Inspekta Jenarali wa Polisi, Ernest Mangu
Na Mwandishi Wetu, BrotherDanny Blog
Arusha: JESHI la polisi nchini limejipanga kufanya kazi zake kisasa kwa kutumia teknolojia ya kompyuta ,kuwanasa wahalifu mbalimbali badala ya kutumia mbinu za kizamani za kutumia vitisho.
Hayo yameelezwa jana na Mnadhimu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishina Msaidizi, ACP Josephat Lusingu, kwenye kikao cha wadau wa kuhusu maswala ya ulinzi na usalama wa jiji la Arusha, kilichofanyika ukumbi wa bwalo la polisi mkoa wa Arusha.
Amesema mfumo huo wa kutumia kompyuta unarahisisha kuwatia mbaroni wahalifu wowote wanaokimbilia eneo lingine kwa ajili ya kujificha baada ya kufanya uhalifu.
Kuhusu ajira, Mnadhimu huyo, amesema mfumo wa kuajiri askari umebadilika ambapo sasa wanachukuliwa vijana kutoka vyuoni na sekondari ,badala ya utaratibu wa zamani wa kutumia ngazi za kata na kuendelea na mchujo hadi ngazi ya mkoa.
Kamanda, Lusingu,amesema mfumo huu unamanufaa makubwa ambapo sasa watapatikana askari waadilifu zaidi tofauti na mfumo uliokuwa ukitumika ambapo baadhi yaaskari wanakuwa hawana uadilifu.
Kuhusu vimo vya baadhi ya askari kuwa wenye maumbo madogo na wengine wafupi, Lusingu, amesema maumbo sio tatizo bali watu wanaajiriwa kutokana na utaalamu na elimu yao ,na kubwa wa maumbo ya miili ni mbinu iliyotumika wakati wa ukoloni kwa ajili ya kutishia watu sasa hivi polisi wanafanya kazi kwa kutumia elimu.
Awali akifungua kikao hicho mkuu wa dawati la jinsia la Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha, Mrakibu mwandamizi, Mary Lugola, amesema kuwa usalama wa Arusha hauwezi kuwa endelevu kama hazitachukuliwa hatua za wananchi kushirikiana na jeshi la polisi .
Lugola, ambae ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi shirikishi mkoa wa Arusha, amesema suala la usalama lina gharama kubwa hivyo ni jukumu la kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika kuimarisha ulinzi na usalama kwenye maeneo mbalimbali kuanzia kwenye makazi yao.
"Mfano mzuri ni kwenye maonyesho ya sikuku ya wakulima Nane Nane ambayo yamemalizika hivi karibuni ambapo hapakutokea uhalifu na hiyo ni kutokana na jinsi tulivyokuwa tumejipanga na tumefanikiwa kuwadhibiti hivyo nina wahakikishia kuwa amani ya Jiji la Arusha imerejea," alisema Lugola.
Mwenyekiti huyo, Lugola, amesema jeshi la polisi linaendelea kujipanga ili kukabiliana na mbinu mbalimbali za uhalifu na hivyo kuhakikisha Jiji la Arusha na mkoa kwa ujumla vinabakia kuwa salama na hivyo kuwezesha wananchi na wawekezaji kuishi kwa usalama na kufanya shughuli zao bila ya matatizo.
Kwa upande wake Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha, OCD, Mrakibu Francis Mduma, akitoa mada kwenye kikao hicho kuhusu umuhimu wa kuimarisha ulinzi shirikishi, amesema kuwa kila mmoja anapaswa kulinda mali yake na ya taifa.
Amesema mbinu ya kutumia doria ,kuwahi kwenye matukio na upelelezi pekee hazitoi jawabu la kumaliza matatizo ya uhalifu bali msingi mkubwa ni kufanya kazi kwa karibu na jamii ambao wanawafahamu wahalifu wakiwemo majambazi.
"Uhalifu sasa unafanyika kwa njia za kitaalamu kutokana na kupanuka kwa teknolojia hivyo jeshi hilo nalo linatumia mbinu za kisasa na kuachana taratibu na mbinu za kizamani ambazo ni sawa na ulinzi wa jadi," alisema Mduma.
Kamanda Mduma, amesema, jeshi la polisi pekee haliwezi kulinda kila mwananchi kwa sababu polisi waliopo nchini ni wachache sana ukilinganisha na idadi ya wananchi ambao ni zaidi ya milioni 45.
Awali katibu wa kamati ya ulinzi shirikishi jiji la Arusha, Adolf Olomi, amesema lengo la kikao hicho ni kufahamiana, kuondoa pengo la kutokuaminiana kati ya jeshi la polisi na wananchi, kuweka mkakati wa kuimarisha ulinzi kwa kushirikiana kati ya polisi na jamii.
Amesema swala la usalama na ulinzi halichagui mtu, hivyo lazima jeshi la polisi liimarishe ushirikiano na jamii katika kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao na kujenga kuaminiana.
No comments:
Post a Comment