Tafrani hiyo ilianzia katika Mahakama ya Mwanzo
Buguruni baada ya mshtakiwa huyo kusomewa mashtaka na Karani wa
Mahakama, Edwin Wandanda na kisha Hakimu Mfawidhi, Benjamin Mwakasonda
aliyekuwa akiisikiliza kusema dhamana ya mshtakiwa iko wazi.
Ingawa mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti ya
dhamana, albino waliokuwapo mahakamani hapo hawakufurahishwa na kitendo
cha kuwapo kwa nafasi ya dhamana kwa mshtakiwa wakidai kwamba ameshatoa
vitisho vya mauaji dhidi yao.
Baada ya kulalamika mahakamani hapo waliandamana
hadi kituoni hapo ambako mshtakiwa alikuwa amepelekwa hali
iliyosababisha polisi kituoni hapo kutumia risasi za baridi kuwatawanya
na kusababisha taharuki kwa wafanyabiashara na wakazi wa eneo hilo.
Mwandishi wetu alishuhudia baadhi ya watu wakiwa wamesimama, wengine wakikimbia ovyo huku polisi wakiwa silaha.
Kamanda wa Mkoa wa Polisi Ilala, Mariam Nzuki alisema vurugu hizo ziliongezeka baada ya kundi la vijana wa sokoni kuungana nao.
Alisema baada ya polisi kuona hivyo, walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya na kumpeleka mtuhumiwa katika Mahabusu ya Segerea.
Hati ya mashtaka
Mshtakiwa anadaiwa kuwa Agosti 16, mwaka huu
maeneo ya Buguruni kwa Mkanda alitishia kuua kwa maneno watu wenye
ulemavu wa ngozi katika maeneo hayo.
Hati hiyo inadai kuwa mshtakiwa alimtishia kwa maneno mlalamikaji, Mwinyiusi Issa kuwa atamuua kama anavyoua albino.
Mengi ajitolea
Wakati hayo yakitokea, Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP,
Reginald Mengi amejitolea kuwasomesha watoto wawili wa albino Suzan
Mungi, aliyekatwa kiganja cha mkono na watu wasiojulikana wilayani
Igunga mkoani Tabora.
Akizungumza jana, Mengi alisema amesikitishwa na
tukio hilo ambalo mume wa Suzan, Mapambo Mashili aliuawa wakati
akijaribu kumtetea ili asifanyiwe ukatili huo.
“Sina mamlaka ya kuwaadhibiti wahalifu hawa lakini
naahidi kutoa Sh10 milioni kwa mtu atakayewezesha kukamatwa kwao,
Serikali inapaswa kuwashughulikia wahusika wote yaani wanaofanya ukatili
huo, wanaohitaji viungo hivyo na waganga wa kienyeji,” alisema.
Imeandikwa na Kelvin Matandiko, Beatrice Moses, Ismail Gass na Salim Shao
CHANZO: MWANANCHI: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Albino-wazua-tafrani-Polisi-Buguruni-/-/1597296/2423706/-/ahsvaaz/-/index.html
CHANZO: MWANANCHI: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Albino-wazua-tafrani-Polisi-Buguruni-/-/1597296/2423706/-/ahsvaaz/-/index.html
No comments:
Post a Comment