NA FREDY AZZAH, DODOMA
MKUTANO uliotangazwa kwa mbwembwe wa kukutanisha wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na wale wa Tanzania Kwanza, umeyeyuka kiaina huku mwandaaji akilalama kutapeliwa na mtu aliyejitambulisha kama ofisa wa Usalama wa Taifa na kada wa CCM.
Mwandaaji wa mkutano huo ambaye ni mmoja wa maofisa wa Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha New Hope Family, Omary Kombe, alisema kuwa ofisa huyo alishatapeli Sh 400,000.
Alisema kuwa mtu huyo alikuwa ameahidi kumtafutia Sh 5,000,000 ili kufanikisha maandalizi ya mkutano huo.
Mkutano huo ulikuwa ukinadiwa kuhudhuriwa na wanasiasa mashuhuri, akiwamo Rais wa awamu ya tatu, Ali Hassan Mwinyi na Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela.
Alisema fedha hizo ambazo zilikuwa gharama za kushikia (advance) ukumbi Dodoma Hotel, zilichukuliwa na mmoja wa watu waliokuwa katika kamati ya maandalizi.
Kombe alisema kuwa mtu huyo aliyemtambulisha kwa jina la John Thomson, alikutana naye karibu ya eneo la Bunge, wakati akielekea kwenye ofisi za Bunge Maalumu ili kutafuta watu wa kuweza kuwasaidia kuendesha mkutano huo.
“Baada ya kukutana naye tuliongea, na mimi nikamweleza lengo langu, akasema kuwa ni kitu kizuri na atanisaidia kukifanikisha,” alisema Kombe.
Alisema jana asubuhi, Thomson alimweleza shughuli hiyo imeahirishwa na kutaka kurejeshewa fedha walizolipa kwa ajili ya ukumbi.
“Asubuhi aliniambia kuwa nisije hapa kuna polisi wamejaa watatukamata,” alisema.
Alisema hatua hiyo ilimfanya kumpigia simu mjumbe mwingine wa kamati ya maandalizi ambaye alikuwa katika hoteli hiyo.
“Mtu huyo aliniambia kuwa Thomson amechukua fedha tulizokuwa tumelipa kwa ajili ya ukumbi, ilibidi niingie hotelini na nilipofika nikapiga simu polisi ambao walimkamata akiwa katika kituo cha polisi alipofika kwa ajili ya kesi nyingine ya kushindwa kulipia malazi,” alisema.
Alipohojiwa Thomson ambaye anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kati, alisema yeye ni mjumbe wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani Dar es Salaam na kati ya fedha hizo, Sh 300,000 ni mali yake aliyochangia katika maandalizi ya mkutano huo.
Thomson alidai kuwa alikutana na Kombe mkoani hapa na akaombwa kusaidia katika kufanikisha mkutano huo.
Meneja wa hoteli hiyo, Agustino Malingumu, alithibitisha mbele ya maofisa wa polisi kumkabidhi fedha hizo Thomson mara baada ya kumweleza kuwa mkutano umeahirishwa.
CREDIT: MTANZANIA: http://mtanzania.co.tz/?p=1146
No comments:
Post a Comment