Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa shule ya Sekondari Uyui mjini Tabora Zitto alisema Tanzania ni moja ya nchi zilizojaliwa kuwa na rasilimali nyingi zinazoweza kubadilisha mfumo wa maisha ya wananchi wake lakini mfumo wa uchumi uliopo haujajikita kumkomboa mnyonge.
Alieleza mfumo wa uchumi wa nchi hii ni mfumo wa kinyonyaji ambao hauwajali wananchi ndio maana unawanufaisha watu wachache pekee na serikali imeshindwa kutumia utajiri wa rasilimali zilizopo kubadilisha maisha ya wananchi wake ikiwa ni pamoja na kuzalisha ajira nyingi.
Alisema uchumi wetu unakua kwa asilimia 7 tu kila mwaka, na ajira milioni 1.6 zinahitajika hapa nchini kwa kila mwaka lakini hakuna mkakati thabiti wa kuinua kiwango hicho au kuzalisha ajira nyingi zaidi kupitia fursa zilizopo katika kilimo, viwanda na biashara.
Alifafanua ACT-Wazalendo inataka kutetea uwepo wa mfumo mzuri wa kisheria utakaomsaidia mkulima wa tumbaku na mazao mengine kujiwekea akiba kidogo kidogo ikiwemo kumhamasisha kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kumwinua zaidi kiuchumi.
Wakati huo huo Kiongozi huyo Mkuu wa ACT Wazalendo ameeleza ili kuking’oa madarakani Chama Cha Mapinduzi hawana budi kuwa na umoja wa ushirikiano na vyama vingine vya upinzani kwa kusimamia mambo ya msingi yanayowagusa wananchi walio wanyonge na sio kugawana vyeo.
Alisema kazi ya ACT sio kukosoa au kulumbana na chama chochote cha siasa, wapo tayari kuungana na UKAWA kama tu watakuwa na dhamira ya dhati ya kurejesha misingi ya uzalendo iliyoasisiwa na Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere ya kumkomboa mwananchi aliye mnyonge.
Kama tutaungana na kuelekeza nguvu zetu katika masuala yanayolenga kuboresha maisha ya mwananchi wa kawaida, kuinua uchumi wa nchi ili kuzalisha ajira kwa vijana walio wengi na kuboresha suala zima la elimu na afya ili iweze kupatikana kwa wananchi wote, litakuwa jambo la maana sana, aliongeza.
Alisema katika uchaguzi mkuu uliopita (2010) asilimia 42 tu ya Watanzania wote ndio walipiga kura wakati asilimia 52 hawakujitokeza kupiga kura na utafiti umebainisha baadhi ya sababu za watu wengi kutopiga kura hawaoni kama kuna jitihada za dhati za kumaliza matatizo yao, jambo ambalo chama chake kimekusudia kulifanyia kazi kwa vitendeo.
Mwenyekiti wa Taifa wa ACT Wazalendo Bi.Anna Mgwira alieleza kuwa ACT imedhamiria kurejesha misingi ya Azimio la Arusha iliyopotea ili kudumisha umoja, undugu, uzalendo, uwajibikaji katika jamii na kusaidiana kuondoa wezi wote wa rasilimali za nchi lengo likiwa kumkomboa mnyonge.
No comments:
Post a Comment