Washambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe (mbele) na Simon Msuva wakishangilia kwa pamoja bao la tatu la timu hiyo lililofungwa na Tambwe katika mechi ya kwanza dhidi ya Platinum jijini Dar es Salaam ambapo Yanga ilishinda 5-1.
...TAZAMA, UMEBAKI WEWE,
WEWE TU KUTULETEA RAHA
Na Daniel Mbega
WAWAKILISHI pekee wa
Tanzania michuano ya klabu barani Afrika, Yanga, wako mjini Zvishavane huko
Zimbabwe kutafuta sare ama ushindi dhidi ya timu ya Platinum ya huko ili
kufukuzu kwa robo fainali ya Kombe la Shirikisho.
Yanga wataingia uwanjani
leo hii wakijivunia ushindi wao wa mabao 5-1 walioupata jijini Dar es Salaam Machi
21 na safari ya basi ya kilometa 385.4 kutoka Harare hadi Zvishavane inaonekana
haitawazuia kufika hatua hiyo ya juu baada ya miaka mingi.
Ule mzimu wa kujisahau
kwa sababu wana faida ya mabao mengi uliojitokeza katika mechi ya raundi ya
kwanza dhidi ya maafande wa Botswana Defence Force unaweza usijirudie kwani
makocha wa timu hiyo, Hans van Der Pluijm na Charles Boniface Mkwasa,
wamewajengea saikolojia nzuri wachezaji wao ambao sasa watatafuta ushindi kwa
bidii zote.
Katika hatua iliyopita,
Yanga walishinda 2-0 nyumbani dhidi ya BDF, na walipokwenda Gaborone hata baada
ya kpata bao la kuongoza, wakajisahau na kujikuta wakifungwa mabao 2-1, hivyo
kuchafua rekodi yao.
Mkwasa anasema kikosi
chake kiko tayari kucheza kwenye uwanja wowote na Platinum ambayo iliing'oa
Sofapaka ya Kenya kwa jumla ya mabao 4-2 katika mzunguko wa kwanza.
“Tunajifua kwenda
kupambana na kushinda, hatufikirii matokeo ya sare wala kufungwa, tumewaambia
wachezaji wakapambane kutafuta mabao mengi zaidi nchini Zimbabwe kama
tulivyofanya hapa katika mechi ya kwanza,” alisema Mkwasa.
Yanga ndiyo timu pekee
yenye dhamana ya kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa baada ya
timu nyingi zote kufungashiwa virago kwenye mzunguko wa kwanza.
Katika Ligi ya Mabingwa
Afrika, Azam ilitolewa na El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-2 na
wanamaji wa Zanzibar, KMKM, wakatolewa na timu nyingine kutoka huko huko Sudan
kwa jumla ya mabao 2-1.
Polisi Zanzibar
ilitolewa kwenye Kombe la Shirikisho baada ya kfungwa jumla ya mabao 8-1 na CF
Mounana ya Gabon.
Haijawahi kutwaa ubingwa
wa Afrika, Kombe la Washindi wala hili la Shirikisho, lakini Yanga ina uzoefu
mkubwa wa mechi za kimataifa ikiwa imeanza kushiriki tangu mwaka 1969.
Itakumbukwa kwamba,
mwaka huo 1969 iliposhiriki kwa mara ya kwanza Klabu Bingwa Afrika, ilianza kwa
kuitoa Fitarikandro ya Madagascar kwa jumla ya mabao 4-3 katika hatua ya awali
na katika raundi ya kwanza ikainyuka Saint George ya Ethiopia kwa jumla ya
mabao 5-0.
Ni mwaka huo ambao klabu
ya TP Englebert ya Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) ilibadili jina
na kuitwa TP Mazembe.
Baada ya kuvuka hatua
hiyo, Yanga ikijivunia wachezaji kama kipa Elias Michael 'Spring', Omar Kapera,
Awadh Gessani, Mohammed Hussein Hassan 'Msomali', Hassan Gobos, Maulid Dilunga,
Omar Zimbwe, nahodha Abdulrahman Juma na wengineo, ikatinga robo fanaili na
kukutana na timu ngumu ya Afrika, Asante Kotoko ya Ghana, iliyokuwa ikitamba na
kipa wake mrefu Emmanuel Okalla.
Katika mchezo wa kwanza
uliopigwa Kumasi, timu hizo zilifunga bao 1-1, matokeo ambayo yalipatikana pia
jijini Dar es Salaam, na kwa ajabu ya wengi, Yanga ikatolewa kwa shilingi!
Mwaka 1970 tena katika
mashindano hayo, Yanga ilianza na US Fonctionnaires ya Madagascar kwenye raundi
ya kwanza na kuitoa kwa jumla ya mabao 6-4, na ilipotinga raundi ya pili
ikaitoa Nakuru All Stars ya Kenya kwa jumla ya mabao 3-2, hivyo kutinga robo
fainali kwa mara ya pili ambako ilikutana tena na Asante Kotoko ya Ghana.
Matokeo ya mchezo wa
kwanza mjini Kumasi yalikuwa 1-1, ziliporudiana mjini Dar es Salaam zikafunga
tena 1-1, hivyo CAF ikaamuru mchezo huo upigwe katika uwanja huru, ambapo
walikwenda kuchezea Addis Ababa, Ethiopia na Kotoko wakashinda kwa mabao 2-0.
Mwaka 1971 Yanga iliitoa
Lavori Publici ya Somalia kwa mabao 2-0, lakini ikajitoa raundi ya pili baada
ya kupangwa kukutana na Coffee FC ya Uganda kutokana na uhusiano wa kisiasa
baina ya Tanzania na Uganda kuwa mbaya hasa baada ya Jenerali Idi Amin Dada
kuipindua serikali ya Milton Obote.
Mwaka 1972 Yanga
ikarudia raundi ya kwanza ya Klabu Bingwa baada ya kutolewa na AS Saint Michael
ya Madagascar kwa jumla ya mabao 2-1 na mwaka 1973 ikatolewa katika hatua hiyo
hiyo na El Merreikh ya Sudan kwa umla ya mabao 3-2.
Katika michuano ya mwaka
1975, Yanga ilipita moja kwa moja na kuingia raundi ya pili ambako ilikutana na
Enugu Rangers ya Nigeria. Matokeo katika mchezo wa kwanza huko Nigeria yalikuwa
suluhu, lakini ziliporudiana jijini Dar es Salaam zikafungana bao 1-1, hivyo
Enugu ikafuzu kwa sheria ya bao la ugenini. Ndio mwaka huo ambao Kombe la
Washindi lilianza kushindaniwa.
Katika mashindano ya
mwaka 1982, Yanga ilianza raundi ya awali kwa kucheza na Tetil Pungue ya
Msumbiji, ambapo iliitoa kwa jumla ya mabao 4-1, lakini katka raundi ya pili
ikatolewa na Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 6-1. Mwaka huo Al Ahly ilitwaa
ubingwa kwa kuifunga Asante Kotoko mabao 4-1.
Mashindano ya mwaka 1984
ndiyo yaliyoleta utata zaidi. Kwanza ilitolewa na Gor Mahia kwa jumla ya mabao
2-1 baada ya sare ya bao 1-1 nyumbani na kukubali kipigo cha bao 1-0 huko
Nairobi.
Kwenye mchezo ule wa Dar
es Salaam inaelezwa kwamba maofisa wa klabu hiyo walipanga kuwahonga waamuzi
kutoka Ethiopia ili 'waibebe', wakagoma na habari zikafika CAF, ambapo maofisa
wawili walifungiwa maisha kujihusisha na kandanda.
Mashindano ya mwaka 1988
Al Ahly ya Misri kwamara nyingi ilikatisha safari ya Yanga kwa kuifunga jumla
ya mabao 4-0 katika raundi ya kwanza, lakini mzimu wa timu za Misri kwa Yanga
ukajirudia tena mwaka 1992 baada ya kutolewa na Ismaili kwa jumla ya mabao 3-1
ingawa Yanga ilikuwa imefuzu hatua ya awali kwa ushindi wa mabao 7-2 dhidi ya
Saint Louis ya Shelisheli.
Katika Kombe la CAF
mwaka 1994, Yanga ilishindwa kufurukuta baada ya kutolewa na Moroka Swallows ya
Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 2-1,
Hii siyo mara ya kwanza
kwa Yanga kupambana na timu za Zimbabwe, kwani mwaka 1995 katika Kombe la
Washindi vijana hao wa Jangwani waliondolewa kwenye robo fainali na Blackpool
kwa jumla ya mabao 4-2. Katika raundi ya kwanza, Yanga ilicheza na Vaal Reef
Professionals ya Afrika Kusini na kuitoa kwa mabao 4-3, mechi ambazo ndizo
zilizowapa ulaji Bakari Malima 'Jembe Ulaya' na Shaaban Nonda 'Papii' na kutua
'Bondeni'.
Kwenye raundi ya pili
Yanga ikaitoa Tamil Cadets Club ya Mauritius kwa mabao 4-2.
Mwaka 1996 APR ndiyo
iliyofupisha safari ya Yanga katika hatua ya awali tu kwa kuifunga jumla ya
mabao 4-0, na mwaka 1997 safari ya vijana hao wa Jangwani ikaishia Uganda kwa
Express FC ambayo mwaka huo ilibadili jina na kujiita Express Red Eagles. Yanga
ilifungwa bao 1-0 ugenini licha ya suluhu ya nyumbani.
Mwaka 1998 ndio angalau
Yanga ilifanya maajabu kwa kucheza hatua ya Ligi Ndogo. Ilianza kwa kuitoa
Rayon Sport ya Rwanda kwa faida ya bao la ugenini baada ya kutoka 2-2 Kigali na
kulazimishwa sare ya 1-1 dar es Salaam; kwenye raundi ikakumbana na Coffee FC
ya Ethiopia na kuishindilia jumla ya mabao 8-3.
Katika hatua ya robo
fainali (makundi) ikavurunda mno na kuishia kuburuza mkia baada ya kufungwa
mechi nne na kuambulia sare mbili tu.
Kwara United ikafaidika
na mgogoro ndani ya Yanga 1999 baada ya kuiondoa kwa jumla ya mabao 4-0 kwenye
Kombe la CAF, ambapo Yanga ilikubali kuchapwa mabao 3-0 nyumbani katika mchezo
wa Machi 28, ambao inadaiwa kwamba kulikuwa na hujuma.
Kwenye Kombe la Washindi
2000, Zamalek ya Misri ikaitoa Yanga kwa jumla ya mabao 5-1.
Mwaka 2001 kwenye Ligi
ya Mabingwa Yanga ilianza kwa kuitoa Highlanders ya Zimbabwe baada ya mchezo wa
marudiano kuvunjika. Awali timu hizo zilitoka sare ya 2-2 jijini Dar es Salaam.
Katika raundi ya pili,
Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ikaifunga Yanga jumla ya mabao 6-5.
Mwaka 2006 kwenye Ligi
ya Mabingwa, Yanga ilitolewa na Zanaco ya Zambia kwa jumla ya mabao 3-2, lakini
mwaka 2007 ilirudia kidogo kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwakama si
kutolewa na Esperance ya Tunisia kwa jumla ya mabao 3-0. Ilianza kwa kuifunga
AJSM ya Mutsamudu Comoro mabao 5-1 katika mchezo ambao haukuwa na marudiano,
kwenye raundi ya pili ikaitoa Petro Atletico ya Angola kwa jumla ya mabao 3-2.
Baada ya kutolewa na
Esperance, ilibidi icheze hatua ya Intermediate dhidi ya timu zilizotolewa
kwenye Kombe la Shirikisho ili ifuzu robo fainali ya kombe hilo, lakini
ikachapwa na El Merreikh ya Sudan mabao 2-0.
Kwenye Kombe la
Shirikisho mwaka 2008, Yanga ilianza kwa kuitoa AS Adema ya Madagascar kwa
mabao 2-1, lakini ikaondolewa na Al Akhdar ya Libya kwa mabao 2-1 pia.
Mwaka 2009 Yanga
ikashiriki Ligi ya Mabingwa ambapo ilivuka raundi ya kwanza kwa ulaini baadaya
kuichabanga Etoile d'Or (Mirontsy) ya Comoro kwa jumla ya mabao 14-1 (ikishinda
8-1 nyumbani na 6-0 ugenini), lakini Al Ahly ya Misri ikawa mwiba kwake baada
ya kuifunga jumla ya mabao 4-0 kwenye raundi ya pili.
Mwaka 2000 Yanga
iliyaaga mapema mashindano ya Ligi ya Mabingwa baada ya kutolewa na FC
Saint-Eloi Lupopo ya Congo Kinshasa kwa jumla ya mabao 4-2.
Katika mashindano ya
Kombe la Shirikisho mwaka 2011, Yanga ikatolewa mapema na Dedebit ya Ethiopia
kwa kufungwa jumla ya mabao 6-4.
Mwaka 2012 katika Ligi
ya Mabingwa, yanga ilitolewa na Zamalek ya Misri katika raundi ya awali kwa
jumla ya mabao 2-1.
Mwaka 2014, licha ya
kupata ushindi mnono wa jumla ya mabao 12-2 dhidi ya Komorozine ya Comoro
kwenye raundi ya awali, safari yake ikarudia Cairo kwa Al Ahly baada ya
kutolewa kwa mikwaju ya penalti kufuatia matkeo ya jumla kuwa sare ya 1-1
(Yanga ilishinda 1-0 nyumbani, ikafungwa 1-0 ugenini).
Wengi wanajiuliza, mwaka
huu wakongwe hao watavuna nini?
0656-331974
IMECHAPWA MARA YA KWANZA NA GAZETI LA SUPASPOTI
No comments:
Post a Comment