Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday 27 August 2014

MAGUFULI ADAI ANAWINDWA


NA JOHN MADUHU, MWANZA

WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ameibuka na kusema kuwa anawindwa na mahasimu wake kwa kumbeza baada ya Mahakama Kuu kuwaachia huru watuhumiwa wa kesi ya kuvua samaki katika Ukanda wa Uchumi wa Tanzania.
Amesema watu hao wanaongozwa na ajenda za siri kisiasa na si wazalendo.
Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, Dk. Magufuli alisema ameshangazwa na namna suala hilo linavyofanywa kisiasa zaidi, na kudai wapo baadhi ya watu wana malengo maalumu na kesi hiyo.
Alisema operesheni iliyofanyika ya kuwasaka wavuvi haramu waliokuwa wakivua samaki katika Ukanda wa Uchumi wa Tanzania katika Bahari ya Hindi, ilikuwa chini ya ushirikiano wa nchi za kusini mwa Afrika, ikiratibiwa na SADC na kuongozwa na Afrika Kusini.
“Nilipofanikiwa kukamata meli hii na wavuvi wake nilipongezwa, lakini leo nabezwa…, wakati nakamata nilikuwa Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, nilikuwa natimiza wajibu wangu kama msimamizi wa wizara,” alisema.
Alisema baada ya Wachina hao kukamatwa, suala lao lilipelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kisha kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kama taratibu zilivyo na watuhumiwa kufikishwa mahakamani.
“Awali walipofikishwa mahakamani walihukumiwa miaka 23 na mahakama iliagiza meli yao itaifishwe. Sikuwashtaki kama Magufuli, ni Jamhuri ndiyo iliyoshtaki na kushinda.
“Baada ya Wachina hao kuhukumiwa kutokana na kazi nzuri niliyoifanya, ambayo hata ninyi waandishi wa habari hamkunipongeza, ilikuwa kimya, leo hii watu wanaibuka na kuelekeza lawama kwangu baada ya Wachina kuachiwa huru na mahakama, mara Magufuli afukuzwe mara hivi, hizo ni siasa,” alisema.
Alisema kuwa awali Mwanasheria Mkuu wa Serikali alipopeleka kesi mahakamani Wachina hao walipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 23, lakini hakuonekana mbaya.
Akizungumzia meli ya MV Tawaliq 1, alisema ilitoka chini ya Wizara ya Uvuvi na kuwa katika uangalizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Alisema ikiwa chini ya uangalizi huo, iliibwa vifaa muhimu kabla ya kuzama, lakini hakuna ambaye amewahi kumuuliza Waziri wa Mambo ya Ndani kuhusu suala hilo.
“Mie kwa sasa si Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, nilitimiza wajibu wangu, na sasa hivi niko Wizara ya Ujenzi nikiendelea kuwatumikia Watanzania, malumbano ya kisiasa yasiyo na tija hayana nafasi kwangu, sitaki kuzungumza kwa undani hukumu ya kuachiwa hawa, watafuteni viongozi wa mahakama au ofisi ya AG na si Magufuli,” alisema.
Wiki iliyopita, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwaachia huru Wachina wa ‘samaki wa Magufuli’ na kuamuru Jamhuri iwarejeshee vitu vyao, ikiwamo meli ya Tawaliq 1.
Wachina hao waliachiwa kwa mara ya pili, kwani mara ya kwanza waliachiwa na Mahakama ya Rufaa Machi 28, mwaka huu, kabla ya kukamatwa tena na kushtakiwa upya kwa mashtaka hayo hayo yaliyofutwa.
Washtakiwa hao ni nahodha wa meli, Hsu Chin Tai na wakala wa meli hiyo ya Tawaliq 1, Zhao Hanquing, waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya uvuvi haramu katika Ukanda wa Uchumi wa Tanzania.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Prosper Mwangamila, aliwasilisha maombi ya kuifuta kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Isaya Harufani.
“Mheshimiwa hakimu, Jamhuri tunaifahamisha mahakama kwamba hatuna haja ya kuendelea na kesi dhidi ya washtakiwa, maombi yetu tunawasilisha chini ya kifungu cha sheria namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ya mwaka 2002,” alidai Mwangamila na kuwasilisha.

Wakili wa washtakiwa, Kapteni Ibrahimu Bendera, alikubaliana na maombi hayo na kuiomba mahakama iwarudishie hati zao za kusafiria, meli iliyokamatwa pamoja na samaki waliokuwamo ikiwezekana.
CHANZO: MTANZANIA

No comments:

Post a Comment