Pius Msekwa
Nchi mbili zinapoungana na kuwa Nchi moja mifumo ya kawaida ya miundo ya
Katiba ni miwili: Muungano wa Serikali Moja, au Shirikisho la serikali Tatu.
Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta serikali yake na nchi mpya inayozaliwa
itakuwa ni nchi moja yenye Serikali moja. Katika mfumo wa pili kila nchi
itajivua madaraka ambayo yatashikwa na serikali ya shirikisho na itakuwa na
serikali ambayo ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliyobaki.
Mambo yatakayoshikwa na serikali ya Shirikisho ili yale ambayo yatashikwa
na serikali ya shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika nchi zilizoungana basi
kwa kweli nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi moja bali zinaendelea kuwa
nchi mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo fulani fulani.
Nchi za Afrika Mashariki zilikuwa katika hali kama hiyo kabla ya
kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Zilikuwa ni Nchi Tatu zenye
ushirikiano mkubwa, lakini hazikuwa Nchi Tatu zilizoungana kuwa Nchi Moja yenye
muundo wa Shirikisho. Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa ni Nchi Moja
yenye Serikali tatu, Serikali ya Shirikisho, na Serikali mbili za nchi mbili za
awali zilizoungana kuzaa nchi mpya moja.
Tanganyika na Zanzibar zilipoamua kuungana na kuwa Nchi Moja, tungeweza
kufuata mmojawapo wa mifumo hiyo ya kawaida. Lakini tulishindwa kufanya hivyo
kwa sababu ya udogo wa Zanzibar na ukubwa wa Tanganyika. Zanzibar ilikuwa na
watu laki tatu (300,000) na Tanganyika watu milioni kumi na mbili (12,000,000).
Muungano wa Serikali Moja ungefanya ionekane kama Tanganyika imeimeza
Zanzibar. Tulikuwa tunapigania Uhuru na Umoja wa Afrika; hatukutaka tuuhaniwe
hata kwa makosa, kwamba tunaanzisha ubeberu mpya!
Kwa hiyo mimi nilipinga mfumo wa Serikali Moja. Shirikisho la Serikali
Tatu lingekuwa ni gharama kubwa mno kwa Tanganyika. Zanzibar ingeendesha
Serikali yake na kuchangia gharama za kuendesha Serikali ya Shirikisho; na
Tanganyika ingefanya vivyo hivyo. Lakini ni dhahiri kwamba mchango wa Tanganyika
ndio hasa ungeendesha SerikaIi ya Shirikisho. Kwa hiyo Tanganyika ingeendesha
Serikali yake ya watu 12, 000, 000 na pia ndiyo ingetoa sehemu kubwa ya
kuendesha Serikali ya Shirikisho la watu 12,300,000.
Ni Watu wanaofikiri kwa ndimi zao wanaodhani kuwa gharama ya Serikali
yoyote kati ya hizo ingekuwa ndogo. Gharama ya Serikali ya Tanganyika
isingekuwa ndogo, (waulizeni Wazanzibari), na wala ya Serikali ya Shirikisho
isingekuwa ndogo. Hata bila ya gharama za mambo yasiyo ya Shirikisho. Na
gharama zote hizo kwa kweli zingebebwa na Tanganyika.
Kwa hivyo ilitupasa tujiulize kwa nini tunataka kuibebesha Tanganyika
gharama zote hizo; na hasa kwa nini tunataka Serikali ya Tanganyika? Hivi tuna
hofu ya kwamba Tanganyika, bila kuwa na SerikaIi yake, itaonekana kuwa imemezwa
na Zanzibar? Hofu yetu ni kwamba tukiwa na Serikali Moja Tanganyika itaonekana
kuwa imeimeza Zanzibar. Basi na tutafute mfumo ambao utaiondolea Zanzibar hofu
hii ya kumezwa, bila kuibebesha Tanganyika mzigo wa kuendesha Serikalli mbili
zenye uzito unaolingana.
Hivyo ndivyo tulivyofanya, na hiyo ndiyo asili ya muundo wa Muungano wa
serikali mbili. Badala ya kutungua mfumo uliopo kama wapumbavu, tulitazamia
hali halisi yetu ilivyokuwa, na tukabuni mfumo uliotufaa zaidi.
Labda ni vizuri kukumbusha kwamba shabaha ya baadhi yetu ilikuwa ni
kuunganisha nchi za Afrika Mashariki ziwe nchi moja. Na wakati Zanzibar na
Tanganyika zinaungana, Kenya, Uganda na Tanganyika zilikuwa katikati ya
mazungurnzo ya kutafuta uwezekano, wa kuungana. Kama jambo hilo, lingetokea,
nina hakika kabisa kwamba mfumo wa nchi mpya ambayo ingezaliwa ungelikuwa ni
Shirikisho; au la Shirikisho la Nchi Tatu zenye Serikali Nne, na Shirikisho la
Nchi Nne zenye Serikali Tano.
Kwa kweli hata kesho Nchi za Afrika ya Mashariki zikiamua kuungana, na
Tanzania ikawa ni mshiriki, naamini kuwa ni rahisi zaidi kushirikisha Tanzania
yenye Serikali Mbili - ya Zanzibar na ya Tanganyika - kuliko Tanzania yenye
Serikali Mbili, ya Tanzania na ya Zanzibar. Wapendao Utanganyika watakuwa
wazalendo zaidi, badala ya kuwa wasaliti, wakiazimia Afrika ya Mashariki
iliyoungana kuwa Nchi Moja. Kuliko Tanzania iliyotengana ikawa nchi mbili.
Siku ya pili yake tarehe 15:8:1993, Wabunge wenye hoja yao na wengine
zaidi, waliomba tena kuja 'Tunywe chai'. Na baada ya mazungurnzo nao ilikuwa ni
dhahiri kabisa kwangu kwamba hata kama hawakuondoa hoja yao. (wala mimi sikuwaomba
waiondoe), wataitumia kutoa dukuduku zao tu; hawataitumia kung'ang'ania kudai
Serikali ya Tanganyika. Kwa hiyo sikushangaa baadaye niliposikia kuwa
waliiondoa hoja yao ya awali, na badala yake wakaleta hoja ya kutafuta maoni ya
wananchi. Mimi kwa upande wangu nilihisi kuwa hoja mpya hii ilikuwa na shabaha
ileile ya "kunawa uso", kama Zanzibar kusema kuwa wanatoka katika
OIC, lakini utafanywa uchunguzi wa kuona kama Tanzania inaweza kuingia katika
OIC.
Huko nyuma baadhi ya viongozi wa Zanzibar wapinzani wa Muungano wamewahi
kudai tufanye referendum Zanzibar kuhusu Muungano. Tukakataa kwa sababu safi
kabisa. Maoni haya ya Wabunge wa Bara ambao mimi naamini kabisa si wapinzani wa
Muungano, nayo yangeweza kukataliwa na Chama na SerikaIi, kwa sababu zile zile
na mambo yakesha.
II SERIKALI INASARENDA
Baadaye, nadhani siku iIiyofuatia, niliitisha kikao cha Watangazaji wa
Habari, nikapinga kwa kirefu hoja ya Utanganyika. Wakati naondoka Dar es Salaam
ili kurudi Butiama, nilitumaini kabisa kwamba Serikali ingeendeleza Bungeni, na
kama na kama hapana budi nchini, kazi tuliyoanza pamoja, ya kupinga hoja ya
Tanganyika. Sikuwa na sababu yoyote ya kuhofia kuwa siku chache tu baadaye
Serikali itageuza msimamo wake na kufanya "abautani".
Sijui lililotokea, maana kila nilipouliza sikupata maelezo. Kama
nilivyokwisha kusema hapo nyuma baadaye wabunge wahusika waliiondoa hoja yao ya
awali ya kutaka Bunge lipitishe azimio la kudai Serikali Tatu, wakaleta hoja
mpya ya kutaka Serikali ifanye referendamu ya kutafuta maoni ya wananchi kuhusu
suala hili. Nasema, SerikaIi ingeweza kuikataa hoja hii kwa maelezo safi kabisa
na mambo yakesha.
Au kama wangeona kuwa si siasa nzuri kuipinga hoja hii nayo, wangeweza
kuikubali, na mimi nina hakika, wananchi wangeikataa na mambo yakesha. Lakini
Serikali ya Muungano, bila maelezo ilikataa hoja mpya ya wabunge ya kutaka
maoni ya wananchi, na yenyewe ndiyo ikafufua hoja ya Utanganyika, na
kupendekeza kwamba badala ya hoja ya Serikali Tatu kujadiliwa Bungeni na
kupigiwa kura, Bunge zima, pamoja na Serikali yenyewe, likubali hoja hiyo, bila
mjadala!
Kumbe jambo ambalo viongozi wetu walikuwa wanahofu kabisa kabisa ni
mjadala, maana huo ungewalazimisha kujitambulisha kama si katika mjadala
wenyewe, basi wakati wa kupiga kura, hasa ikiwa ni kura ya kuita mbunge mmoja
mmoja kwa jina, pamoja na mawaziri wetu! Badala ya kupita katika adha hiyo
wakaona afadhali wakubali Serikali Tatu, bila ya mjadala. Basi SerikaIi yetu
ikanywea ghafIa, kama mpira uliotoboka au puto lililopasuka. Nadhani hata
wabunge wenye hoja ya awali walishangaa!
Kuongoza ni kuonyesha njia. Viongozi wetu walikuwa Wametumwa na chama
chao waende bungeni, Bunge Ia wanachama watupu wa CCM wakawaonyeshe njia.
Wakawaambie wabunge wahusika kwamba hoja yao ya kutaka Serikari Tatu ni kinyume
cha sera ya chama chao, na ina hatari ya kuigawa na kuiangamiza Nchi yetu.
WaIiagizwa wazi wazi wakaipinge hoja hiyo. Wakapata mtihani mdogo sana
bungeni. Wakasarenda. Wakatupa silaha chini; wakasalimu amri. Viongozi hawa
hawawezi kusimama mbele ya Kamati Kuu, au mbeIe ya Halmashauri Kuu ya Taifa
kusema kwa fahari kama wao ni hodari: Kazi mliyotutuma tumeikamilisha! Wala
hawataki kukubali matokeo ya kusarenda kwao.
Kwa sababu uamuzi wa kutaka Serikali ya Tanganyika ‘ndani ya muungano’
ulifanywa na viongozi wetu kwa hila, na kupitishwa bungeni bila mjadala, sisi
wengine hatukujua lililotokea. Baadaye tulifahamishwa kuwa huo ndiyo ulikuwa
uamuzi wa ‘bunge zima” kutokana na kauli ya Pius Msekwa aliyekuwa msimamizi wa
kikao cha Bunge kilichofikia uamuzi huo.
Nadhani viongozi wetu walitaka kuendelea kuficha na kuuvuga vuga, lakini
yeye akatoboa. Nasikia baadaye aliitwa akakemewa. Sijui kwa nini.
REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA
REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA
No comments:
Post a Comment