Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday, 18 August 2014

MAELEZO KWA UMMA KUHUSU UDHIBITI WA VYAKULA VILIVYOONGEZWA VIRUTUBISHI

MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA

MAELEZO KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU UDHIBITI WA VYAKULA VILIVYOONGEZWA VIRUTUBISHI UKUMBI WA IDARA YA HABARI MAELEZO, TAREHE 18 AGOSTI, 2014


Wakurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo,
Ndugu Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana.

Napenda kwa heshima na taadhima kutumia fursa hii kwa niaba ya Menejimenti ya TFDA na wafanyakazi wote kwa ujumla kuwakaribisha katika mkutano huu. Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ni taasisi iliyopo chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambayo imeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura ya 219. Pamoja na mambo mengine, TFDA imepewa jukumu la kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti usalama wa vyakula.
Ndugu wanahabari,
Upungufu wa vitamini na madini ni mojawapo ya matatizo makubwa ya kilishe yanayoathiri afya ya watoto na wanawake walio katika umri wa kuzaa duniani kote. Kwa Tanzania, upungufu mkubwa upo katika vitamini “A”, madini chuma na madini joto. Upungufu wa virutubisho hivyo una uhusianio na kuwepo kwa upungufu wa vitamini na madini mengine muhimu kwa binadamu kama vile foleti (folate), naiacini (niacin), thiamine, riboflavin, zinki, chokaa na seleniam.
Baadhi ya madhara yanayosababishwa na upungufu wa viini lishe hivi ni pamoja na kutoona vizuri, uharibifu wa macho, watoto kuzaliwa wakiwa na uzito pungufu, kuwa na uwezo mdogo wa ubunifu na umakini, ulemavu, kudumaa, upungufu mkubwa wa damu, kinga ya mwili kupungua na kuongezeka kwa madhara ya magonjwa nyemelezi yanayoambatana na VVU/UKIMWI.
Takwimu za kitaifa juu ya Idadi ya Watu na Utafiti wa Afya (Demographic and Health Survey) za mwaka 2010 zinaonesha kuwa hapa nchini upungufu wa vitamin “A” unaathiri 33% ya watoto walio chini ya miaka mitano, 37% ya wanawake walio katika umri wa kuzaa. Aidha, upungufu wa madini chuma unaathiri 59% ya watoto wadogo, takribani 41% ya akina mama wajawazito na pia karibia 7% ya watanzania wote.
Kwa vile imekuwa ni vigumu kubadili tabia za ulaji wa watu ili kula vyakula vyenye vitamini na madini hayo muhimu kama maziwa, nyama, samaki, mayai, matunda na mbogamboga; Serikali imekuwa na mikakati mbadala ya kutatua tatizo hili kama vile utoaji wa matone ya nyongeza ya vitamini “A”, madini chuma na foliki asidi kwa watoto na akina mama wajawazito, kuhimiza uzalishaji bora wa vyakula na kutoa elimu ya lishe. Aidha, programu ya kitaifa ya urutubishaji (uongezaji) wa vitamin “A” kwenye mafuta ya kula, na uongezaji wa madini chuma, zinki, vitamini ya foleti na vitamini “B12” kwenye unga wa mahindi na ngano imeanzishwa.
Ndugu wanahabari,
Katika kufanikisha Mpango wa Kitaifa wa Urutubishaji Vyakula, TFDA pamoja na mambo mengine imepewa jukumu la kudhibiti ubora na usalama wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi kwa lengo la kulinda afya ya walaji kwa kutekeleza majukumu yafuatayo:-
1. Uratibu wa Kanuni za Uongezaji Virutubishi kwenye vyakula
Mamlaka imeandaa Kanuni za Uongezaji Virutubishi kwenye Vyakula {Tanzania Food, Drugs and Cosmetics (Food Fortification) Regulations, 2011} Kanuni hiyo iliidhinishwa na Waziri na kuchapisha kwenye Gazeti la Serikali la tarehe 27/06/2011 kwa GN No. 205 na tayari imeanza kutumika.
2. Kuandaa miongozo ya udhibiti wa ubora na Usalama wa Vyakula vilivyoongezewa virutubishi.
a. Miongozo ya wasindikaji
Ili kuwajengea uwezo wasindikaji kuweza kutekeleza matakwa ya Kanuni za Uongezaji Virutubishi kwenye vyakula pamoja na kufanya uhakiki wa ubora na usalama wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi, Mamlaka imeandaa miongozo ya wasindikaji kama ifuatavyo:
(i) Mwongozo wa Uhakiki wa Ubora na Usalama katika Usindikaji wa Mafuta ya Kula yaliyoongezwa Virutubishi
(ii) Mwongozo wa Uhakiki wa Ubora na Usalama katika Usindikaji wa Unga wa Mahindi ulioongezwa Virutubishi.
(iii) Mwongozo wa Uhakiki wa Ubora na Usalama katika Usindikaji wa Unga wa Ngano ulioongezwa Virutubishi
b. Mwongozo wa Wakaguzi
Ili kurahisisha usimamizi wa Kanuni za uongezaji virutubishi, Mamlaka imeandaa Mwongozo wa Ukaguzi wa Vyakula vilivyoongezwa virutubishi ambapo pamoja na mambo mengine, Mwongozo huu umeanisha taratibu za kufuata katika udhibiti wa vyakula viliyoongezwa virutubishi.
3. Kutoa mafunzo kwa wadau muhimu kuhusu uhakiki na udhibiti wa ubora na usalama wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi.
i. Mafunzo ya wataalamu kutoka katika viwanda vinavyooongeza virutubishi kwenye vyakula
Mamlaka imetoa mafunzo kwa wataalamu 18 kutoka katika viwanda vikubwa vinavyoongeza virutubishi kwenye vyakula.
Vilevile kwa kushirikiana na wadau wengine kama Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) na ‘Tuboreshe Chakula’, Mamlaka imetoa mafunzo kwa jumla ya wasindikaji wadogo wa vyakula 350 kutoka katika Halmashauri za Kilolo, Iringa Vijijini, Njombe Mjini, Babati, Bahi, Mvomero na Morogoro Mjini ambazo zinahusika katika mpango wa majaribio wa uongezaji virutubishi kwenye unga wa mahindi unaosindikwa na wasindikaji wadogo na wale wa kati. Mafunzo hayo pamoja na mambo mengine yalihusu Kanuni Bora za Usindikaji Vyakula ikiwa ni pamoja na uhakiki wa ubora na Usalama wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi.
ii. Mafunzo ya wakaguzi
Mamlaka imetoa mafunzo kwa jumla ya wakaguzi 270 kutoka katika halmashauri zote za Tanzania Bara. Mafunzo haya yalifanyika kwa lengo la kuwapa ujuzi wakaguzi kuhusu namna ya udhibiti wa ubora na usalama wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi.
4. Kusambaza vitendea kazi vinavyotumika katika uhakiki na udhibiti wa ubora na usalama wa vyakula
Mamlaka imefanya warsha ya ugawaji wa vitendea kazi vinavyotumika katika uhakiki na udhibiti wa ubora na usalama wa vyakula kwa wawakilishi wa viwanda vinavyosindika vyakula vinavyoongezwa virutubishi na wakaguzi kutoka katika vituo vya forodha Tanzania. Wawakilishi hawa walipewa vitendea kazi kulingana na mahitaji ya maeneo yao wanayo yawakilisha. Vitendea kazi vilivyosambazwa ni, Kanuni, Miongozo na vifaa vya ukaguzi (field test kits)
5. Kusimamia utekelezaji wa Kanuni za Uongezaji wa Virutubishi kwenye Vyakula.
a. Ukaguzi
Mamlaka imetekeleza suala la usimamizi wa Kanuni za Uongezaji virutubishi kwenye vyakula kwa kufanya yafuatayo:-
(i) Kufanya marekebisho ya usajili wa unga wa ngano na mafuta ya kula yanayosindikwa na viwanda vikubwa baada ya wasindikaji wa vyakula husika kukidhi viwango vilivyowekwa. Hadi hivi sasa vyakula vyote vinavyosindikwa na viwanda 12 vilivyopo kwenye mpango wa Kitaifa wa Uongezaji Virutubishi vimesajiliwa na TFDA.
(ii) Mamlaka pia imeweka utaratibu wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika viwanda vyote vinavyosindika vyakula vilivyoongezwa virutubishi. Katika kaguzi zote hizi sampuli huchukuliwa kutoka viwandani kwa ajili ya kuhakiki ubora na usalama wake.
(iii) Kwa vyakula vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi, Mamlaka imetoa muda wa miezi sita wa kufanya maandalizi hadi kufikia 31 Desemba 2014 kwa waingizaji wa vyakula nchini kuhakikisha kuwa wanakidhi matakwa ya Kanuni za Uongezaji Virutubishi kwenye vyakula. Muda huu unawahusu pia wasindikaji wa ndani ambao hawamo katika Mpango wa Kitaifa wa Uongezaji Virutubishi. Lengo ni kutoa muda wa kufanya maandalizi yanayohitajika ambayo ni pamoja na kufunga mitambo ya uongezaji virutubishi (viwandani) na kufanya mawasiliano na wasambazaji wa vyakula husika kutoka nje ya nchi (waingizaji).
6. Ufuatiliaji wa ubora na usalama wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi kwenye soko.
Mamlaka imeandaa mpango wa ufuatiliaji wa ubora na usalama wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi kwenye soko. Mpango huu umeanza kutekelezwa kuanzia mwezi Aprili, 2014.

Ndugu wanahabari,
Pamoja na kuwa Kanuni za uongezaji wa Virutubishi haivihusu viwanda vidogo na vya kati kutokana na kutokuwepo kwa teknolojia muafaka ya uongezaji wa vyakula katika ngazi ya wasindikaji wadogo na wa kati, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, inafanya majaribio katika Halmashauri 6 za mikoa ya Iringa (Kilolo, Iringa Vijijini), Njombe (Njombe Mji) na Arusha (Karatu, Meru na Monduli) kuhusu uongezaji virutubishi kwenye unga wa mahindi unaosindikwa na wasindikaji wadogo. Kwa upande wa mafuta ya kula yanayozalishwa na wasindikaji wadogo majaribio yanafanyika katika Mkoa wa Manyara (Babati), Singida na Dodoma.
Ndugu wanahabari,
Kwa kuhitimisha, TFDA inatoa shukurani kwa ushirikiano ambao mmekuwa mkiuonesha katika kutoa taarifa za kiudhibiti pale inapotokea ikiwa ni pamoja na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kufanya maamuzi sahihi katika uchaguzi na matumizi ya bidhaa nyingine zinazodhibitiwa na TFDA ikiwa ni pamoja na dawa, vipodozi na vifaa tiba.
Asanteni kwa kunisikiliza!

No comments:

Post a Comment