Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday, 17 April 2015

MKWARA WA GWAJIMA KWA KOVA WAZAA MATUNDA

Kamanda Kova 
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Hoja za kisheria alizowasilisha Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuhusu kutakiwa kuwasilisha nyaraka 10 za utajiri na usajili wa kanisa lake polisi zimezaa matunda.
Sasa, agizo la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam la kumtaka Askofu Gwajima kuwasilisha nyaraka hizo leo limesitishwa kusubiri utatuzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka.
Wakili John Mallya anayemtetea Askofu Gwajima alilieleza gazeti hili jana usiku kuwa baada ya makubaliano na polisi mteja wake leo hatafika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kama ilivyokuwa imepangwa mpaka hoja hizo za kisheria zitakapotolewa uamuzi.
Alhamisi iliyopita, polisi ilimtaka Gwajima kuwasilisha vielelezo hivyo, lakini hatua hiyo ilipingwa na kiongozi huyo akieleza kuwa hatapeleka nyaraka yoyote iwapo jeshi hilo halitajibu barua aliyoliandikia kutaka liombe vitu hivyo kwa maandishi.
Nyaraka zilizotakiwa kuwasilishwa polisi ni hati ya usajili wa kanisa, namba ya usajili, majina ya Baraza la Wadhamini (Baraza la Kiroho), idadi ya makanisa (matawi) anayohudumia na nyaraka za helikopta ya kanisa.
Nyaraka nyingine ni; muundo wa uongozi wa kanisa, waraka wa maaskofu uliosomwa makanisa yote, nyaraka za nyumba na mali za kanisa, nyaraka kuonyesha taarifa za hesabu kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Hiari na kuambatana na mtu anayepiga picha za video kanisani hapo.
“Siwezi kuwasilisha kwa mdomo kwa kuwa hizi si mali za Gwajima… ni mali ya taasisi na si vitu vyake binafsi,” alisema wakili huyo.
Katika barua yake kwa polisi, Wakili Mallya alisema: “Tunaiomba Polisi kumwandikia rasmi mteja wetu kimaandishi nyaraka mnazozihitaji na vifungu vya sheria vinavyotumika na polisi kutaka nyaraka hizo… tutashukuru kupata hati hiyo.”
Kauli ya Kova
Mapema alipoulizwa kuhusu kitakachotokea leo, Kamanda Kova alisema: “Suala la Mchungaji Gwajima kwenda na vielelezo alivyoagizwa na Polisi siwezi kulizungumzia hadi hapo itakapotokea hakuja navyo ndipo nitakapotoa tamko langu la mwisho.
“Nitazungumziaje hili? Si hadi itokee hakuja na vielelezo na kama akija navyo halafu mimi nimeongea tofauti, nimeona italeta malumbano kati yangu na yeye na mimi sitaki ifikie huko.
“Kuna mambo mengi ya kufanya hivyo nitalitolea tamko la mwisho kwa waandishi wa habari kuhusu mchungaji Gwajima kama itatokea hivyo ili tuendelee na mambo mengine.”
Kwa msisitizo zaidi
Mallya alisema nchi inaongozwa kwa sheria, hivyo kila kitu kinatakiwa kiwe cha kisheria na kwamba wameiandikia polisi kuitaka waombe nyaraka hizo kimaandishi na kuonyesha vifungu vya sheria vinavyowaongoza kuziomba badala ya kusema kwa mdomo kwa sababu vitu hivyo ni vya kanisa na siyo vya Gwajima peke yake.
Askofu Gwajima alihojiwa na Polisi, Kanda ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kumtolea maneno makali Polycarp Kardinali Pengo baada ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki kutoa tamko lililotofautiana na la viongozi wa Jukwaa la Wakristo Tanzania kuhusu suala la Katiba.
Nyongeza na Pamela Chilongola
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment