Dodoma. Kamati za Bunge Maalumu, zimekamilisha kazi ya kujadili na kuchambua Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, huku ikiwa imefanyiwa mabadiliko makubwa tofauti na ilivyokuwa awali.
Wajumbe wanatarajiwa kuanza kukutana kama Bunge zima kuanzia Jumanne ijayo, Septemba 2, 2014 wakati kamati zitakaposoma taarifa zake baada ya kufanya uchambuzi wa sura 15 za Rasimu ya Katiba kwa zaidi ya wiki tatu, huku yakitarajiwa mabadiliko makubwa.
Mabadiliko yaliyofanywa yameondoa mambo makubwa yaliyokuwa yakiifanya rasimu hiyo kuonekana mpya, hivyo sasa baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaiona rasimu kama ‘Katiba ya 1977 iliyofanyiwa marekebisho.’
Mwelekeo wa kubadili karibu misingi yote muhimu iliyojengwa na tume iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba akiwa mwenyekiti, ilianza baada ya kuwekwa kando kwa mfumo wa muungano wa Serikali tatu uliopendekezwa na badala yake kurejea katika muundo wa sasa wa serikali mbili.
Uamuzi huo uliathiri mtiririko na muundo mzima wa sura na ibara za rasimu hiyo, kwani sasa wajumbe wa Bunge Maalumu walilazimika kutengeneza Katiba yenye mwelekeo wa serikali mbili na siyo tatu tena zilizokuwa zimependekezwa na tume.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad aliwahi kuliambia gazeti hili kwamba mwelekeo wa uchambuzi wa rasimu kwa sura hizo 15, lazima ufuate kile ambacho kamati zilikiamua katika uchambuzi wa awali wa sura ya kwanza na ya sita.
Miongoni mwa mambo ambayo yameachwa baada ya kurejesha mfumo wa serikali mbili ni muundo wa uongozi wa juu wa nchi hususan nafasi ya Makamu wa Rais, muundo wa Bunge la Jamhuri, kupunguzwa mamlaka ya Rais, uwajibikaji na uwajibishwaji wa wabunge na ukomo wa ubunge.
Kadhalika, habari kutoka ndani ya kamati zilisema suala la kuwekwa kwa maadili ya uongozi kwenye Katiba nalo lilizua mjadala mkali kutokana na baadhi ya wajumbe kutaka liondolewe kwa maelezo kwamba linapaswa litajwe kwenye sheria na siyo Katiba.
Mambo ya muungano
Miongoni mwa mambo ambayo kuna kila dalili kwamba yatabadilika ni Bunge Maalumu kuongeza mambo ya muungano kutoka saba yaliyopendekezwa na tume na huenda idadi yake ikazidi 22 yaliyomo kwenye Katiba ya sasa.
Uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa katika baadhi ya kamati za Bunge hilo na kuthibitishwa na baadhi ya wenyeviti wake, umebaini kuwa yapo mapendekezo ya mambo ya muungano kuongezwa, tofauti na mtazamo wa awali kwamba yangepungua kama moja ya njia za kuondoa kero za muungano.
Tume ya Jaji Warioba ilipendekeza mambo saba tu kwenye orodha ya muungano chini ya mfumo wa Serikali tatu, mfumo ambao hata hivyo ni dhahiri umeshawekwa kando na Bunge Maalumu na kurejesha muundo wa serikali mbili.
Mambo yaliyopendekezwa na tume hiyo ambayo yapo kwenye sura ya 17 ya Rasimu ya Katiba inayohusu masharti ya mpito ni pamoja na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Uraia na Uhamiaji.
Mengine ni Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa na Ushuru wa Bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
Mapendekezo hayo yaliyaacha nje mambo mengine 15 yaliyopo kwenye Katiba ya sasa ambayo ni polisi, mamlaka juu ya mambo yanayohusika na hali ya hatari, mikopo na biashara ya nchi za nje, utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, bandari, mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta na simu na leseni ya viwanda na takwimu.
Pia yamo elimu ya juu, maliasili ya mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta ya aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa na gesi asilia, Baraza la Taifa la Mitihani la Tanzania, usafiri na usafirishaji wa anga, utafiti, utafiti wa hali ya hewa na Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano.
Baadhi ya wenyeviti wa kamati za Bunge Maalumu wamesema kuna kila dalili kwamba baadhi ya mambo yaliyoachwa yatarejeshwa huku kukiwa na mtazamo kwamba mengine yanaweza kuongezwa kutoka nje ya orodha ya sasa.
Mwenyekiti wa Kamati Namba Tano, Hamad Rashid Mohamed alisema orodha iliyopo kwenye Rasimu ya Katiba ina upungufu mkubwa kwani imeacha mambo mengi ya msingi yenye sura ya muungano.
“Mathalani huwezi kuzungumzia kwamba usalama ni suala la muungano halafu ukaacha mambo ya anga, au ukaacha suala la mitihani, yaani Baraza la Mitihani limeachwa pia suala la utafiti nalo huwezi kuliacha, kwa hiyo orodha itaongezeka,” alisema Mohamed.
Mwingine ni Mwenyekiti wa Kamati Namba Sita, Stephen Wassira alisema kuna mambo mengi ya muungano yaliyotajwa kwenye Rasimu ya Katiba lakini hayako katika orodha iliyowekwa kama moja ya nyongeza kwenye rasimu hiyo.
“Ngoja nikwambie kwamba mambo hayo yataongezeka, hilo halina ubishi na kamati yangu tulijadili kidogo na kesho (leo) tutakutana kumalizia. Ukisoma vizuri ibara kwa ibara, utagundua kuwa kuna mambo mengi kama vile Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ambayo ni chombo cha muungano hata ukiangalia muundo wake,” alisema Wassira.
Alitaja mambo mengine kuwa mahakama ya juu inayopendekezwa kuanzishwa lakini haimo kwenye orodha pamoja na masuala ya elimu ya juu na utafiti.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Kamati Namba nne, Christopher Ole Sendeka alisema kuna kazi kubwa ya kutazama upya orodha ya mambo ya muungano na kwamba suala la usalama wa anga ni moja ya mambo hayo.
Naye Mwenyekiti wa Kamati Namba Moja, Ummy Mwalimu alisema, licha ya kwamba kamati yake haikujadili suala hilo lakini orodha hiyo inaweza kuongezeka kwani kuna mambo mengi yameachwa.
“Leo tulikuwa tunaangalia suala la fedha na kuna mambo ukichuguza humo yanagusa sehemu zote mbili, sisi hatukujadili sehemu hiyo kutokana na kwamba haikuwa kwenye orodha ya kazi tulizopewa ila nadhani tukipata fursa bungeni lazina mambo hayo yaangaliwe,” alisema Mwalimu.
Kamati nyingine ambayo haikujadili suala hilo ni namba tatu ambayo mwenyekiti wake, Dk Francis Michael alisema orodha ya mambo ya muungano iko kwenye sura ya 17 ambayo haikuwa sehemu ya kazi za kamati.
No comments:
Post a Comment