Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday 18 April 2015

CCM YATAKA WANANCHI KUWA MAKINI NA WAGOMBEA

 Katibu wa CCM Wilaya ya Sumbawanga, Bi. Lucy Mfupe
Diwani wa Kata ya Pito, L. Ndasi

Na Prosper Mgimwa, Sumbawanga
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) wilayani Sumbawanga kimewaonya wanachama wake kuwa makini na wagombea wa nafasi mbalimbali wanaojitokeza na kwamba wafanye uamuzi sahihi kumpata mgombea makini atakayekisaidia kupata ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Akizungumza na viongozi na watendaji wa chama hicho wa Kata ya Pito katika kikao cha ndani kilichofanyika katika Kijiji cha Malagano hivi karibuni, Katibu wa CCM Wilaya ya Sumbawanga, Bi. Lucy Mfupe, alisema ingawa muda wa kura za maoni haujafika, ni vyema wanachama hao wakawa makini kuwapata wagombea wanaokubalika na jamii badala ya kurubuniwa.
“Tunahitaji tupate ushindi wa kishindo kuanzia ngazi za chini, hivyo lazima kuteua watu wanaokubalika kuwa wawakilishi wetu katika udiwani na ubunge, chagueni mtu anayeweza kuleta maendeleo, anayekubalika na jamii na ambaye hataweza kutuangusha,” alisema.
Bi. Mfupe aliwataka viongozi na watendaji wa chama hicho kuwahamasisha wananchi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura pamoja na kuipigia kura Katiba Pendekezwa.
Alisema ingawa muda umebaki mfupi, lakini viongozi hao wanapaswa kuandaa mikutano na kuwasomea wananchi Katiba Pendekezwa ili waielewe na kuwahamasisha wajitokeze kuipigia kura.
“Siyo wakati wa kubweteka, ni lazima kuandaa mikutano hata katika makundi na kuwasomea wananchi Katiba Pendekezwa waielewe ili waweze kuipigia kura,” alisema Bi. Mfupe.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2010 hadi 2015, Diwani wa Kata ya Pito, L. Ndasi, alisema sekta ya elimu kwa shule za msingi na sekondari kwenye kata hiyo imeendelea kuboreshwa ikiwa ni pamoja na uandikishwaji wa watoto wa madarasa ya awali hadi darasa la kwanza.
“Wastani wa uandikishwaji watoto kwenye madarasa ya awali umeongezeka kutoka 250 hadi 440 wakati ule wa kuingia darasa la kwanza umeongezeka kutoka 240 hadi kufikia 442,” alisema Ndasi.
Aidha, Diwani huyo alisema kwamba, ufaulu wa wahitimu wa darasa la saba kwenda kidato cha kwanza umeongezeka kutoka 80 hadi 175 na kwamba ufaulu kwa wahitimu wa kidato cha nne katika shule ya Itwelele umeongezeka kutoka daraja la tatu mwaka 2010 hadi kufikia daraja la kwanza kwa mwaka 2014.
Diwani Ndasi alisema kwamba miradi mbalimbali ya maendeleo imetekelezwa katika kipindi hicho ukiwemo ujenzi wa vyumba 6 vya madarasa ya shule za msingi Mpwita na Malagano uliogharimu Shs. 46 milioni, ambapo Shs. 17 milioni kati ya hizo ni michango ya wananchi.
“Tumejenga vyoo katika shule za msingi Azimio, Tamasenga, Pito, Malagano na Mpwita kwa gharama ya Shs. 50,750,000 na kati ya hizo michango ya wananchi ni Shs. 14,750,000,” alisema na kuongeza kwamba halmashauri ya wilaya pia ilitoa jumla ya madawati 157 kwa shule hizo.
Miradi mingine iliyotekelezwa ni ukarabati wa madarasa, ujenzi wa maabara katika shule ya sekondari Itwelele, ujenzi wa zahanati na nyumba za watumishi na kituo cha rasilimali za kilimo na mifugo huku barabara zenye urefu wa kilometa 51 zikiwa zimechongwa kuunganisha vijiji vya kata hiyo.

No comments:

Post a Comment