Meneja Mawasiliano wa
Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) Innocent Mungy (Kulia) akiongea na wadau
wa Sanaa (hawako pichani) wakati akiwasilisha mada kuhusu matumizi sahihi ya
mitandao ya kijamii kwa wasanii kwenye Jukwaa la Sanaa lililofanyika Jumanne ya wiki hii makao makuu
ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Ilala, Sharif Shamba. Kushoto ni
Mwanasheria wa BASATA Deogratius Nchimbi.
Mwanasheria wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Deogratius Nchimbi (Kushoto) akiongea jambo na wadau wa Sanaa (hawako pichani) mapema wiki hii wakati akihitimisha mjadala kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwa wasanii uliowasilishwa na Meneja Mawasiliano wa mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia programu ya Jukwaa la Sanaa ya Baraza hilo kwenye Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala, Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa wadau wa Jukwaa la Sanaa akiuliza swali kwa Meneja mawasiliano wa TCRA juu ya athari za sheria mpya ya mitandao ya kijamii kwa wasanii na waandishi wa habari.
Sehemu ya wadau wa Sanaa waliohudhuria programu ya Jukwaa la Sanaa ya Baraza la Sanaa la Taifa mapema wiki hii.
Na
Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) na mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA) mapema wiki hii wamelaani
matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii miongoni mwa wasanii wakati wa programu
ya Jukwaa la Sanaa iliyofanyika makao makuu ya Baraza hilo yaliyoko Ilala
Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.
Akiongea wakati
akiwasilisha mada iliyohusu ‘Matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwa
wasanii’, Meneja mawasiliano wa TCRA Innocent Mungy alisema kuwa wasanii ni
kioo cha jamii hivyo kwa namna yoyote ile hawapaswi kuwa sehemu ya uharibifu wa
jamii inayowazunguka au kuharibu wajihi (taswira) yao kwa jamii yao.
“Unapokuwa kioo cha jamii,
unategemewa kuishi kwa kuwa mfano katika jamii yako. Vijana wengi wanaiga
kutoka kwa wasanii ambao ni maarufu. Tunatarajia wasanii wawe mfano kwao”
alisisitiza Mungi.
Aliongeza kwamba, msanii
anapotumia mitandao ya kijamii kwa kuweka picha chafu, zisizo na maadili au
kitu chochote kisicho na staha ni kuchafua wajihi wake mbele ya jamii na hili
linampotezea fursa nyingi za kibiashara na kiuchumi maana hakuna kampuni au
asasi itakayopenda kufanya kazi na msanii mwenye sifa mbovu.
“Wasanii wanapotumia hovyo
mitandao ya kijamii wanachafua wajihi wao katika jamii. Wanajikosesha fursa za
kimapato. Mfano; mfanyabiashara anapotaka kutangaza shule yake ya watoto wa
awali hawezi kutumia msanii mwenye wajihi mchafu na unaoharibu watoto”
aliongeza Mungy.
Alizidi kueleza kwamba
wasanii hawana budi kutumia mitandao hii ya kijamii hususan facebook, twitter,
instargram, u-tube na kadhalika katika kujitangaza na kuuza kazi zao na zaidi
kutenga muda mwingi kutumikia jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Idara ya Ukuzaji Sanaa na Masoko wa BASATA, Vivian Shalua alisema kwamba
Baraza hilo muda wote limekuwa likisisitiza maadili mema miongoni mwa wasanii
maana vijana wengi huwaangalia kama mfano katika maisha yao.
“Kila mara BASATA limekuwa
likisisitiza maadili kwa wasanii wote. Kazi hii ni ngumu na inataka wadau wote
kushiriki katika kunyoosha maadili ya wasanii na vijana kwa ujumla” alimalizia
Shalua.
No comments:
Post a Comment