IV. MSIMAMO WA RAIS
Wakati wa mgogoro wa Zanzibar kuingia katika OIC, na utaratibu wa
kuchagua Makamu wa Rais, yawezekana kuwa Rais mwenyewe alikuwa akipendelea msimamo
wa "Wazanzibari". Na hasa kuhusu suala la OIC, maelezo yake kwa Wazee
wa Dar es Salaam, na baadaye alipowahutubia wananchi siku ya Mei Mosi, Mtwara,
yalifanya watu wengi waamini hivyo. Na washauri wake wa karibu walitaka tuelewe
hivyo: kwamba ugumu wa suala la OIC ulikuwa unaletwa na Rais mwenyewe, maana
alikuwa akiliona suala hilo kwa jicho la Uzanzibari, badala ya kuliona kama
Rais wa Tanzania na mlinzi mkuu wa katiba yake.
Lakini pamoja na kwamba hivyo ndivyo washauri wake wakuu walivyotaka
tuelewe, na yawezekana kuwa walikuwa wakisema kweli, kila tulipojaribu kuelewa
kwa nini wao hawajiuzulu, hatukupata jibu lolote, achilia mbali jibu la maana.
Waziri akihitilafiana na Rais wake katika jambo la msingi, kwa kawaida
anatazamiwa kujiuzulu na kueleza kwa nini hawezi kuendelea kuwa Serikalini.
Hawa hawakufanya hivyo. Lakini walitaka tuelewe kuwa mwenye hatia ni Rais.
Katika suala la Utanganyika, inaelekea kuwa Rais si miongoni mwa mrubani,
yeye anakokotwa tu, moyo wake haumo. Lakini washauri wake wamemfikisha pagumu. Kutokana
na msimamo wake wa awali kuhusu OIC, inaelekea kuwa Rais anaambiwa, ama ni
washauri wake au na dhamiri yake mwenyewe: "Madhali suala la OIC
ulilifumbia macho, huna budi ulifumbie macho na suala la Utanganyika pia.
Usipofanya hivyo 'Watanganyika' hawatakuelewa."
Kwa hiyo washauri wake walipomshauri akubali hoja ya kufufua Tanganyika
na kuipa Serikali yake, badala ya kukataa na kumfukuza Waziri Mkuu kwa
ukigeugeu wake, Rais wetu alikubali! Alifanya hivyo akijua athari za kufufua
Utanganyika, na baada ya yeye mwenyewe kusimama mbele ya wabunge siku chache tu
zilizopita, na kupinga hoja ya Serikali Tatu. Na alifanya hivyo baada ya kukiri
na kusahihisha kosa la Zanzibar, hatua ambayo nilitazamia kuwa itampa nguvu ya
kupinga hoja ya Utanganyika.
Hatuwezi kuwa wakweli tukisema kuwa Rais hana hatia, Rais wa Tanzania si
sawa na Malkia wa Uingereza. Huyo ni Mkuu wa Nchi kikatiba ambaye hana madaraka
ya kuongoza nchi yake. Kwa mujibu wa Katiba na mazoea ya nchi yao, hana budi
akubali ushauri wa Waziri Mkuu wake, Hata kama yeye mwenyewe binafsi
hakubaliani na ushauri huo. Rais wa Tanzania sivyo alivyo. Yeye ni Mkuu wa nchi
Mtendaji. Kikatiba halazimiki kukubali na kutekeleza agizo la Rais ambalo
hakubaliani nalo, hasa kama tofauti yenyewe ni kwa jambo la msingi, kama vile
jambo la maadili na dhamiri, au sheria, au Katiba ya Nchi.
Waziri akiagizwa na Rais kufanya jambo la namna hiyo ana haki na wajibu
wa kukataa na kujiuzulu. Rais hawezi kuagizwa na Waziri ye yote, yeye
hushauriwa tu na Mawaziri wake. Akikubali ushauri mbaya hawezi kujitetea kwa
kumtupia lawama Waziri aliyemshauri, maana uamuzi wa mwisho ni wake. Alikuwa na
hiari kukubali au kukataa ushauri huo. Na ingawa Waziri hawezi kumfukuza Rais
wake anayehitilafiana naye katika jambo kubwa, Rais anaweza, na mara nyingi
anawajibika kumfukuza Waziri wake anayepingana naye katika suala kubwa na la
msingi. Kwa hiyo ni dhahiri kwamba Rais hawezi kukubaIi ushauri mbaya, halafu
aepuke lawama, na amsukumie lawana Waziri aliyemshauri vibaya. Kanuni hii ni ya
wazi, na ni vizuri ikaeleweka hivyo.
Lakini pamoja na hayo, katika suala hili ni kosa kutanguliza na
kusisitiza zaidi uwajibikaji wa Rais. Kuwajibika kuna ngazi yake. Hatuwezi
kusema ati kwa sababu Mkuu wa Nchi yetu ni Rais Mtendaji, basi atawajibika kwa
kila kosa la Serikali yake na Mawaziri wake, hata pale, ambapo mkosaji halisi
na wa wazi wazi ni Waziri. Rais hawezi kuwajibika kwa makosa ya Uongozi wa Serikali
Bungeni, kama kwamba yeye naye ni Mbunge.
Viongozi wa chama na Serikali waliomo Bungeni, hasa Waziri Mkuu na
Katibu Mkuu, ndio wanaostahili kuwajibika moja kwa moja. Kwa vyo vyote vile
hatuwezi kujenga utaratibu ambapo Waziri akikosa Rais ndiye anayewajibika. Mara
mbili sasa Rais amelazimika kukiri hadharani makosa ya Serikali yake; na Mawaziri
wahusika hawana wasi wasi. Kwanza, Rais ndiye aliyekiri kosa la Zanzibar
kuingia katika OIC, na pili, ndiye aliyelazimika kukiri kule Dodoma kwamba
utaratibu wa kushughulikia hoja ya Utanganyika ulikosewa. Lakini Mawaziri wake,
mara zote mbili, walitulia tu na kumwacha Rais ndiye akiri kosa na kubeba
lawama.
Katiba ya Nchi yetu, na utaratibu tunaojaribu kujenga, vinataka kuwa
katika hali kama hiyo Mawaziri ndio wawajibike, na hivyo kumlinda Rais, si Rais
awajibike, na kuwalinda Mawaziri wake, na tena kwa kosa ambalo si lake. Watu
walioshindwa uongozi Bungeni, hata tukafikishwa hapa tulipo leo, ni Waziri Mkuu
na Katibu Mkuu wa CCM. Hawawezi kukwepa matokeo ya kusarenda kwao Bungeni, na
wamtupie Rais, ati kwa sababu Rais wetu ni Rais Mtendaji na walipomshauri
kusarenda kama wao, alikubali. Tukikubali hoja hiyo hakuna Waziri ye yote
atakeyetakiwa kuwajibika kwa kosa lo lote; maana kila wakati Rais atatakiwa
awajibike badala yake.
REJEA:
NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA (1994)
No comments:
Post a Comment