Na Pamela Chilongola
Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Mark Bomani ameshauri Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa iahirishwe na badala yake Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iendelee kuboresha Daftari la Wapigakura.
Pia, alisema Serikali iachane na mfumo wa uandikishaji wananchi wa Biometrick Voters Registration (BVR) kwa kuwa ilikurupuka bila ya kufanya maandalizi ya kutosha na fedha na vifaa havitoshi kuendeshea mpango huo.
Jaji Bomani alisema jana kuwa mujibu wa Tangazo la Rais, Kura ya Maoni itapigwa Aprili 30 mwaka huu, lakini walioandikishwa hawazidi milioni moja.
Alisema Serikali ikilazimisha upigaji kura, itasababisha mgogoro mkubwa na manung’uniko mengi nchini.
“Hadi hii leo, uandikishaji wapigakura bado unasuasua, zaidi ya watu milioni 20 wataweza kweli kuandikishwa katika wiki nne zilizobaki?
“Itakuwa ni muujiza kufanya hivyo na ni Mkoa wa Njombe tu ambao wanaendelea kuandikishwa,” alisema Jaji Bomani.
Alisema Tume ya Jaji Joseph Warioba ya kukusanya maoni, ilifanya kazi kwa umakini na kukamilisha Desemba 2013 na kuitishwa Bunge Maalumu la Katiba liangalie ripoti ya Rasimu Iliyopendekezwa.
Alisema Bunge lilifanya kazi yake, lakini ilikuwa siyo nzuri, hivyo kusababisha baadhi ya wajumbe kutoka nje ya ukumbi kwa kutofautiana.
“Katiba haitegemei kura za washiriki wachache wanaokubali ndiyo na hapana, bali kupata Katiba Mpya kwa maelewano ya kila upande,” alisema.
Pia, alisema baadhi ya mambo mazuri yaliyomo kwenye Katiba Inayopendekezwa yafanyiwe mabadiliko ili yatumike kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Wakati Jaji Bomani akisema hayo, tamko lilitolewa tume hiyo na kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi wake, Dk Sist Cariah linasema upigaji wa Kura ya Maoni uko pale pale kama ulivyopangwa.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment