Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM (hayati) Horace Kolimba akisalimiana na (hayati) Baba Mtakatifu Papa John Paul II wakati kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani alipozuru nchini Tanzania Oktoba 1990.
Kosa kubwa la Rais (na ni kosa kubwa), ni kule kukubali kushirikishwa
kosa, badala ya kuwafukuza wale waliomshauri ashiriki kosa lao. Waziri Mkuu
aliposhindwa kupinga hoja ya Utanganyika alipaswa kujiuzulu; lakini
aliposhindwa kufanya hivyo, na badala yake akamshauri Rais naye akubali kuwa
geugeu, Rais angemfukuza pale pale na kuteua Waziri Mkuu mwingine. Rais
hakufanya hivyo; na badala yake Rais naye akakubali kweli kuwa geugeu na
kushiriki kosa la washauri wake.
Lakini kosa hilo la Rais, pamoja na ukubwa wake wote, haliwezi kufuta
kosa la awali la washauri wake na hoja ya kuwataka wawajibike kwa kosa hilo. Na
sasa wanalo kosa la nyongeza Ia kumfikisha Rais katika hali ngumu na ya
fedheha; na kuiingiza nchi yetu katika mabishano ya chuki zinazoweza kuigawa.
Pengine inafaa niseme kwamba inashangaza na kutisha kidogo kuona kuwa kujiuzulu
kwa Waziri ye yote kunafanywa kuwa ni jambo la kuvutana au kubembelezana. Ndugu
Ali Hassan Mwinyi aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya
Muungano. Makosa fulani yalifanyika katika Wizara yake. Hakuwa ameyafanya yeye;
yalikuwa yamefanywa na watendaji fulani walio chini ya Wizara yake. Alilazimika
kubeba lawama, akajiuzulu. Nadhani kuna wengine waliolazimika kujiuzulu
kutokana na mkasa huo huo.
Wala kubadili Waziri Mkuu si jambo la ajabu. Ndugu Rashidi Mfaume Kawawa
alikuwa Waziri Mkuu wangu kwa muda mrefu. Hakuwa amefanya kosa lolote; lakini
nilitaka kumbadili na kuteua Waziri Mkuu mwingine. Nilimwita, nikamwambia
hivyo. Tukakaa pamoja, mimi na yeye, tukashauriana na kukubaliana ni nani
anafaa kushika nafasi yake. Nikamteua hayati Edward Moringe Sokoine: Najua kuwa
watu wa aina ya Rashidi Kawawa ni adimu sana duniani, hawazaliwi kila siku;
lakini hata hivyo ni jambo la kushangaza kidogo kwamba viongozi wetu wa
Mageuzi, hata bado hatujafa, wanaona kuwa ni kosa kuwakumbusha kuwa vyeo
walivyo navyo ni dhamana. Wanadhani kuwa uwaziri ni usultani: ukisha kuwa
sultani utakufa sultani! Nadhani wanakosea.
Nchi hii imewahi kung'oa masultani wa kila aina. Tukianza kuvumilia
masultani wa kuchaguliwa tutapanda mbegu ya masultani wa kuzaliwa.
Narudia: kumbadili Waziri, hata Waziri Mkuu, si jambo la ajabu. Anaweza
kujiuzulu, anaweza kufukuzwa, na nchi isitikisike. Lakini huwezi kumtikisa Rais
wa nchi bila kuitikisa nchi yenyewe. Ni vizuri jambo hili likatamkwa wazi wazi
na likaeleweka sawa sawa. Maana watu wengine wananong'ona nong'ona kuwajibika
kwa Rais kana kwamba ni jambo la mchezo mchezo tu. Kulazimika
kumchukulia hatua Rais wa nchi ni mkasa na balaa kwa nchi yoyote ile. Ndiyo
maana tunatakiwa kuwateua na kuwachagua marais wetu kwa uangalifu mkubwa; na
ndiyo maana wakisha kuchaguliwa, wanatakiwa wajiheshimu na kuwa waangalifu sana.
Ni jambo muhimu kabisa, kwa kweli la kufa na kupona, kufanya kila jitihada ili
kujenga na kuimarisha utaratibu na mazoea ya kuchagua na kubadili Rais wa Nchi
yetu kwa njia ya kupigiwa kura, baada ya Rais anayetoka kumaliza kipindi chake
kimoja au viwili kwa mujibu wa Katiba. Utaratibu mwingine wo wote haufai, na ni
lazima tufanye kila lililo ndani ya uwezo wetu kuuzuia. Mnapolazimika kuutumia,
ni jambo la kufanyaje, si jambo la kurukia.
Katika suala hili Iililotufikisha hapa tulipo, watu wa kuwajibika ni Waziri
Mkuu, kwa sababu zilizoelezwa kwa kirefu kabisa; na Katibu Mkuu wa CCM kwa
sababu hizo na zaidi, maana yeye ndiye aliyekuwa Kiongozi na Mchochezi wa chini
chini wa hoja ya Utanganyika. Waziri Mkuu alisarenda ili wenzake, wakiongozwa
au kuchochewa na Katibu Mkuu, wasije wakamwacha katika mataa.
Waheshimiwa wawili hawa walikwisha kuambiwa kuwa watamsaidia Rais wao
kama wakijiuzulu. Aliyewaambia ni mimi, kwa niaba ya Rais. Katika kikao cha
mwisho nilichofanya na Rais kabla ya kuondoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam,
nilimwarifu kuwa nimeufikisha ujumbe wake kwa Washauri wake waheshimiwa.
Nilimwambia kwa mdomo na kwa maandishi, kwamba nilihisi kuwa viongozi hao
watafanya mshikamano wa kukataa kujiuzulu. Kama watafanya hivyo, nilisema,
tatizo litakuwa lake. Lakini kwa sababu tatizo halitakuwa lake kama Ali Hassan,
bali litakuwa lake kama Rais Mwinyi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mimi
kwa upande wangu sitakubali liishie hapo. Na kama nilivyohisi, kweli walifanya
mshikamano na mkakati wa kukataa kujiuzulu na Rais akawakubalia! Nimeambiwa
kuwa ama wao wenyewe au wajumbe wao, walitoa kwa Rais sababu mbili kubwa "za
kukataa kujiuzulu”:
(i) Kwanza, Waziri Mkuu akijiuzulu katika hali hii, na Rais akalazimika
kuteua Waziri Mkuu mwingine kwa kufuata Katiba ya sasa, ati Wabunge, hasa wale
"55" watakataa kumpa kibali Waziri Mkuu mpya huyo! Wabunge hawa sasa
wanatumiwa kama chaka la kufichia madhambi ya kila mila! Mimi katika ujinga
wangu nilidhani kuwa tatizo moja la Rais katika uhusiano wake na Wabunge,
linatokana na kutokuwa na Waziri Mkuu aliyechaguliwa kwa utaratibu mpya; na
akapata kibali cha Wabunge.
Kumbe Rais akijaribu kusahihisha hali hii ya sasa, ili achague Waziri
Mkuu atakayetaka kibali chao, Wabunge hao hao, hasa "Kikundi cha 55",
watamgomea kwa kutaka kuwaondolea Saulo wao aliyekwisha kuona mwangaza!
Naendelea kuwa Toma!
(ii) Sababu ya pili ya kukataa kujiuzulu: Waheshimiwa wahusika
waliyanong'oneza Magazeti, na Magazeti yakatangaza, kwamba ujumbe wa
kuwanong'oneza wajiuzulu ulifikishwa kwao na Mwalimu Nyerere: ati wakijiuzulu,
itaonekana kuwa Mwalimu Nyerere anaendesha nchi kichini chini kutoka Butiama.
Mtu ye yote aliyesoma maelezo haya mpaka hapa atatambua kuwa sikuwa na
sababu ya kusita kwenda kuwanong'oneza waheshimiwa hawa ujumbe wa Rais. Nataka
wajiuzulu, kwa sababu nilizozieleza. Katika masuala ya nchi mimi si mpole kama
Rais Mwinyi, ndiyo maana tulikubaliana nikamfanyie kazi hiyo. Lakini kisiasa
mtu mbaya wako hakunong'onezi kujiuzulu: hupiga baragumu! Pengine
anayekunong'oneza kujiuzulu anakutakia mema, na unaweza kujidhuru mwenyewe kwa
kufanya ukaidi.
Inawezekana kabisa kwamba Ndugu AIi Hassan Mwinyi, Waziri wa Mambo ya
Ndani aliponong'onezwa alijiuzulu hakushangilia. Lakini sina hakika kama
angekuwa hapo alipo leo, kama baada ya kunong'onezwa hivyo angetafuta hila za
kutojiuzulu. Nchi yetu bado changa; bado inajenga misingi na mazoea
yatakayowaongoza viongozi wetu katika kutuongoza, na wananchi wetu katika
kuwahukumu viongozi wao. Jitihada za kujaribu kusaidia kujenga maadili ya viongozi
wetu lazima ziendelee.
Waziri Mkuu si mpishi wa Rais, hala tuseme kuwa maadamu Rais mwenyewe
anayapenda mapishi yake, sisi wengine tusipoyapenda si kitu. Waziri Mkuu ni
Mpishi Mkuu wa Tanzania nzima. Kama hatupendi mapishi yake, au kuanza
kutupakulia vyenye sumu, au kachoka, au kashindwa kupika, ni wajibu wetu
kumwambia mwajiri wake ateue mpishi mwingine.
Narudia: sababu peke yake nilizoambiwa za kutojiuzulu kwa viongozi
wahusika ni hizo mbili nilizozitaja. Lakini sikusikia wala sijasikia kwamba ama
wao wenyewe au wajumbe wao, walimwambia Rais kuwa hawastahili kujiuzulu au
kufukuzwa ikiwa watakataa kujiuzulu. Na hilo ndilo muhimu; mengine yale ni hila
tu za kuwatia watu kiwi na kiinimacho.
REJEA:
NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA (1994)
No comments:
Post a Comment