THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIADIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898Fax: 255-22-2113425 PRESIDENT’S OFFICE,STATE HOUSE,1 BARACK OBAMA ROAD,11400 DAR ES SALAAM.Tanzania.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
JK: Acheni woga na udhaifu wa kusimamia sheria
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka viongozi nchini kuacha woga na ulegevu katika kusimamia sheria za kulinda mazingira na vyanzo vya maji ambavyo ni namna ya uhakika ya kuwawezesha wananchi kuendelea kupata maji ya uhakika, safi na salama.
Aidha, Rais Kikwete amewataka watu wanaokopa fedha katika vyama vya ushirika vya akiba na mikopo kuhakikisha kuwa wanarudisha fedha hizo kwa wakati kwa sababu kushindwa kurudisha mikopo hiyo kwa wakati kunawarudisha nyuma wengine ambao pia wanahitaji mikopo hiyo.
Rais Kikwete amesema hayo jana, Ijumaa, Agosti 22, 2014 kwenye siku yake ya tatu ya ziara yake ya
kikazi katika Mkoa wa Morogoro ambako ametembelea, amekagua na kuzindua miradi ya maendeleo ya wananchi katika Wilaya ya Morogoro na Manispaa ya Morogoro.
Akizindua mradi mkubwa wa maji ambao umegharimiwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Changamoto za Milenia Tanzania (MCA-Tanzania) katika Manispaa ya Morogoro, Rais Kikwete aliwaambia viongozi wa Manispaa ya Morogoro na wengine nchini:
“Acheni ulegevu, acheni woga, kazi yenu haiwezi kutoa simulizi kwa sababu mamlaka yote ya kuzuia watu kulima na kujenga katika maeneo ya vyanzo vya maji mnayo. Yatumieni.”
Rais Kikwete ambaye pia alirudia ujumbe huo kwa viongozi kwenye mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Jamhuri aliwaambia viongozi hao:
“Shughuli za binadamu za kilimo na makazi haziwezi kuruhusiwa katika vyanzo vya maji. Acheni tabia hii ya kushindwa kusimamia sheria na kutumia mamlaka ambayo mnayo. Mkiendekeza tabia hii iko siku wananchi wa Morogoro mjini watakosa maji kabisa.”
Rais Kikwete alikuwa anajibu malalamiko ya awali ya uongozi wa Manispaa ya Morogoro ambao ulikuwa umemwomba Rais alitangaze eneo la Milima ya Uluguru na Bwawa la Mindu kuwa hifadhi za taifa kutokana na kuwa vyanzo vikuu vya maji kwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro.
“Hamna mtu wa kumnung’unikia. Kazi yake haiwezi kuwa kumsubiri Rais ili kumsimulia kuhusu haya. Najua mkichukua hatua wako wanasiasa ambao watajitia wanawatetea wananchi, lakini kwenye hili la kulinda vyanzo vya maji hakuna la msalie Mtume.Kama sehemu nyingine kama kule Kinole (Wilaya ya Morogoro) wameweza, nini kinawashinda nyie kuwaondoa watu kwenye vyanzo vya maji?”
Mradi huo wa Ukarabati wa Miundombinu ya Maji Safi katika Manispaa ya Morogoro ulioanza kujengwa mapema mwaka 2011 kwa gharama ya sh. bilioni 56 kutoka Serikali ya Marekani na kupitia MCA-Tanzania, utaongeza kiwango cha kupatikana kwa maji safi na salama kwa wakazi wa Manispaa kutoka mita za ujazo 29,000 hadi 33,000 kwa siku na kunufaisha maelfu ya wananchi.
Hata kama ni kweli kuwa mradi huo hautamaliza mahitaji yote ya maji kwa Manispaa ya Morogoro, ambayo ni mita za ujazo 39,400 bado zitawezesha upatikanaji wa maji kwa kiasi cha asilimia 85 kwa wakazi wa Manispaa hiyo na hivyo kuboresha maisha ya wakazi hao.
Rais Kikwete amewaomba wananchi wa Manispaa ya Morogoro na viongozi wao kutunza miundombinu hiyo na kuhakikisha kuwa maji yanaendelea kupatikana kwa wakazi wa Manispaa.“Tukifanya hivyo, hata hao waliotusaidia wataona kuwa tumewaheshimu.”
Mapema jana hiyo hiyo, Rais Kikwete alitembelea eneo la Kinole na kuzindua Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Kinole – SACCOS- ambacho kilindikishwa rasmi mwaka 2001 na mpaka sasa kimetoa mipoko ya kiasi cha Sh. bilioni nne kwa wanachama wake wapatao 1,700.
Rais Kikwete amekuwa kiongozi mkuu wa pili wa Tanzania kutembelea Kinole tokea Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambaye alitembelea eneo hilo mwaka 1961 na wananchi walionyesha furaha yao kwa ujio huo kwa kumsimika Rais Kikwete kuwa Chidukila, yaani chifu msaidizi wa eneo hilo.
Rais Kikwete aliwapongeza wananchi wa Kinole kwa kuendesha SACCOS yenye mafanikio makubwa na manufaa kwa wakulima wa eneo hilo ambao miongoni mwa mambo mengine huingiza sokoni kiasi cha fuso 10 za ndizi kila siku.
“Huu ni ukombozi kwenu. Haya ndio maisha bora kwetu kwa sababu hii mikopo ambayo mnapata msingeweza kuipata kwa mabenki. Benki hiyo rafiki wa masikini. Benki haikopeshi masikini, asiyekuwa nacho hapati kutoka benki.”
Rais Kikwete alihimiza kurudishwa kwa wakati kwa mikopo inatolewa na chama hicho akisisitiza kuwa wale ambao wanachelewesha kurudisha mikopo“wanawarudisha nyumba wenzao ambao nao wanataka mikopo.”
Rais Kikwete amekatisha ziara hiyo ya siku saba Mkoani Morogoro kwenda Arusha, Tanga na Dar Es Salaam kwa siku moja kwa shughuli nyingine za kitaifa. Ziara hiyo itaendeleo tena kesho, Jumapili, Agosti 24, 2014.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
23 Agosti,2014
Twitter Buzz
....
...
IMETOSHA!
Featured post
KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO
Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...
Tuesday, 26 August 2014
RAIS KIKWETE ASEMA, ACHENI ULEGEVU NA WOGA!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment