Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday, 20 April 2015

WIZI WA MAGARI NI BALAA TUPU


Dar es Salaam. Wezi wa vifaa vya magari jijini hapa wameunda mtandao mzito kama vile wana ‘serikali yao’ inayowalazimisha waathirika kuacha kutoa taarifa polisi badala yake kwenda kununua upya vifaa kwa wezi hao.
Licha ya wizi wa vifaa, kumekuwa na wizi mkubwa wa magari Dar es Salaam kiasi kwamba mwaka 2013, magari yaliyoibwa ni 400. Mwaka 2014 yaliibwa 375 na kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu magari 70 yameibwa.
Kutokana na hali hiyo, polisi jijini Dar es Salaam wamelaumiwa kwa kushindwa kutokomeza mtandao huo, licha ya wahusika kufahamika kwa majina, makazi na mahali wanakohifadhi vifaa hivyo vya wizi.
Hata hivyo, polisi nao kwa upande mwingine wametupa lawama kwa wananchi wanaoibiwa vifaa hivyo, kuwa hawatoi ushirikiano kwa jeshi hilo badala yake wameona njia rahisi ni kwenda kununua upya mali zao kwa wezi hao.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa baadhi ya wananchi walioibiwa vifaa hivyo wanakataa kutoa taarifa polisi kwa kuhofia kupoteza muda, gari kubaki polisi kama kielelezo hadi vifaa vipatikane, kutakiwa kutoa fedha kwa wapelelezi au kuhisi kuwa baadhi ya askari wanahusika na mtandao huo.
Baadhi ya wakazi wa jiji waliowahi kuibiwa vifaa hivyo wamesema haichukui muda mrefu kwa mtu kubaini mahali vilipo na kuvipata tena, lakini kwa polisi wenye kila ujuzi kiupelelezi limeendelea kuwa tatizo.
Vifaa vinavyoibwa zaidi
Kutokana na uchunguzi wa gazeti hili, vifaa vinavyohitajika zaidi kwa sasa ni side mirror, control box, power window, vioo vya mbele na nyuma, taa, dash board, redio na baadhi ya vifaa vya injini.
Magari ambayo vifaa vyake vinaibwa zaidi ni yale yanayopatikana kwa wingi hasa aina ya Toyota na Suzuki, yakiwamo Escudo, Altezza, Mark II Grand, Cresta, Verossa, Noah, Ipsum, Klugger, Harrier, Vitz na Ist ambayo kutokana na wingi wake vifaa hivyo hupata wateja haraka.
Katika uchunguzi huo Mwananchi limebaini kuwa, watu wanaoharibikiwa magari, kugongwa au kuibiwa vifaa kwa siku ni wengi kwa hivyo wezi hupata uhakika wa kuuza vifaa hivyo.
Kauli ya polisi
Mkuu wa Upelelezi, Kanda ya Dar es Salaam, Constantine Massawe alipoulizwa sababu za kukithiri kwa tatizo hilo, alisema wizi wa vifaa vya magari unashughulikiwa kama uhalifu mwingine, lakini jeshi hilo halipati ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi wanaoibiwa vifaa hivyo.
“Watu wengi hawataki kuripoti polisi pale wanapoibiwa. Wameshajizoesha kuwa wakiibiwa vifaa vya magari wanakwenda kuvinunua tena, kwa hiyo unakuwa ni mzunguko, unaibiwa unavinunua, unaibiwa tena unavinunua,” alisema Massawe.
Alipoulizwa kama hatua hiyo ya wananchi inatokana na kukosa imani na polisi, Massawe alisema jeshi hilo linashughulikia tatizo hilo na baadhi ya wezi wa vifaa hivyo na wengine wa magari walikwishakamatwa.
Mbali na wizi wa vifaa hivyo, Massawe alisema hata magari yamekuwa yakiibwa kwa wingi jijini Dar es Salaam.
Kwa mfano, alisema kwa mwaka 2013, magari yaliyoibwa ni 400. Mwaka 2014 yaliibwa 375 na kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu magari 70 yamekwishaibwa.
Waathirika wasimuliwa
Mkazi wa Tabata Kisukuru, Zena Musa alilieleza gazeti hili kuwa Julai mwaka jana vifaa vya gari lake aina ya Harrier vikiwamo power window, taa, redio, side mirror viliibwa na kioo cha mbele kuvunjwa.
“Nilitumia zaidi ya Sh4 milioni kununua vifaa vipya, hata hivyo bado gari limekuwa bovu kwa sababu walinyofoa bila utaratibu,” alisema.
Zena alisema pamoja na kutoa taarifa polisi vifaa vyake havikupatikana wala hakupata taarifa za kutia moyo.
Mkazi wa Buguruni, Salim Rashid alisema aliamua kufuatilia vifaa vyake Gerezani, Kariakoo badala ya kwenda polisi kwa kuhisi atapoteza muda mwingi bila sababu na waliomwelekeza mahali vifaa vyake vilipo walisema akiwaeleza polisi hatavipata, atalazimika kununua vipya kwa bei mbaya.
“Nilipima nikaona bora nivinunue vifaa vyangu kwa bei ndogo kuliko kwenda kununua vipya dukani kama ningefuata utaratibu wa polisi,” alisema Rashid.
Mkazi wa Yombo Vituka, Mwansasu Mwaipopo alisema vifaa kama hivyo vilipoibwa katika gari lake aina ya Vitz hakuona haja ya kutoa taarifa polisi kwa kuwa aliona hata akifanya hivyo hawezi kuvipata, hivyo aliingia mitaani na kupata vifaa vyake vilevile baada ya siku moja.
Mbali na Gerezani, maeneo mengine yaliyotajwa kuhusika na mtandao wa vifaa hivyo ni Ilala, Kariakoo na maduka mbalimbali yanayouza vifaa vilivyotumika.
Mwandishi wa habari hizi aliyejifanya ameibiwa vifaa vya gari aina ya Altezza, alikutana na fundi gereji mmoja wa eneo la Ilala na baada ya kupewa maelezo ya mahali na tarehe vilipoibwa, walikubaliana vitafutwe ili avinunue tena.
“Kwa kifupi ili kupata vifaa vyako vilevile ni lazima uwahi siku moja hadi tatu baada ya kuibwa,” alisema fundi huyo na vilitafutwa, ingawa vilipatikana vingine vinavyofanana kwa kuwa tukio halikuwa la kweli.
Mwananchi limebaini kuwa wauzaji huwa makini wakiogopa kumuuzia mwenye gari kwa hofu ya kukamatwa, badala yake huwauzia wenzao waliopo kwenye mtandao wao. “Ukitaka vifaa vyako usiingie kichwa kichwa, lazima umtafute mtu anayefahamiana nao au ambaye yupo kwenye mtandao wao,” alisema Kazibure Sadiki, fundi gereji, Gerezani, Kariakoo.
“Kama thamani ilikuwa Sh1 milioni mtu anaweza kuvipata kwa Sh500,000, anachotakiwa yeye ni kuwaamini tu hao vijana na asijionyeshe kuwa ni mwenye gari. Mkishakubaliana, unaweza kuvipata kwa dakika 20 hadi 30 tu.
Mbinu za wizi
Mwananchi limebaini kuwa, wezi hao huvunja vioo vidogo vya magari kwa kutumia mafuta maalumu ya nywele kwa kuyamwaga kwenye kioo kisha kukigonga taratibu kwa kutumia chuma au spana na kukipasua bila mlio mkubwa.
Chanzo cha habari kimedokeza kuwa iwapo gari lina king’ora cha tahadhari, huitoa kwa kuweka sumaku kwenye boneti ambayo hukata mawasiliano, hivyo kutimiza uhalifu huo bila kushtukiwa.
“Mara nyingi mwizi ni lazima awe na uzoefu mkubwa wa ufundi wa magari, hivyo hujua kifaa kinavyochomolewa, mahali kilipo na kazi yake katika gari,” alisema mmoja wa mafundi gereji, eneo la Ilala.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, wezi wa vifaa vya magari huzunguka na pikipiki katika maeneo mbalimbali ili kuchunguza nyumba zinazolaza magari nje, wakishazibaini, hutafuta ramani ya kutekeleza uhalifu huo.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment