Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday 18 April 2015

VIJANA, WATOTO 115 WANASWA MAZOEZI YA KARATE DODOMA

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime 
Na Sharon Sauwa na Habel Chidawali
Dodoma. Jeshi la Polisi mkoani hapa limefunga vituo vitatu katika eneo la Nkuhungu baada ya kubaini uwepo wa watoto na vijana 115 kutoka mikoa 13, ikiwa ni pamoja na visiwani Zanzibar, waliokuwa wakilelewa kwenye mazingira hatarishi.
Hata hivyo, kubainika kwa watoto hao ni tofauti na matukio ya mkoani Kilimanjaro ambako Jeshi la Polisi lilibaini zaidi ya watoto 200 waliokuwa wamefungiwa kwa miaka takriban mitatu wakipewa mafunzo ya kisiri na hivyo kuibua hisia za ugaidi.
Katika tukio la Dodoma, polisi imesema inaendelea na uchunguzi kujua walichokuwa wakifundishwa vijana hao.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, kamanda wa polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema watoto hao wanatoka katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Mtwara, Kagera, Tanga, Tabora, Singida, Pwani, Lindi, Geita, Mwanza na Manyara.
Alisema baada ya kupokea taarifa ya uwepo wa watoto hao, walifika katika vituo hivyo saa 6:30 usiku jana na kukuta watoto hao wenye umri wa chini ya miaka 25.
“Polisi iligundua vituo vitatu katika eneo la Nkuhungu, Dodoma Mjini baada ya kupokea taarifa kwamba kuna nyumba ambazo zinaonekana kuingia watoto wengi na inawezekana siyo mazingira salama ya kuishi binadamu hasa watoto na wanachofundishwa huenda ni kinyume cha maadili,” alisema.
Kamanda Misime alisema katika vituo hivyo walipatikana jumla ya watoto 63 wenye umri wa chini ya miaka 18, wakati walio na vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 na 25 walikuwa ni 52. Alifafanua kuwa kati ya watoto hao waliotoka Wilaya ya Kondoa mkoani hapa ni 50 wakati waliotoka wilaya za Dodoma Mjini, Chamwino na Mpwapwa ni watoto 26.
“Uchunguzi unaendelea na yeyote atakayeguswa na ushahidi kuwa amekiuka sheria atafikishwa mahakamani, wakiwemo wazazi walioruhusu watoto kuwa katika uangalizi ambao siyo wa kutosha kama sheria ya watoto ya mwaka 2009 inavyoelekeza,” alisema.
Pia alisema jeshi hilo linachunguza watoto hao walikuwa wakifundishwa kitu gani na kama walikuwa wakihudhuria shule kulingana na umri wao na sheria za nchi zinavyoelekezwa.
Ingawa hakulihusisha tukio hilo na mafunzo ya ugaidi, Kamanda Misime aliwataka viongozi na watu wataka maeneo kama hayo katika himaya zao na vituo visivyosajiliwa ambavyo ni hatarishi kwa watoto, watoe taarifa mapema.
Pia alitoa wito kwa familia, viongozi wa serikali za mitaa, dini na taasisi nyingine kutoruhusu watoto wao kupelekwa na kuelelewa katika vituo hatarishi.
Aidha, aliwataka wazazi wanaofahamu watoto hao wajitokeze ili kupewa maelekezo kabla ya kutafutwa na mkono wa dola.
Mkuu wa wilaya ya Dodoma Mjini, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Betty Mkwasa alisema jana kuwa aliyoyaona katika kituo hicho hayakubaliki.
“Kwanza watoto wanalala wengi, hakuna hewa ya kutosha, wanajipikia wenyewe chakula na hawana uangalizi wa watu wazima,” alisema Mkwasa.
Alisema serikali haikatai dini yoyote kufundishwa kwa watoto bali taratibu, kanuni, sheria pamoja na haki za mtoto lazima zifuatwe.
“Siwezi kujua walikuwa wanafundishwa nini lakini baada ya upembuzi yakinifu utakaofanywa na wataalam ambao nimekuja nao, tutaweza kuzungumza kama walifuata kanuni na utaratibu,” alisema.
Mwananchi ilipofika katika moja ya kituo hicho, jana asubuhi lilikuta watoto hao wakicheza kwenye eneo hilo lililokuwa chini ya ulinzi wa polisi waliokuwa na silaha za moto.
Watoto wengi walikuwa hawajavaa viatu na baadhi yao walisema kuwa viatu walivyokuja navyo kutoka makwao vimeshakwisha.
Bakwata
Sheikh mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Shaaban Rajabu alisema wanakitambua kituo hicho kama ilivyo kwa vituo vingine vinavyofundisha dini ya Kiislamu.
Sheikh huyo alipinga suala la watoto kukosa elimu, akisema wazazi wao wamehiyari vijana wao kusoma dini tu.
“Naomba ifahamike kuwa, wapo wazazi ambao wanapenda watoto wao wasome dini tu na hata mimi nilisoma hivyo kabla ya kwenda nje kwa masomo zaidi na kurudi,” alisema.
Alipinga suala la kusajiliwa kwa kituo akisema viko vituo vingi havijasajiliwa hata katika dini nyingine, lakini havisumbuliwi na kushangazwa kuona utaratibu wao unakuwa na shida.
Kwa upande mwingine alishauri Bunge kutunga sheria kali kwa ajili ya kuvilazimisha vituo vyote kuwa na usajili ili viweze kufuatiliwa kulingana na matakwa ya serikali.
Kwa upande wake, katibu wa Bakwata mkoani hapa, Hassan Kuzungu, aliyeongozana na kamati hiyo, alieleza kusikitishwa na kitendo cha mazingira waliyokuwapo watoto hao.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Nkhungu, Kasian Mponela alisema kuwa amekuwa akiwaona watoto hao, lakini hajui wanachojifunza hapo.
Alisema suala la kuangalia kama wanajifunza dini au mambo mengine sio jukumu lake, kwani yeye anajua kila mtu anapanga mwenyewe matumizi ya nyumba yake.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment