Dar es Salaam. Serikali imefanya mabadiliko makubwa ya wakurugenzi wanane wa Wizara ya Maliasili na Utalii akiwamo aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Wanyamapori, Paul Sarakikya ambaye amehamishiwa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri).
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na baadhi ya wakurugenzi waliohusika katika uteuzi huo, zinaeleza kuwa mabadiliko hayo yalifanyika hivi karibuni na barua za kutekeleza majukumu yao mapya walipewa juzi.
Hata hivyo, Waziri wa wizara hiyo, Lazaro Nyalandu alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema atalizungumzia Jumatatu ijayo.
Taarifa kutoka ndani ya wizara hiyo, zilieleza kwamba barua ya mabadiliko hayo imeandikwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais -Utumishi, George Yambesi.
Akizungumza na gazeti hili jana Yambesi alisema, “Taratibu za uteuzi wa wakurugenzi ndani ya wizara ziko wazi kwamba zinafanywa na katibu mkuu wa wizara hivyo (Maimuna Tarishi) hivyo naomba mtafuteni yeye.” Hata hivyo Tarishi hakuweza kupatikana kuzungumzia mabadiliko hayo.
Katika mabadiliko hayo, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa amepelekwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Afrika, Mweka na mkurugenzi mpya ameteuliwa kuwa Herman Keraryo aliyekuwa mkurugenzi msaidizi wa idara hiyo.
Aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Profesa Jafari Kidegesho amepelekwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua).
Dk Charles Mulokozi aliyekuwa Kaimu Mkuu Msaidizi Matumizi Endelevu Wanyamapori anabaki katika nafasi hiyo na Julius Kidede amepelekwa Ngorongoro kupangiwa majukumu mengine ya kazi.
Mkuu wa Kitengo Kidogo cha Migogoro cha Wanyamapori ameteuliwa David Kanyata na Faustine Masalu akiteuliwa kuwa Mkurugenzi Uzuiaji Ujangili nchini, awali alikuwa Mkuu wa Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Mashariki- Dar es Salaam.
Kwa upande wake Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa akizungumzia mabadiliko hayo, alisema kubadilishwa kwa wakurugenzi hao ni jambo zuri lakini haliwezi kuleta ufanisi endapo Ikulu itaendelea kuingilia utendaji wa wizara hiyo.
“Bado watendaji wa juu wanaingilia utendaji kazi wa wizara, katika hotuba yangu bungeni nilipendekeza wakurugenzi hao kuchukuliwa hatua jambo ni jema, lakini bado wizara hii ina matatizo lukuki ambayo ili kuyamaliza kunahitajika kufanyika kwa ushirikiano wa wadau wote,” alisema Msigwa ambaye ni Mbunge wa Iringa Mjini kupitia Chadema.
Akizungumzia uteuzi huo, Keraryo alisema ameupokea kwa furaha na kuahidi kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni zinavyomtaka kutenda.
“Nimejipanga kuendeleza mazuri aliyoacha(Profesa Songorwa), nitatekeleza majukumu yangu kwa kuzingatia kanuni na sheria na kama kutatokea mengine hiyo itakuwa nje ya uwezo wangu,” alisema Keraryo
Utekelezaji wa Operesheni
Mabadiliko haya yanatokea mwaka mmoja, tangu mawaziri wanne kung’olewa katika nafasi zao kutokana na Operesheni Tokomeza Ujangili kukumbwa na kashfa ya kukiuka haki za binadamu.
Mawaziri hao ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
Mbali na mawaziri hao, Kamati ya Bunge Desemba 22 mwaka jana ilipendekeza Serikali kuwawajibisha watendaji waliozembea kwenye Operesheni hiyo.
Mei 2 mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete aliunda Tume ya Uchunguzi, kuhusu vitendo vilivyotokana na Uendeshaji wa Operesheni hiyo.
Rais aliunda Tume hiyo kwa mujibu wa kifungu cha tatu cha Sheria ya Uchunguzi Sura ya 32.
Sakata lilivyoanza
Februari 24 mwaka huu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alitangaza kuubadili uongozi wa Idara ya Wanyamapori ya Wizara hiyo ikiwa ni utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati Teule ya Bunge ya kuitaka Serikali kuwawajibisha watendaji waliohusika na uzembe huo.
Nyalandu alisema Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Profesa Songorwa alitangaza kumwondoa katika nafasi hiyo kutokana na tuhuma za uzembe na ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Waziri huyo alimteua Paul Sarakikya kukaimu nafasi hiyo huku akimwondoa Profesa Jafari Kidegesho katika nafasi ya Mkurugenzi Msaidizi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori na kumteua Dk Charles Mulokozi kukalia kiti hicho.
Pia, alimteua Julius Kibebe kuwa Mkurugenzi Msaidizi Uzuiaji – Ujangili nafasi ya aliyekwenda kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Katika mabadiliko hayo, Nebbo Mwina aliendelea kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo, Utafiti na Takwimu huku Herman Keiraryo anaendelea kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji wa Wanyamapori.
Warudishwa kazini
Mei mwaka hu, agizo la Waziri Nyalandu la kuwasimamisha kazi vigogo hao lilitenguliwa baada wakurugenzi hao kurejeshwa katika nyadhifa zao.
Taarifa kutoka ndani ya wizara hiyo zilieleza kwamba watendaji wote waliokuwa wamesimamishwa kazi walirejeshwa na katibu mkuu wa Wizara hiyo, Maimuna Tarishi jambo lililozua mvutano baina ya Nyalandu na Tarishi kutokana na kupingana kwa maauzi.
Tutegemee utekelezaji mpya toka kwao.
ReplyDelete