TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
SERIKALI HAIJAWATELEKEZA WATANZANIA WANAOSOMA UKRAINE
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inapenda kukanusha vikali
taarifa iliyotangazwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC),
tarehe 30 Julai, 2014, iliyodaikuwa Serikali ya Tanzania imetelekeza
wananchi wake wanaosoma Ukraine Mashariki, ambako kunarindima vita ya
wenyewe kwa wenyewe.
Taarifa hiyo ya upande
mmoja, iliyomnukuu mtu anayeitwa Shamila, aliyedai ni mmoja wa wanafunzi
Watanzania nchini Ukraine, ilisema eti wananchi hao wameachwa bila
msaada wowote.
Wizara imesikitishwa na taarifa
hiyo iliyotolewa bila kufanyiwa uchunguzi wa kutosha. Ukweli ni kwamba
Ubalozi wa Tanzania nchini Urusi, ambao unatuwakilisha pia Ukraine,
umechukua hatua za haraka tangu mwezi Juni, 2014, kuhakikisha wanafunzi
Watanzania wote wanaondoka katika jimbo la Lugansk lililoko vitani.
Ubalozi
ulishirikiana na Rais wa wanafunzi wa Tanzania katika mji wa Lugansk,
Bwana Ahmad Juma, kufanikisha kuondoka kwa Watanzania wote 32
waliokuwepo huko kurudi nyumbani au kuhamia mji wa Kharkov, ambao ni
salama zaidi.
Serikali kupitia Ubalozi wake
Moscow iliwaombea wanafunzi hao malazi kwenye Chuo cha Kharkov Technical
University ambacho kilikubali kutoa hosteli kwa wanafunzi hao. Hata
hivyo, wengi wa wanafunzi hao waliondokea Lugansk kurudi nyumbani
isipokuwa wanafunzi saba ambao walihamia Kharkov. Mpaka tarehe 31 Julai,
2014, ni wanafunzi watatu tu waliokuwa wamebaki mjini Kharkov.
Wanafunzi 20 wamedhaminiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia
Bodi ya Mikopo.
Orodha ya wanafunzi iliyopo
Ubalozini haijumuishi jina la Shamila anayedaiwa kuhojiwa na BBC.
Inasemeka na mtu huyo alikwishamaliza masomo yake ya shahada ya kwanza
na ya pili lakini akaamua kubakia Ukraine akifanya udalali wa kuleta
wanafunzi kutoka Tanzania kwa kushirikiana na vijana wa Nigeria.
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inapenda kuuhakikishia Umma
kuwa inasimamia kikamilifu usalama na ustawi wa Watanzania walioko
Ukraine na popote ulimwenguni, na inasikitishwa na taarifa ya uzushi,
upotoshaji na uzandiki iliyomnukuu mtu anayeitwa Shamila.
IMETOLEWA NA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA DAR ES SALAAM
02 AGOSTI, 2014

No comments:
Post a Comment