Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi akishika gazeti la Taifa Imara wakati akizu ngumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana . PICHA: TRYPHONE MWEJI
NA BEATRICE SHAYO
Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi amesema anahofia usalama wa maisha yake, kufuatia habari iliyoandikwa katika gazeti moja la kila wiki kwamba, Rais Jakaya Kikwete aliapa kupambana naye jambo ambalo limempa hofu kubwa.
Kadhalika, amelalamikia Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na Idara ya Habari Maelezo kwa kukaa kimya na kuacha kutoa ufafanuzi dhidi ya tuhuma hizo, huku taarifa hizo zikiendelea kusambazwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mengi alisema kuwa tuhuma zilizotolewa dhidi yake kuwa yeye ni kinara wa kuhujumu serikali ya Rais Kikwete siyo za kweli.
Dk.Mengi alisema amesoma kwa masikitiko makubwa habari iliyochapishwa Machi 23, mwaka huu na gazeti la Taifa Imara, yenye kichwa cha habari 'Zitto amchongea Mengi kwa JK' ambapo pamoja na mambo mengine inasema kuwa Zitto Kabwe amemchongea Dk. Mengi kwa Rais Kikwete kwamba ndiye kinara wa kuhujumu serikali yake.
Alisema habari hiyo ambayo chanzo chake kimeelezwa kwamba ni Ikulu, iliendelea kueleza kuwa Zitto alikutana na Rais Kikwete muda mfupi baada ya kuwasilisha bungeni ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusiana na kashfa ya Escrow ambayo Zitto alikuwa ni mwenyekiti wake.
"Habari hiyo inasema kwamba katika mazungumzo yake na Rais Kikwete Zitto amenukuliwa akimueleza mkuu huyo wa nchi kuwa anayesababisha serikali yake iyumbe kila mara ni Mengi," alisema Dk. Mengi.
Dk. Mengi alisema habari hiyo ambayo nakala yake ameiambatanisha kwenye taarifa yake, inasema yeye Zitto , binafsi amekuwa akishawishiwa na Dk. Mengi kuiangusha serikali ya Rais Kikwete.
Hata hivyo, Dk. Mengi alisema katika habari hiyo Zitto alikwenda mbali zaidi kumueleza Rais Kikwete kuwa Dk. Mengi ameapa kuwa Rais Kikwete akimaliza muda wake wa Urais atamshughulikia kwa nguvu zake zote.
Alisema habari hiyo imeeleza kwamba baada ya maelezo hayo, Rais Kikwete aliapa kupambana na Dk. Mengi na akamshukuru Zitto kwa kumpa taarifa hizo.
Mengi alisema tuhuma zilizotolewa kuhusu nia yake ya kutaka kuiangusha serikali ya Rais Kikwete na kumshughulikia baada ya kumaliza muda wake wa uongozi, zimemshtua sana na tamko la kwamba Rais Kikwete aliapa kuwa atapambana na yeye zimempa hofu kuhusu mustakabali wa maisha yake.
Alisema kuwa hofu yake kubwa inasababishwa na Ikulu na Idara ya habari Maelezo kukaa kimya kwa zaidi ya wiki tatu bila kutoa ufafanuzi wowote.
"Najua umakini wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na Idara ya habari Maelezo katika kutoa ufafanuzi wa haraka wa jambo lolote linalomhusu Rais, lakini katika hili nashangaa kuona taasisi hizo zimeamua kukaa kimya na kuacha tuhuma hizo kusambaa,"alisema Dk. Mengi.
Aliongezea kusema kuwa," hofu yangu inazidi kuwa kubwa kwa sababu Rais ni Mkuu wa Majeshi ya ulinzi na usalama. Kauli yake kama ilivyonukuliwa na gazeti hili kwamba atapambana na mimi inawezekana kuchukuliwa kama agizo kwa vyombo vya dola kuniangamiza," alisema.
Alitolea mfano mwaka 1170, Askofu Mkuu wa Canterbury nchini Uingereza aliuawa baada ya walinzi wa mfalme kusikia mfalme akisema "hakuna anayeweza kuniondolea huyo mkorofi?". Walinzi wake wakadhani mfalme ameagiza wamuue Askofu huyo na wakamuua, alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment