Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday, 19 April 2015

MANUSURA ASIMULIA: KILICHOSABABISHA AJALI YA KIWIRA, MBEYA HIKI HAPA!

Mmoja wa manusura  wa ajali iliyotokea eneo la Mto Kiwira, Rungwe mkoani Mbeya, Mariam Manfredy akiwa amelazwa kwa matibabu katika  Hospitali ya Rufaa Mbeya.  Picha na Godfrey Kahango. 
Na Godfrey Kahango na Amanyisye Ambindwile, Mwananchi
Mbeya/Tukuyu. Mmoja wa majeruhi wa ajali iliyoua watu 19, Mariam Manfredy (28) aliyevunjika mguu wa kushoto, anasimulia ajali hiyo na kusema chanzo ni mwendo kasi na kuungua kwa breki.
Gari hilo lilikuwa ‘limeshona’ abiria, lilikuwa likitoka jijini Mbeya  kwenda Kiwira wilayani Rungwe kabla ya kuanguka eneo la Mto Kiwira na kuua watu 18 palepale na mmoja alifia Hospitali ya Igogwe huku wengine watatu wakijeruhiwa.
Mariam aliyelazwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya (MRH), alisema alipanda basi hilo katika Kijiji cha Simambwe akienda Kiwira kununua bidhaa za biashara.
 “Tulipofika Kijiji cha Ndaga, magurudumu yalianza kutoa cheche na moshi jambo lililomfanya kondakta kuteremka na kuzima kwa maji na kwamba wengi walisema breki zimeungua kwa kuwa kulikuwa na harufu kali ya kitu kinachoungua.
“Baada ya kuzima moto kwenye matairi hayo, dereva aliendelea na safari kwa kasi na ndipo basi lilipoongeza kasi kubwa ambayo iliwafanya abiria wote wapige kelele kumtaka dereva apunguze mwendo, lakini yeye hakusema lolote.
“Mimi nilikuwa nimesimama mlangoni na kondakta wa gari hilo na hata ajali hiyo ilipotokea sikuiona bali alijikuta nikiwa kwenye maji hadi nilipookolewa na wasamaria wema.
“Nilipotokea ni kama Mungu tu hakutaka nife…gari ilipinduka vibaya na wengi wamekufa, jamaa zangu na wengi tulikuwa tunakwenda kununua bidhaa kwa ajili ya biashara zetu.”
Katika ajali hiyo watu 19 walipoteza maisha na hadi jana maiti 15 kati ya 18 zikichukuliwa na ndugu zao.
Hospitali ya Rufaa ya Mbeya ilifurika umati wa watu waliokuja kushuhudia na kutambua majeruhi pamoja na kuchukua miili ya jamaa zao.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Aminiel Ngamuo  alisema baada ya ajali ndugu wa marehemu walimimika juzi jioni kuzitambua na walifanikiwa kuwatambua ndugu zao huku maiti tatu za wanaume zikiwa zimebaki hadi jana mchana.
Hata hivyo Dk Ngamuo alishindwa kutaja majina ya waliotambuliwa akisema majina yalifungiwa kwenye ofisi zingine.
Maeneo mengi ya mkoa wa Mbeya yalikuwa na vilio hasa katika maeneo ya Iyunga, Nzowe, Uyole na Mwanjelwa ambako abiria hao walitokea.
94 wapoteza maisha Aprili
Jumla ya watu 94 wamepoteza maisha katika matukio mbalimbali ya ajali zilizotokea kuanzia Aprili Mosi hadi Aprili 17 pekee nchini.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini chanzo kikubwa cha ajali hizo ni mwendo kasi wa madereva na ubovu wa miundombinu katika barabara  nyingi nchini.
Miongoni mwa ajali zilizotikisa nchi kwa mwezi April ni kama ifuatavyo
April 17
Gari ndogo aina ya Toyota Hiace lilitumbukia mtoni katika eneo la Kiwira wilayani Rungwe mkoani Mbeya na kusababisha vifo vya watu 19.
Katika ajali hiyo walifanikiwa kupona watu wawili akiwemo utingo huku chanzo chake kikielezwa kuwa ni mwendo kasi wa kipanya hicho hali iliyosababisha breki kugoma.
Siku hiyo hiyo wachimbaji wadogo 19 wa dhahabu waliokuwa katika mgodi wa Kalole wilayani Kahama walipoteza maisha baada ya kufunikwa na kifusi kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.
Aprili 15
Basi la Air Jordan lilipinduka wilayani Nzega barabara ya kwenda Igunga, mkoani Tabora na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi kadhaa akiwemo mwanamke mmoja aliyekatika mkono.
Aprili 12
Watu 18 waliteketea kwa moto baada ya basi la Kampuni ya Nganga Express na lori aina ya Fuso kugongana uso kwa uso na kuwaka moto katika eneo la Iyovi, Milima ya Udzungwa, Morogoro.
April 10
Gari aina ya fuso liligongana na powertiller katika kijiji cha Endasak wilaya ya Hanang’ na kusababisha vifo vya watu saba.
Siku hiyo hiyo basi la Nyahunge liligongana na gari ndogo ya Toyota Mark II mkoani Mwanza na kusababisha vifo vya watu wanne.
Mkoani Iringa mtu mmoja (mwanafunzi) alipoteza maisha baada ya kugongwa na gari aina ya Toyota Costa.
April 9
Watu 12 walifariki dunia katika ajali iliyohusisha magari matatu  eneo la Mkata, Kijiji cha Mbweni wilayani Handeni Mkoani Tanga. Magari yaliyohusika ni mabasi ta Ratco, Shengena na gari dogo aina ya Passo.
Siku hiyo hiyo basi la kampuni ya Happy Nation lililokuwa linatoka Dar es Salaam kwenda Mbeya lilipata ajali na kusababisha vifo vya watu wawili.
April 7
Watu watatu  walipoteza maisha wilayani Butiama baada ya lori kuacha njia na kuwagonga watembea kwa miguu.
April 3
Gari aina ya Toyota Coastal lililokuwa limebeba mashabiki wa Simba waliokuwa wakielekea Kagera lilipata ajali katika eneo la Makunganya mjini Morogoro na kusababisha vifo vya watu saba.
*Nyongeza na Elizabeth Edward.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment