DODOMA
12.11:1993
Nadhani uamuzi wa kuitisha kikao
cha mchanganyiko ulifanywa na viongozi wetu katika kikao cha Dodoma II.
Nimesema awali kwamba Waziri Mkuu alipohisi kuwa baadhi ya mawaziri wenzake
walikuwa wanaunga mkono hoja ya Utanganyika, na yeye kwa wakati huo alikuwa
hajui aiunge mkono au aipinge, alipendekeza ifanyike semina ya viongozi wote ili
jambo hili lizungumzwe na lipingwe nje ya Bunge.
Viongozi ambao wangehudhuria
katika semina hiyo ndio walioalikwa kuja katika kikao cha mchanganyiko cha
Dodoma. Lakini shabaha ya kuwakutanisha ilikuwa imebadilika. Kama semina ya
awali ingefanyika, shabaha yake ilikuwa ni kupinga hoja ya Wabunge, na mimi
niliombwa niende nisaidie. Kamati Kuu ya CCM ikaamua kuwa hapakuwa na haja ya
kufanya semina hiyo. Lakini baada ya kuona msimamo wa Halmashauri Kuu ya Taifa
na ugumu wa kushawishi wajumbe wake wakubali hoja ya Serikali Tatu, viongozi
wetu walifufua tena wazo la semina.
Huenda waliona wanahitaji msaada,
na kwa kuwa sasa hoja ni ya wabuge wote, walihisi kuwa itafaa itafutwe njia ya
kuikutanisha Halmashauri Kuu ya Taifa pamoja na wabunge wote. Na kwa kuwa isingetoa
sura nzuri kuita wabunge peke yao, ikapendekezwa kuwa Serikali ya Mapinduzi na
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi nao waitwe!
Mazungumzo na maamuzi ya kikao
hicho cha mchanganyiko yanafahamika vizuri zaidi, na hayana haja ya kuelezwa
sana. Inatosha kusema kuwa wote walikubaliana, na baada ya mjadala wa wazi wazi,
kwamba sera ya Serikali Mbili ni sera ya Chama Cha Mapinduzi. Wakapendekeza
kuwa suala hili lizungumzwe na wanachama wa CCM ili tupate maoni yao. Ni aina
ya referendamu, lakini badala ya kutafuta maoni ya wananchi wote, waulizwe
wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kama wanataka,
(i) Tubaki na Sera ya Serikali
Mbili;
(ii) Tuibadili na kuwa na sera ya
Serikali Tatu; au
(iii) Tuibadili na kuwa na sera
ya Serikali Moja
Jambo hili yafaa lisisitizwe.
Viongozi wetu, kama kawaida yao,
walipachika maneno "haja ya kuwa na Serikali ya Tanganyika," katika
mapendekezo ya kikao cha pamoja. Hizo ni hila; maelewano sivyo yalivyokuwa.
Mapendekezo ni kwamba sera ya Serikali Mbili, izungumzwe ndani ya Chama ili kuona
kama pana haja ya kuibadili.
Kikao kile hakikusema kuwa endapo
wanachama wetu wataamua kubadili sera ya Serikali Mbili, basi wazingatie hoja
na haja ya kuwa na Serikali Tatu. Kwa bahati njema maswali waliyoulizwa
wanachama wa CCM yanazingatia na kuheshimu uhuru wao, bila kujali hila hizi za
viongozi.
Hapo ndipo tulipo hivi sasa. Mimi nitashangaa kabisa ikiwa wanachama wa CCM watasema kuwa wanataka Serikali ya Tanganyika. Iwafanyie kazi gani ambayo haiwezi kufanyika hivi sasa? Na kuvunja Muungano kutawafaa nini, wao na raia wenzao? Na wana uhasama gani na Wazanzibari, au wamewafanyia nini hata waseme wamechoka nao?
Hapo ndipo tulipo hivi sasa. Mimi nitashangaa kabisa ikiwa wanachama wa CCM watasema kuwa wanataka Serikali ya Tanganyika. Iwafanyie kazi gani ambayo haiwezi kufanyika hivi sasa? Na kuvunja Muungano kutawafaa nini, wao na raia wenzao? Na wana uhasama gani na Wazanzibari, au wamewafanyia nini hata waseme wamechoka nao?
III HAJA
YA KUWAJIBIKA
Kabla ya kuondoka Dodoma kwenda
Dar es salaam ambako nilionana na watangazaji wa habari baadaye, nilipata
nafasi ya kuzungumza na Rais kuhusu matokeo ya mkutano wa pamoja, na nini la
kufanya. Nilimweleza maoni yangu. Kwa kuwa mazungumzo haya yanayotakiwa
yafanywe na wanachama wa CCM ni ya kusukumizwa, na hayana maelezo, si busara
kufanya haraka. Ilikuwa imetangazwa kuwa Rais atateua kamati ya kuratibu maoni
ya wananchi. Nilitazamia kuwa badala yake atateua kamati ya kusimamia utaratibu
wa kupata maoni ya wanachama. Nilishauri ateue kamati ya watu makini; iongozwe na
mtu mwenye busara, iandae maelezo yatakayokuwa mwongozo wa mazungumzo
yatakayofanywa na wanachama wa CCM. Wanachama hawana budi waelezwe kwa nini
tunataka wazungumze muundo wa Muungano. Lazima tueleze tena asili ya muundo wa
Serikali Mbili. Tuwasaidie wanachama, na wananchi kwa jumla, kuelewa sababu za
muundo huo; uzuri wake na upungufu wake.
Lazima tueleze ni upungufu gani
tunadhani unatokana na muundo wenyewe, na ni upungufu gani unaotokana na
utekelezaji tu. Lazima tuchambue namna mbali mbali za kuendesha Muungano; jinsi
ya kurekebisha muundo wa Serikali Mbili, na jinsi ya kuondoa upungufu
unaotokana na utekelezaji. Kamati hiyo ingeweza kusaidiwa na kazi ambayo
imeanzwa na kamati mbali mbali za Chama na Serikali.
Kama itaonekana kuwa muundo wa
Serikali Mbili lazima uachwe, hatuna budi tuchambue na kueleza faida na hasara
za miundo mbali mbali: muundo wa Serikali Moja, na muundo wa SerikaIi Tatu.
Tunaweza, tukipenda, kuchambua na kueleza pia faida na hasara za kuwa na muundo
wa Serikali zaidi ya Tatu.
Kinachopendekezwa na washabiki wa
Serikali Tatu ni Muundo wa Shirikisho. Wako watu wanaoamini kwamba ni rahisi
zaidi kuwa na Shirikisho la Zanzibar yenye Serikali Moja na Tanganyika yenye
Serikali zaidi ya moja, kuliko kuwa na Shirikisho la Zanzibar yenye Serikali
Moja na Tanganyika yenye Serikali Moja.
Yote haya yanatakiwa yachambuliwe
na kuelezwa vizuri kabisa. Na wakati huo huo maelezo hayo hayana budi
yasisitize historia na mwelekeo wa nchi yetu, na Chama Cha Mapinduzi. Historia
yetu na mwelekeo wetu mpaka sasa umekuwa ni wa kuimarisha Muungano.
Kama tunaona kuwa inafaa kuacha
muundo wa Serikali Mbili hatuna budi tuseme wazi wazi katika Mwongozo huo
kwamba kwa maoni ya uongozi wa Chama muundo unaoweza kuendeleza historia na
mwelekeo wa nchi yetu, ni muundo wa Muungano wa Serikali Moja. Uongozi wa Chama
hauwezi kusema kuwa hauna maoni yake, ila unasubiri maoni ya wanachama! Kuongoza
ni kuonyesha njia.
Baadaye wanachama wa CCM walipoombwa
watoe maoni yao kuhusu suala hili, hapakuwa na maelezo wala mwongozo kama huo.
Sababu zinazotolewa ni kwamba viongozi wetu hawakutaka waonekane kama
wanawashawishi au kuwalazimisha wanachama kufuata msimamo fulani. Nadhani
ukweli ni kwamba viongozi wetu walidhani kuwa sera ya Chama isipokuwa na
mtetezi wake, na uwanja ukaachwa wazi kwa washabiki wa Serikali Tatu, basi
wanachama wa CCM watakubali hoja ya Utanganyika. Lakini hata bila maelezo hayo
na mwongozo huo siamini hata kidogo kwamba wanachama wa CCM watakubali hoja ya
Serikali Tatu.
llikuwa ni dhahiri kwamba kazi
hii haiwezi kufanywa chini ya usimamizi wa viongozi waliopo. Hawa sasa wanaona
kuwa heshima yao na "nyuso" zao, na labda baadaye zao, zinawadai
watetee msimamo wa Serikali Tatu. Hawawezi kutetea sera ya Chama ya Serikali
Mbili, wala mwelekeo wa Chama wa Serikali Moja. Watatumia uwezo walia nao
kutokana na hadhi walizo nazo, kuvuruga sera ya Chama na mwelekeo wake.
Tutahitaji kiongozi mpya wa Serikali, na kiongozi mpya wa Chama.
MAANA YA MANENO:
Neno la Kiingereza "resign", lina maana mbili:-
(i) to give up or surrender (one's job or property or claim etc.). Ni
kuacha au kuachia; kama kuacha au kuachia, (kazi, au mali au haki, au madai
n.k.). Maana ya "give up"; to
cease (doing something); to part with; to surrender; to abandon hope; to
declare a person to be incurable or a problem to be too difficult for oneself
to solve. Ni kuacha (kufanya jambo); kuachia au kuachana na; kusalimu amri;
kukata tamaa; kusema kuwa mtu hatibiki au tatizo fulani linakushinda kutatua.
Maana ya "Surrender": (1) to
hand over, to give into another person's power or control, especially on demand
or under compulsion. Ni kutoa kwa, au kumwachia mwingine uwezo au mamlaka,
hasa kwa kudaiwa au kulazimishwa. (2) to
give oneself up, to accept an enemy's demand for submission. Ni kusalimu
amri, kukubali amri ya adui ya kujitolea. Hayo ndiyo maelezo ya maana ya kwanza
ya neno "resign," yaani
“jiuzulu".
(ii)Maana ya pili: "Resign onself to": to be ready to accept or endure, accept as
inevitable. Ni kuwa tayari kukubali na kustahimili; kukubali kuwa jambo
fulani ni lazima liwe, halizuiliki. Ni kukubali kuwa umeshindwa au utashindwa,
na kuwa tayari kustahimili matokeo ya kushindwa. Ni kukubali kusalimu amri ya
adui au mpinzani wako na kuwa tayari kustahimili matokeo yake. Ni kukubali
kutekwa, na kuwa tayari kustahimili matokeo ya kuwa mateka. Nikukubali
kushindwa; ni kubwaga silaha. Mkazo katika maana hii ya pili ni kule kukubali
kustahirnili matokeo ya kukata tamaa na kubwaga silaha.
REJEA: NYERERE J.K.: UONGOZI WETU
NA HATMA YA TANZANIA (1994)
No comments:
Post a Comment