KIKAO CHA
PILI DODOMA 14:10:I993
Nilipokwisha kuhakikishiwa kuwa
sasa sera ya Serikali Tatu ndiyo sera rasmi ya Bunge la Muungano na Serikali ya
Muungano, nilijaribu kupata maelezo kutoka kwa viongozi wetu; lakini
sikufanikiwa. Waziri mkuu nilipomuuliza kama kweli wamebadili sera, alicheka
tu!
Nilikuwa na safari ya kutembelea
nchi za Asia kwa ajili ya shughuli zinazotokana na uenyekiti wangu wa Tume Nchi
za kusini. Niliporudi kutoka safari nilijaribu tena kuonana na viongozi wetu
ili nipate maelezo lakini sikufanikiwa kumpata kiongozi yeyote mhusika.
Nilipopata habari kwamba Halmashauri
Kuu ya Taifa itakutana Dodoma, nilihisi kuwa bila shaka viongozi wetu wataeleza
kwa nini wameacha msimamo wa Chama na maagizo ya Kamati Kuu ya kupinga hoja ya
Utanganyika, wakaamua kukubali hoja hiyo.
Basi nikaomba angalau nipatiwe
nafasi nihudhurie kikao hicho cha Halmashauri Kuu ya Taifa, ili nami nisikie
maelezo watakayotoa. Baada ya maajabu ambayo haina maana kuyaeleza,
nilikubaliwa nikaenda Dodoma.
KIKAO CHA
FARAGHA
Safari hii tulikuwa na vikao
viwili. Kwanza kikao cha faragha wakiwapo viongozi wakuu wote wa Chama na
Serikali, na wengine wa nyongeza. Kilikuwa kikao kirefu na kigumu.
Sina kawaida ya kulizwa na mambo
ya siasa, lakini katika kikao hiki nilishindwa kujizuia kulia. Sikupata maelezo
ya maana ya kuwafanya watu wafanye walivyofanya. Nilipouliza kwa nini
hawakupinga hoja ya Serikali tatu kama tulivyokuwa tumekubaliana, majibu ya
viongozi wetu Wakuu yalikuwa ni ya ajabu kabisa. Ati wabunge wenye hoja baada
ya kuonana na mimi Msasani walikwenda Bungeni wakiwa wakali kama mbogo! Tena
walikuwa wakiwatukana wenzao (yaani wabunge wa Zanzibar), kwa kuwataja majina.
Hizi ni sababu za ajabu sana za
kuwafanya viongozi watu wazima watekeleze msimamo mzima wa Chama chao na
makubaliano ya watu makini kuutetea msimamo huo, na waamue kuikumbatia hoja ya
mbogo wakali! Huu ni uongozi wa ajabu kabisa!
Nilipowabana zaidi niliahidiwa
kuwa maelezo mazuri yatatolewa kesho yake na waziri wa Sheria na mambo ya
katiba katika kikao cha Halmashauri Kuu ya taifa.
KIKAO CHA
HALMASHAURI KUU:
Hakika siku ya pili yake
waligawiwa ‘TAARIFA YA SERIKALI JUU YA AZIMIO LA BUNGE KUHUSU HAJA YA KUUNDA
SERIKALI YA TANGANYIKA NDANI YA MUUNDO WA MUUNGANO’. Taarifa yenyewe ni ndefu
ina maelezo mengine ya mapambo tu, au ya kiini macho. Lakini vipengele
vinavyohusika na suala lenyewe vilikuwa vichache na nimevinukuu kwa ukamilifu.
9. “Tarehe 30 Julai, 1993 wakati
wa mkutano wa bunge la bajeti ukiendelea, zaidi ya wabunge 50 kwa pamoja
walitoa taarifa ya kusudio la kuwasilisha hoja Bungeni ambayo inadai, miongoni
mwa mambo mengine;
Kwa kuwa kuendelea mfumo huu wa
Muungano usiowaridhisha wananchi wengi wa upande mmoja ni kuhatarisha kuendelea
na kudumu kwa Muungano na pia kuathiri uelewano kati ya watu pande zote mbili;
na
Kwa kuwa uwezekano wa kuunda
serikali moja ya Jamhuri ya Muungano kwa nchi nzima kwa mambo yote
haujajionyesha;
Hivyo basi wabunge hawa
wanaliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano katika mkutano wake wa kumi na mbili
unaofanyika Dar es salaam liazimie kwamba;
Serikali ya Jamhuri ya Muungano
ilete Muswada Bungeni, kabla ya Februari 1994, kurekebisha Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ili kuwezesha uundaji wa “Serikali ya Tanganyika” ndani ya Muungano.
Tarehe 12 Agosti, 1993 hotuba ya
kuwasilisha Makadirio ya Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba ilisomwa Bungeni.
Katika hotuba hiyo Serikali ilieleza kusudio la kuandaa Waraka wa Serikali
(White Paper) kutafuta maoni ya wananchi kuhusu muundo wa Muungano. Tarehe 20
Agosti, 1993 wabunge wahusika waliwasilisha taarifa nyingine inayobadilisha ile
hoja ya awali iliyosambazwa kwa wabunge wote. Hoja mpya ilikuwa inalitaka Bunge
zima liazimie kwamba:
Serikali ya Jamhru ya Muungano
iandae kura ya maoni ambayo itafanyika kabla ya 31 Desemba, 1994 ili kupata
maoni ya wananchi wa Tanzania juu ya kuundwa kwa “Serikali ya Tanganyika” ndani
ya Muundo wa Muungano utakaozingatia mabadiliko hayo. Kutokana na taarifa hizi,
Baraza la Mawaziri lilifanya kikao cha dharura ili kutafakari taarifa hizi na
athari zake kama zingewasilishwa Bungeni na kupigia kura.
Kwanza kabisa, inaonekana kwamba hoja
ya awali ingekuwa vigumu kutekelezeka kutokana na muda mfupi uliowekwa kufikia
Februari, 1994, na pia haikutoa fursa kupata maelekezo ya Chama wala serikali
zetu mbili kushauriana. Kwa kutambua kwamba Bunge linafanya maamuzi yake kwa
njia ya kura baada ya mijadala ya wazi, Serikali iliona kwamba hoja yoote kati
ya hizi ingewasilishwa Bungeni, ingeweza kuligawa Bunge, kukigawa chama chetu
na kuwagawa wananchi katika suala zito kama hili la Muundo wa Muungano.
Kuhusu suala la kura ya maoni,
serikali iliona kwamba utekelezaji wake ni sawa na kufanya uchaguzi mkuu, jambo
ambalo ni la gharama kubwa. Aidha, kwa kuzingatia kwamba kura ya maoni kupigiwa
suala linalohitaji jibu la ‘NDIYO’ au ‘HAPANA’ , ni vigumu kupata swali lililo
wazi kwa wananchi ambao hawana uzoefu wa utaratibu huo wa kura ya maoni.
Pamoja na hayo, kwa kuzingatia
kwamba uamuzi wa kura ya maoni ni lazima ukubalike katika sehemu zote mbili za
Muungano, itakuwa vigumu kupata uwiano wa kura utakaokubalika pande zote mbili
kuwa ndio kiwango cha uamuzi.
10. Pamoja na juhudi za Serikali
rote mbili kupitia Kamati ya Pamoja, Serikali zetu pia zilifikia makubaliano na
kufanya maamuzi kuhusu baadhi ya matatizo mazito yaliyokuwapo katika Muungano
wetu. Maamuzi hayo ni:
(a) Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
kukubali Zanzibar kujitoa katika uanacharna wa 'OIC';
(b) Utaratibu wa kumpata Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano uwe ni kwa njia ya kupigiwa kura kwa pamoja na
mgombea urais (running mate).
11. Kwa msingi huu na kwa
kuzingatia maamuzi ya awali ya Serikali ya kutaka kupata maelekezo ya chama na
maoni ya wananchi kuhusu muundo utakaotatua matatizo ya Muungano, Serikali
iliona kuna umuhimu wa kushauriana na wabunge waliohusika ili kupata muafaka wa
maudhui ya hoja yenyewe. Muafaka huo ulifikiwa katikaKikaochaKamati ya Wabunge
wakikaa kama Kamati ya Chama tarehe 2218/93. Kutokna na muafaka huo, hoja ya
wabunge ilirekebishwa na azimio la Bunge kupitisha kwa kauli moja kwamba:
"Selikali iandae na
kusimamia utaratibu utakaoshirikisha wananchi na taasisi mbali mbali ili
kufikisha Bungeni kabla ya Aprili, 1995, mapendekezo ya muundo muafaka wa
Muungano ambao utazingatia haja ya kuwapo Selikali ya Tanganyika ndani ya Muungano
pamoja na mambo mengine.
12. Azimio hili linaagiza mambo
mawili yaliyo wazi:
(a) kupatikana kwa muundo muafaka
wa Muungano ambao unazingatia haja ya kuwapo Serikali ya Tanganyika.
(b) Kuwapo na utaratibu wa
kushirikisha wananchi na taasisi mbalimbali utakaosimamiwa na Serikali kabla ya
mapendekezo ya mwisho kufikishwa Bungeni.
13. Kwa kuwa suala la muundo wa
nchi ni zito na ni la kikatiba, ushirikishwaji wa wananchi ni jambo lisiloweza
kuepukwa. Aidha kwa uzoefu wetu na hali halisi ya nchi yetu, ni lazima
utaratibu wo wote utakaokubalika, uwezeshe Serikali ya Jamhuri ya Muungano
kushauriana na Chama na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
REJEA:
NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA
No comments:
Post a Comment