NA ESTHER MBUSSI, DODOMA
MWENYEKITI wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, amepinga madai ya Bunge hilo kuchukuliwa kama la mazuzu na baadhi ya watu kulishusha hadhi kwa kulifananisha na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Amesema Bunge hilo lina mamlaka zaidi kuliko tume hiyo, ndiyo maana linafanya kazi kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013.
Sitta alisema hayo jana na kuongeza kuwa, baadhi ya watu wasiolitakia Bunge hilo mema, wanachukia wakiona linaendelea vyema na shughuli zake.
“Tuache chuki katika zoezi hili, hili ni zoezi la maana, kuchukuliwa kwamba tulio hapa Dodoma ni mazuzu, ni watu wasio wazalendo, hivyo ndiyo watu wasiotupenda wanatupima, hapa kuna mchanganyiko wa watu wasomi na makini,” alisema Sitta.
Alisema pia kuwa kuna watu wanaipandisha hadhi rasimu ya Jaji Joseph Warioba na kuifanya kuwa sawa na msahafu usiotakiwa kubadilishwa huku wakifanya Bunge hilo kuonekana liko chini ya tume hiyo.
“Wanaifanya msahafu wakati imeandikwa na binadamu na ina mapungufu mengi,” alisema Sitta.
Kuhusu hadhi ya Tume na Bunge Maalumu, alisema si sawa kuonekana wako hadhi moja, kwamba tume ina mamlaka yake, lakini Bunge Maalumu lina mamlaka makubwa zaidi kuliko tume.
“Maana kila mara tunaambiwa rasimu sijui inachakachuliwa, sijui inafanywaje, ni wajibu wetu ndiyo maana walichokileta tume hapa kinaitwa rasimu, tutakachokitoa sisi kwenda kwa wananchi kinaitwa Katiba inayopendekezwa, huitaji kuhangaika sana kuona maana ya hili jambo kutoka rasimu kwenda Katiba inayopendekezwa, waliotunga sheria waliona iko kazi hapo inafanyika na kazi yenyewe ni pamoja na kufanya marekebisho,” alisema.
Kauli hiyo ya Sitta inatokana na baadhi ya vyombo vya habari, baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo maalumu na wananchi kwa ujumla, kuhoji mamlaka ya Bunge hilo kuchukua mapendekezo kutoka kwa baadhi ya makundi yaliyofika bungeni, kazi ambayo ilitakiwa kufanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akifafanua kuhusu kupoka mamlaka ya tume, Sitta alisema si kweli kwamba Bunge hilo limefanya hivyo, isipokuwa zoezi hilo limechukua sura mpya baada ya baadhi ya makundi ambayo Bunge Maalumu halikuyaalika kuleta mapendekezo yao ambayo awali waliyatoa, lakini hayakuingizwa katika Rasimu ya Katiba.
“Zoezi linaloendelea hapa linahusu Watanzania wote, nawajibika mara kwa mara ninapohisi kuna upotoshaji wa jambo nitoe maelezo kwa niaba ya Bunge Maalumu la Katiba.
“Jana magazeti yametutuhumu kwamba tunafanya kazi ya Tume ya Jaji Warioba, mimi naelewa kuna watu wanakasirishwa sana kwa namna tunavyoendelea na kazi hii vizuri, sasa basi nao ni haki yao pamoja na haki ya kukasirika.
“Lakini kinachofanywa hapa Dodoma sasa hivi ni kwamba wananchi ambao hatuwaaliki sisi wanakuja kwa makundi kuelezea wanachoona ni mapungufu ndani ya rasimu, hivi mapungufu ndani ya rasimu watayapeleka wapi zaidi ya Bunge Maalumu la Katiba?” alihoji Sitta.
Alisema Bunge linafanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kwamba kitendo cha kusema kuchukua maoni kwa wananchi ni kufanya kazi ya tume, ni upotoshaji wa watu ambao hawalitakii mema Bunge la Katiba.
Alisema rasimu haichakachuliwi ila inafanyiwa maboresho na mabadiliko kidogo na kutolea mfano wasanii waliofika kuleta mapendekezo yao ambapo miongoni mwa maoni waliyoyatoa, lakini hayakuzingatiwa, ni suala la mali isiyoshikika (Intellectual property).
Alisema Bunge kwa vigezo vyake tume ilikuwa na haki ya kuona linastahili kuwapo kwenye rasimu kwa sababu haiwezekani kuzungumzia magari, nyumba na mali nyingine ukaacha mali isiyoshikika au mali ya ubunifu ambayo tayari imeingizwa kwenye rasimu na kupigiwa kura.
“Hiyo rasimu yenyewe imeandikwa na binadamu tu, sijui kwanini inapewa hadhi kama vile ni msahafu, imeandikwa na binadamu, ina mapungufu mengi na tumeyaona, kuanzia Septemba 2, mtaona watakavyokuwa wanachambua wenyeviti wa kamati.
“Sisi hatukuchukua maoni ya wananchi kwa maana ya maoni mapya, kuna vikundi na wananchi wanaoona tume katika baadhi ya mambo haikuwawekea sawa yale waliyokwishayatoa kama maoni, na mahali pa kwenda ni kwenye chombo cha juu zaidi ambacho ni Bunge la Katiba, tuna haki na tuna wajibu wakija hapa Dodoma kuwapokea, hata leo wakija tutawapokea,” alisema Sitta.
CREDIT: MTANZANIA: http://mtanzania.co.tz/?p=1158
No comments:
Post a Comment