Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima.
NA MOSHI LUSONZO
Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, jana alijisalimisha Makao Makuu ya Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, baada ya nyumba yake kuzingirwa na polisi kwa saa saba, kutokana na kushindwa kuwasilisha nyaraka za umiliki wa mali zake.
Tukio hilo lilitokea eneo la Salasala, mtaa wa Kilimahewa, ambapo Polisi wakiwa na silaha mbalimbali pamoja na magari sita walikaa nje ya nyumba hiyo wakiweka doria kwa nia ya kumkamata.
Hali hiyo iliyoanza majira ya saa 12:00 asubuhi ilisababisha Askofu Gwajima, kukaa ndani hadi pale polisi walipoondoka majira ya saa 6:30 mchana.
NYARAKA ANAZODAIWA
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana eneo hilo zinasema alitakiwa kurudi kituoni hapo juzi akiwa na vielelezo 10 vya umiliki wa mali.
Vilitajwa vielelezo hivyo kuwa ni hati ya usajili wa kanisa lake, nyaraka za idadi ya makanisa anayomiliki pamoja na kuwasilisha muundo wa uongozi wa kanisa lake.
Viingine ni idadi ya nyumba na mali ambazo kanisa linamiliki, nyaraka ya umiliki wa helikopta na muundo wa Bodi ya Wadhamini wa Kanisa pamoja na majina yao.
Aidha vingine ni returns (makusanyo) ya kanisa, kumpeleka mtu anayepiga picha za video katika kanisa lake, waraka ulioandaliwa na Maaskofu wa Jukwaa la Wakristo pamoja na namba ya usajili ya kanisa analomiliki.
Hata hivyo, hadi kufikia juzi, Askofu Gwajima, hakuripoti kituoni hapo na hakutoa taarifa jambo ambalo ilielezwa ni kuvunja sheria ya jeshi hilo.
“Askofu alitakiwa kufika kituoni tangu majuzi kuwasilisha nayara zake, lakini hakutokea kitu ambacho wakuu wetu walituamuru tuje kumkamata,” alisema polisi mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake.
HALI HALISI
Hekalu la Gwajima, ni maarufu eneo la Salasala kwa jina la `Ngome kuu’ kutokana na kujengwa katika mtindo wa aina yake unaomzuia mtu yeyote kuingia ndani.
Jumba hilo la ghorofa mbili limezungushiwa ukuta imara wenye urefu wa mita tano kwenda juu na uzio wa waya wa umeme.
Hata hivyo, jana watu walikuwa hawashangai uzuri wa jumba hilo, badala yake walikuwa wakiangalia jinsi polisi walivyotanda kila kona ya nyumba hiyo.
Polisi hao waliokuwa ndani ya magari sita, walihakikisha kwa muda wote hakuna mtu anayeingia wala kutoka kwenye nyumba hiyo.
Magari hayo ni Landrover nne zenye namba T337 AKV, PT 1686, PT 2083, T475 BNM. T 848 na gari moja namba yake haikupatikana.
Kundi kubwa la waumini wake waliomiminika wakitoka katika kanisa lake lililopo eneo la Kawe, walizuiwa eneo la mita 100 kutoka nyumba hiyo baada ya polisi kuweka kizuizi.
Baadhi ya waumini hao walisikika wakilalamikia kitendo hicho kwa maelezo kwamba kiongozi wao hastahili kutafutwa kwa nguvu kubwa kama iliyoonekana jana kwani yeye siyo mhalifu wa Kimataifa.
“Tunachoshuhudia hapa ni kama baba Askofu ni gaidi au amefanya uhalifu wa kimataifa, hii siyo haki lazima serikali itambue yeye ni kiongozi wa kiroho lazima apewe heshima zake,” alisema Mchungaji Miriam Elia.
MWENYEKITI WA MTAA ANENA
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kilimahewa, Richard Njela, alithibitisha polisi kufika eneo hilo kumkamata Askofu Gwajima baada ya kutotii amri halali ya polisi.
“Niliwauliza polisi ana kosa gani, walinijibu kwamba hakutii agizo la kuripoti kituoni, hivyo kwa upande wangu siwezi kufuatilia sana kwa sababu lipo kisheria zaidi,” alisema Njela.
MAJIRANI HOFU TUPU
Baadhi ya majirani wa Askofu Gwajima, walisema kwamba kutanda kwa polisi katika eneo lao liliwapa hofu kutokana na nyumba hiyo kuwa na matukio ya utata kila mara.
Walisema baadhi ya matukio yaliyowahi kutokea ndani ya nyumba hiyo ni kusikika milio ya risasi ya bastoka kila mara.
“Tulishtuka kuona polisi wanakuja asubuhi na kuzingira nyumba, tulidhani inatokana na milio ya risasi inayotoka ndani ya nyumba kwa sababu kwetu imekuwa kero,” alisema mkazi mmoja wa eneo hilo ambaye hakutaja jina lake.
Hata hivyo, walisema wao hawajamuona Askofu Gwajima hata mara moja kutokana na nyumba hiyo kujengwa kama ngome na magari anayotumia yanapewa ulinzi mkali na walinzi wake.
POLISI WAONDOKA
Ilipofika majira ya saa 6:30, Polisi walianza kuondoka katika eneo hilo baada ya kuwapo kwa maafikiano kati ya viongozi wa Pentekosti na jeshi la polisi.
Moja ya sharti walilokubaliana ni kiongozi huyo ajisalimishe mwenyewe kituoni ndani ya saa moja kuanzia muda huo na endapo hatatii basi akamatwe mara moja.
Ilipofika saa 7:00 mchana Askofu Gwajima alitoka ndani akiwa ndani ya gari dogo lenye vioo vya kiza na kuelekea polisi.
Kabla ya kuondoka Mwanasheria wake, Peter Kibatala, aliwaambia waandishi wa habari kwamba mteja wake ameitwa ofisi ya Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam lakini hadi wakati huo hawafahamu ni kitu gani anachoitiwa.
AFIKISHWA MAHAKAMA YA KISUTU
Gwajima alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka mawili, likiwemo la kumtukana Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycard Kardinali Pengo pamoja na kushindwa kutunza silaha anazozimiliki kihalali.
Akisomewa mashtaka hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Wilfred Dyansobela, huku upande wa Jamhuri ukiongozwa na wakili wa serikali Shedrack Kimaro akisaidiana na Joseph Maugo.
Wakili Maugo alieleza mahakama kuwa tarehe isiyofahamika, akiwa viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe alitoa lugha ya matusi na kumkashfu Kardinali Pengo.
Katika shitaka la pili Gwajima alishatakiwa kwa kushindwa kuhifadhi silaha pamoja na risasi kuziweka katika usalama kinyume cha sheria ya silaha ya vyombo vya moto ambayo anamiliki kihalali.
Katika shitaka hilo hilo maaskofu pamoja na wachungaji watatu wa Kanisa la Gwajim ambao ni Yekoma Bihagaze, Jofrey Andrew na George Mzava waliunganishwa kwa kushitakiwa kukutwa na silaha kinyume cha sheria na taratibu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment