MAMBO YALIVYOKWENDA
WAZIRI Mkuu alipohisi kuwa baadhi ya mawaziri walikuwa wanaunga mkono
hoja ya Serikali ya Tanganyika,
(i) Alimwarifu Rais na kupendekeza ifanyike Semina kama mbinu ya kupinga
hoja hiyo. Hii ilikuwa hatua sahihi.
(ii) Alipaswa kumshauri Rais kuitisha kikao cha Baraza la Mawaziri, ili
wale watakiwe kuweka msimamo na mkakati wa pamoja wa kupinga hoja ya Serikali
Tatu. Hakufanya hivyo; lilikuwa kosa.
(iii) Baada ya Rais na mimi kusema na Wabunge, na kupinga hoja ya Utanganyika,
Waziri Mkuu alipoona kuwa mawaziri wahusika bado wanaendelea na msimamo wao,
angeitisha kikao cha Baraza la Mawaziri, ili mawaziri hao watakiwe kueleza
msimamo wao Serikali inayo kanuni ya msimamo wa pamoja wa Kabineti nzima.
Katika suala kubwa kama hili Waziri Mkuu, Msimamizi wa Shughuli za
Serikali Bungeni, akijua kuwa baadhi ya wenzake walikuwa wanaendelea kuunga mkono
hoja ya Serikali Tatu, alikuwa na haki na wajibu wa kudai kanuni hii ya msimamo
wa pamoja ifuatwe. Rais angetazamiwa kumuunga mkono. Lingekuwa jambo la ajabu
sana kama baada ya maagizo ya Kamati Kuu ya Chama, na Rais mwenyewe kuipinga
hoja ya Serikali Tatu Bungeni, angemgeuka Waziri Mkuu wake anayeendeleza
msimamo huo, na hivyo akamfedhehesha na kujifedhehesha yeye mwenyewe kwa
kukubaliana na msimamo wa mawaziri wapinzani.
(iv)(a) Kama mawaziri wapinzani wangeamua kubadili msimamo wao, Baraza
zima la Mawazili lingekwenda Bungeni na kupinga kwa pamoja hoja ya Utanganyika.
(b) Kama mawaziri wapinzani wangekataa kubadili msimamo wao, (na mimi siamini
kuwa angetokea hata waziri mmoja ambaye angefanya hivyo), basi ama mawaziri hao
wangejiuzulu na kueleza sababu zao, au Rais angewafukuza na kueleza kwa nini.
Angeteua mawaziri wapya wenye msimamo wa Chama, na Serikali ingekwenda Bungeni
mawaziri wake wale wakiwa na msimamo mmoja na mkakati mmoja wa kupinga hoja ya
Utanganyika.
Basi kama Wabunge wahusika wangeng'ang'ania hoja yao ijadiliwe, Serikali
ingeipinga kwa pamoja, ingeungwa mkono na wabunge walio wengi, wa Bara na
Visiwani, na hoja hiyo ingekufa kifo cha kawaida. Na huo ndio ungekuwa mwisho
wa ngoma hizi.
Viongozi wetu walijua hivyo. Wabunge wale, pamoja na wabunge wenye hoja
walijua hivyo: siyo kwamba Serikali ikipinga hoja haitapita; bali wote
waliamini na walitazamia kuwa Serikali itaipinga hoja ya Serikali Tatu, na hoja
hiyo haitapitishwa na Bunge.
Badala yake Serikali ikaamua kusarenda. Viongozi wetu waheshimiwa, kwa sababu
wanazozijua wao wenyewe, ambazo mpaka sasa hawataki au hawawezi kulieleza
Taifa, wakaona kuwa hoja ya Utanganyika haizuiliki; wakakubali kushindwa,
wakajitolea. Wakaamua kumshauri Rais wetu. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Jemadari Mkuu wa Majeshi yetu, aliyechaguliwa na Watanzania
akaapishwa kwa Katiba ya Nchi yetu na Msahafu wa Mwenyezi Mungu ailinde
Tanzania; wakamshauri akubali hoja ambayo wanafahamu kuwa ikitekelezwa,
itavunja nchi yetu.
Lakini viongozi wetu waheshimiwa baada ya kusarenda kwa aibu hivyo,
hawataki kukubali matokeo ya kusarenda kwao. Wanaendelea kutuongoza katika kikao
kile kile cha Bunge Waziri Mkuu huwezi ukamshauri Rais wako kupinga, halafu
baada ya siku chache tu, wewe, huyo huyo umshauri Rais huyo huyo kukubali hoja
hiyo, ambayo juzi tu ulimshauri na kumwomba kupinga, na akapinga; na bado
ukabaki na wadhifa wako.
Ama ushauri wako wa awali haukuwa sahihi, na wajibu wako ni kujiuzulu;
au ulikuwa sahihi, lakini ukashindwa kuutetea na wajibu wako ni kujiuzulu. Huwezi
kuendelea kuongoza Serikali. Ama umwachie Waziri Mkuu mwingine anayeweza kutetea
msimamo wa awali; au umwachie mwingine anayeweza kumpa Rais ushauri huu wa
pili. Wewe huyo huyo huwezi kushindwa kuutetea ushauri wako wa awali, halafu
umshauri Rais akubali ushauri ulio kinyume cha ule wa kwanza, na utazamiwe kuwa
huo sasa utautetea. Utakuwa Saulo aliyeona mwangaza akageuka kuwa Paulo!
Lakini hata yeye wale aliokuwa akiwatesa awali waliendelea kuwa na
mashaka naye kwa muda mrefu sana, mpaka akasaidiwa kwa miujiza ya Mwenyezi
Mungu. Katika siasa hatuwezi kutegemea miujiza hiyo. Lazima tuhukumu kwa
kutumia akili zetu za kawaida.
Ushauri wa pili, ambao ni kinyume cha ule ushauri wa kwanza, ulitakiwa
utolewe na Waziri Mkuu mwingine, baada ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu aliyetoa
ushauri wa kwanza. Hii ndiyo maana ya kuwajibika.
Kwa maana ya kwanza ya kujiuzulu, yaani maana ya kuacha kazi, Waziri Mkuu
hajajiuzulu, maana bado ana cheo hicho; hajakiachilia au kukisarenda. Lakini
kwa maana ya pili ya kujiuzulu: yaani maana ya kukata tamaa, na kukubali kuwa
Utanganyika hauzuiliki, na hoja ya Serikali Tatu haipingiki, Waziri Mkuu
alikwisha kujiuzulu zamani pale alipotishwa au alipoambiwa: 'Wenzake wale
wamekwisha kukubali kwamba hoja ya Serikali Tatu haizuiliki na wao wataiunga
mkono; na wewe usipobadili msimamo wako ukakubaliana nao utaachwa katika mataa:',
hakulazimika kusarenda - kutupa silaha chini.
Alikuwa na hiari ya kuendelea kutetea msimamo wa Chama; Maagizo ya
Kamati Kuu, na kauli ya Rais wake mbele ya Wabunge. Alikuwa na hiari ya kuwakumbusha
Wabunge waheshimiwa hotuba yake ya tarehe 30, Aprili, 1992; na msimamo wa Chama
chao kuhusu suala la Serikali Tatu. Alikuwa na hiari kuamua kuachwa katika
mataa. Hakufanya hivyo. Badala yake aliamua kusarenda. Aliacha msimamo wa Chama
na, Rais wake, akakubali msimamo wa Wabunge wenye hoja ya Utanganyika.
Huwezi kujiuzulu kwa maana hii ya kusalimu amri, kukubali kuwa
umeshindwa, halafu usilazimike kujiuzulu kwa maana ya kuiacha hiyo kazi
iliyokushinda. Ukisha kubwaga silaha lazima ukubali kuwa mateka. Waingereza
wana msemo: huwezi kula kekiyo kisha ukabaki nayo. Na akina mama wa Kiswahili
husema: Uliyataka mwenyewe, mambo ya kuolewa!
Kujiuzulu, kwa maana ya kuacha kazi, ni matokeo tu ya kujiuzulu kwa
maana ya kushindwa kazi. Kazi hii imekushinda, ondoka! Hiyo ndiyo maana ya
kuwajibika.
REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA (1994)
REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA (1994)
No comments:
Post a Comment