Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi
Hatua za Serikali baada ya
aazimio na mapendekezo
14. Kutokana na Azimio la Bunge,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeona kwamba suala la muundo wa Muungano sasa
linahitaji kufanyiwa kazi na kupatiwa uamuzi haraka zaidi na hivyo ni muhimu
kuwasilishwa kwenye Chama mapema kwa maelekezo, bila kusubiri mapendekezo ya
Kamati ya pamoja ili kuondoa hisia kwamba Serikali inajaribu kulikwepa suala
hili.
15. Katika hali hii, Serikali
inapendekeza kwamba Halmashauri Kuu ya Chama iafiki pendekezo la Serikali la
kuandaa Waraka wa Serikali wa kutafuta maoni ya wananchi (White Paper) kuhusu
muundo muafaka wa Muungano kwa kuzingatia mambo yafuatayo:
(a) Dhana ya kuwa na Serikali
tatu ndani ya Muungano, yaani Serikali ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar na Serikali ya Tanganyika ikubalike. Muungano wa aina hii kwa Sheria
za Katiba na za Kimataifa ni wa Shirikisho (Federation).
(b) Kwamba muundo uwe ni Muungano
wenye Serikali tatu, yaani Serikali ya Muungano, Serikali ya Tanganyika na Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar. Ikumbukwe kwamba neno Muungano linavyofahamika kwenye
Sheria za Katiba na za Kimataifa linamaanisha kwamba majukumu yale ya msingi ya
dola yanahamishiwa kwenye Serikali ya Muungano."
Haya ni maelezo ya ajabu sana
kutoka kwa watu wazima kwenda kwa watu wazima wengine. "Kwanza
kabisa", Serikali yetu inaiambia Halmashauri Kuu ya Taifa,
"inaonekana kuwa hoja ya awali ingekuwa vigumu kuitekeleza kutokana na
muda uliowekwa kufikia Februari, 1994, na pia haikutoa fursa ya kupata
maelekezo ya Chama wala Serikali zetu mbili kushauriana.
Aidha, "Kwa kutambua kwamba
Bunge linafanya maamuzi yake kwa njia ya kura baada ya mijadala ya wazi wazi,
Serikali iliona kwamba hoja yo yote kati ya hizi ingewasilishwa bungeni
ingeweza kuligawa Bunge, kukigawa chama chetu na kuwagawa wananchi katika suala
zito kama hili la Muundo wa Muungano."
Kwanza, hii "hoja ya
awali" ambayo waheshimiwa hawa wanasema hawakuwa na muda wa kutosha
kuitekeleza ni ile ya kutaka Serikali Tatu, ambayo kwanza, ni kinyume na sera
ya Chama, pili, walikuwa wameagizwa na Kamati Kuu ya CCM siku chache zilizopita
wakaipinge Bungeni.
Tatu, tarehe 12 Agosti, 1993,
Selikali yenyewe ilikuwa imeliambia Bunge kwamba ilikuwa inaandaa waraka wa
kutafuta maoni ya wananchi kuhusu suala hili;
Na nne, (na pengine kutokana na
kauli hii ya Serikali), tarehe 20 Agosti, 1993, wabunge wahusika walikuwa
wamekwisha kuondoa hoja yao ya awali, nao wakaleta hoja mpya: ya kuitaka
Serikali ifanye referendamu ya kutafuta maoni ya wananchi.
Labda waheshimiwa wabunge nao
waliona kuwa hoja hii ya kudai Serikali tatu "ikiwasilishwa Bungeni,
ingeweza kuligawa Bunge, kukigawa Chama chetu; na kuwagawa wananchi katika
suala zito kama hili la Muundo wa Muungano." Mimi siamini hivyo; naamini
kuwa kama ingewasilishwa bungeni ili ijadiliwe, ingejadiliwa ikakataliwa na
mambo yakesha. Maamuzi yoyote ya kidemokrasia hayana budi yatokane na mjadala.
Bila ya mjadala, maamuzi, hata yaliyo muhimu kabisa, yatafanywa kwa nguvu hila.
Lakini kwa vyo vyote vile, hoja hii, Wabunge wahusika walikwisha kuiondoa.
Kama viongozi wetu waliamini kuwa
kujadiliwa kwake kutaleta mgawanyiko huo waliouhofu, kwa nini, basi, walitaka
kuitekeleza ila muda wa Wakati CCM ilipotaka kubadili sera yake itatafuta
kwanza maoni ya wananchi? Halmashauri Kuu ya Taifa iliketi Unguja ikabadili
Azimio la Arusha bila kwanza kutafuta maoni ya wananchi. Na walikuwa na haki
kufanya hivyo, maana sera ni yao. Ubaya wao ni kwamba jambo lenyewe walilifanya
kwa hila na 'janja janja", na mpaka sasa wanaendelea kudanganya wananchi
kwamba sera ya CCM bado ni Ujamaa na Kujitegemea.
Ndivyo viongozi wetu waheshimiwa
wanavyojaribu kufanya hata katika suala hili la Muungano. Wanataka kuvunja
Tanzania maana "wamechoka na Wazanzibari"; lakini hawataki kusema
hivyo wazi wazi. Wanachosema ni kwamba wanataka Serikali ya Tanganyika
"ndani ya Muungano", ingawa wanafahamu, maana si watu wapumbavu,
kwamba ukifufua Tanganyika utaua Tanzania.
Muundo wa Muungano, pamoja na
kwamba hatutaki uwe ukitibuliwatibuliwa mara kwa mara, ni suala la sera, si
amri ya Mungu. Vyama vya siasa mbalimbali vinaweza vikawa na maoni mbalinbali
kuhusu muundo unaofaa kwa Katiba ya nchi yetu. Muundo utakaokubaliwa na
wananchi walio wengi ndio utakaokuwa sehemu ya Katiba ya nchi yetu. Muundo wa
Serikali mbili unakubaliwa na wananchi, lakini unatokana na sera ya TANU na
ASP, na kwa sasa CCM. Chama Cha Mapinduzi kikipenda kinaweza kubadili sera hiyo
ya muundo wa Serikali mbili bila kuuliza wananchi kwanza. Kinaweza kufunyahivyo
kwa kuhisi kuwa hivyo ndivyo wananchi wengi watakavyo; lakini pia kinaweza
kufanya hivyo kwa sababu kinaamini kuwa inafaa kufanya hivyo, hata kama
wananchi wengi hawakudai au hawapendi mabadiliko.
Pendekezo hili la kutaka Serikali
ya Tanganyika lilizushwa kwanza na Tume ya Nyalali, bila madai ya wananchi.
Chama Cha Mapinduzi kikalikataa, kwa sababu nzuri kabisa; lakini kingeweza
kulikubali, kama kilivyokubali kuacha mfumo wa chama kimoja na kuleta mfumo wa
vyama vingi, pamoja na kwamba wananchi walio wengi walipenda tuendelee na mfumo
wa chama kimoja. Maoni ya wananchi yanaweza kukifanya chama kibadili sera zake;
lakini si lazima. Chama cho chote kinaweza kubadili sera zake bila kutafuta
kwanza maoni ya wananchi. Siku ya Uchaguzi Mkuu maoni ya wananchi yatajulikana.
Nasema, niliamini kuwa ni kosa
kwa Halmashauri Kuu ya Taifa kukubali chama kiulize wananchi kama inafaa tuwe
na Serikali Tatu. Kwanza, kwa sababu hiyo niliyoeleza; na pili, hata kama CCM
ingependa kubadili sera yake, kwa nini turukie Serikali Tatu? Kwa nini tusitake
maoni ya wananchi kuhusu Serikali Moja! Au hata kuhusu Serikali za Majimbo?
Tumejadili katika vikao gani tukakubaliana kuwa miundo mingine yote haifai, ila
muundo unaofaa ni ule wa Serikali Tatu? Au hata Bunge lenyewe, limejadili
miundo mbali mbali ya Muungano katika kikao gani, hata wabunge waheshimiwa,
pamoja na waheshimiwa mawaziri weiu, wakafikia uamuzi, baada ya mjadala, kwamba
muundo peke yake unaofaa ni huu wanaopendekeza, wa kuwa na Serikali Tatu?
Hizi zote ni mbinu za viongozi
wetu waheshimiwa kutaka kukiingiza Chama katika njia moja tu nyembamba, na kutuburura
kama vipofu tuitumbukize nchi yetu shimoni. Ni jitihada za kukifanya chama, na
sisi wengine wote , tuukubali msimamo wao wa kutaka kuigawa nchi yetu.
Lakini kwa bahati njema, pamoja
na viongozi wetu, Halmashauri Kuu ya Taifa katika uamuzi wake wa kikao hicho
ilirudia kufanya hivyo ndiyo iliokuwa hauwatoshi? Na kwa nini waliifufua tena?
Hivi wao waliamini kuwa mjadala wa hoja hiyo- ndio utaweza kugawa Bunge, na
Chama na wananchi, lakini kutekelezwa kwake hakutakuwa na matokeo hayo? Na ni
nani alikuwa amewatuma wakaitekeJeze?
Pili, Chama ambacho walikuwa
hawakupata fursa ya kupata maelekezo yake kuhusu hoja ya Serikali Tatu mpaka
sasa sikijui! Chama Cha Mapinduzi kilikwisha kutoa, maelezo yake zamani sana,
kilipolikataa pendekezo la Tume ya Jaji Nyalali; Waziri Mkuu alikuwa amelieleza
hivyo Bunge kwa maelezo mazuri sana; na Kamati Kuu ilikuwa imeyarudia siku
chache tu kabla ya Serikali haijaamua kuipitisha hoja hiyo Bungeni. Selikali
ilitaka maelekezo ya Chama gani? Na Serikali zetu mbili zilitakiwa zishauriane
kuhusu nini?
Serikali zote mbili ni za Chama
Cha Mapinduzi. Na viongozi wake wote ni Wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri
Kuu ya Taifa, ambayo tarehe 10:8: 1993 iliwaagiza wakaipinge hoja ya Serikali
Tatu. Walitaka zishauriane juu ya jambo gani?
Hoja ya pili wanayoisema ni ile
ya kura ya maoni. Wanasema: "Kuhusu suala la kura ya maoni, Serikali
iliona kwamba utekelezaji wake ni sawa na kufanya uchaguzi mkuu, jambo ambalo
ni gharama kubwa. Aidha, kwa kuzingatia kuwa kura ya maoni hupigiwa suala
linalohitaji jibu NDIYO au HAPANA, ni vigumu kupata swali lililo wazi kwa
wananchi ambao hawana uzoefu wa utaratibu huu wa kura ya maoni.
REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI
WETU NA HATMA YA TANZANIA (1994)
No comments:
Post a Comment