini hilo jambo limeendelea mpaka leo.”
Ili kuondokana na umaskini nchini, Profesa Lipumba alishauri Serikali
kukubali kuwekeza katika huduma za jamii, zikiwamo elimu na afya huku
rasilimali nyingine zikifuata.
“Ukizungumzia mambo ya afya katika hotuba, si jambo utakalopigiwa
makofi, lakini ndilo jambo linalosababisha umaskini, yaani watoto na
kinamama kukosa lishe bora.
“Kwa takwimu za sasa, asilimia 42 ya watoto wa Tanzania wana
utapiamlo, wamedumaa. Kwenye ‘Big Result Now’ (Mpango wa Matokeo Makubwa
Sasa), sekta ya afya haimo, nimebaki nastaajabu,” alisema.
Huku akitaja utajiri wa dhahabu kama mojawapo ya rasilimali zilizopo
nchini, alisema Serikali haiko wazi katika mapato yake, badala yake
imejikita zaidi katika kodi ya bidhaa ndogo ndogo.
“Tumejaliwa kuwa na rasilimali za asili. Tuna dhahabu, lakini
ukisikiliza hotuba ya bajeti kila mwaka huwezi kusikia wakizungumzia
tumepata kiasi gani katika sekta ya madini. Tunarudi kule kwenye sigara
na bia na konyagi,” alisema.
“Tumegundua gesi, lakini hatuna mikakati inayoeleweka,” alisema.
. Kuna gesi imegunduliwa katika maji mafupi ndiyo hiyo ya Msimbati,
Mnazi Bay na Songosongo iliyoko kusini mwa Tanzania ambayo ilitakiwa
itumike kuzalisha megawati 300 za kuingiza gridi ya Taifa, lakini
haikufanyika.”
“Sasa kuna gesi ya kina kirefu… lakini ukiangalia mkataba wa mfano
ulioko kwenye tovuti ya TPDC, unasema Serikali itakuwa inapata asilimia
80 hadi 90. Lakini, mkataba halisi uliotolewa na (kampuni ya utafiti na
uchimbaji mafuta) Statoil, unaonyesha kuwa Serikali itapata chini ya
asilimia 50, hatuna uwazi katika mapato ya gesi,” alisema.
Aliongeza kuwa licha ya Kampuni za China kujenga bomba la gesi, bado
hata mikataba yake haiko wazi hata kwa wabunge ili waweze kuhoji.
Aliitaka Serikali kuweka mikakati endelevu ya kufaidika na gesi ikiwa
pamoja na kuihakiki ili kuhakikisha kuwa ina faida kwa Watanzania.
CHANZO: MWANANCHI: MOYO WETU UKAWA NI WAJUMBE 14
CHANZO: MWANANCHI: MOYO WETU UKAWA NI WAJUMBE 14
No comments:
Post a Comment