Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Damian Lubuva.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Damian Lubuva, amesema Tume yake haina mpango wa kuahirisha Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.
Tamko hilo alilitoa jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari. Alisema kuwa viongozi wa siasa wamekuwa wakiwapa hofu wananchi kuwa Uchaguzi Mkuu unaweza kuahirishwa.
Alisema wanasiasa wanadhani kuna njama za kuiwezesha serikali iliyopo madarakani kuendelea wakati kufanya hivyo ni kuvunja Katiba.
Jaji Lubuva alisema nchi haiendeshwi kidikteta hivyo haiwezekani Rais kubaki madarakani, kwani hata Rais mwenyewe anatamani muda ufike aondoke.
Jaji Lubuva alisema kuahirishwa kwa kura ya maoni kusitumike kama kigezo cha kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu.
“Tunatoa rai kwa viongozi wa vyama vya siasa kuacha kueneza hofu kwa wananchi juu ya kuwapo kwa uwezekano wa kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu kutokana na kuchelewa kukamilika kwa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura,” alisema Jaji Lubuva.
Alivitaka vyama vya siasa kuendelea na kampeni zake. Aidha, alisema Tume itaanza zoezi lake la awamu ya pili la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa ya Iringa, Ruvuma, Lindi na Mtwara.
Alisema zoezi hilo litaanza rasmi katika mikoa hiyo Aprili 24, mwaka huu kufuatia kukamilika kwa awamu ya kwanza iliyohusisha mkoa wa Njombe na Wilaya zake leo.
Jaji Lubuva alisema leo wanatarajia kupokea BVT Kits 1,600 ambazo zitawasili kwa ndege ya kukodiwa.
Alisema wakati zoezi hilo likianza wanatarajia kupokea BVT Kits nyingine 1,600 zitatumika katika mikoa ya Dodoma, Mbeya, Katavi na Rokwa ambapo zoezi hilo litaanza Mei 2 mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment