Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday 24 October 2015

LOWASSA AJIMALIZA MWENYEWE, ASHINDWA KUJIBU MASWALI YA BBC


Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa.
Na Hamida Hassan
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa, (pichani) ameshindwa kujibu maswali aliyoulizwa na Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Zuhura Yunus, kuhusu ahadi yake ya elimu bure hadi chuo kikuu pamoja na namna atakavyopambana na ufisadi.

Katika mahojiano hayo yaliyorushwa hewani Oktoba 21, 2015, Lowassa amesema suala la ufisadi linahitaji mjadala wa peke yake na kuomba kutafakari kidogo kuhusu ufisadi wa ngazi za juu.
Hata hivyo, Lowassa amesema endapo atashindwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atarudi kijijini kwake Ngarash, Monduli  kuchunga ng’ombe.
Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Zuhura Yunus, Aliyekuwa akimfanyia mahojiano Lowassa.
“Nitakuja kuchunga ng’ombe. Nina ng’ombe, nitakaa na ng’ombe wangu kijijini na kuendelea na maisha,” alisema.
Aidha, Lowassa ameshindwa kufafanua ni kwa nini akiwa ndani ya CCM na serikali ameshindwa kuleta mabadiliko anayoyasema, hususan katika suala la kutoa elimu bure, huku akiishia kusema anategemea fedha za gesi na kwamba wanaweza kukopa kwenye Gas Reserve.
Mahojiano kamili baina yake na mwandishi huyo wa BBC yalikuwa kama ifuatavyo:
Zuhura Yunus alimhoji Lowassa akiwa nyumbani kwake Monduli, Arusha na kwanza akataka maelezo zaidi kuhusu kipaumbele chake cha elimu.
Edward Lowassa: Watanzania wengi sana hawapati elimu, hawapati elimu inayopasa, elimu bora. Unajua dunia ya sasa imebadilika. Dunia ni teknolojia. Ajira za dunia huzipati kama huna elimu inayopasa. Na sisi elimu tunayotoa kwa kweli hatuwezi ku-compete katika dunia ya leo.
Zuhura Yunus: Lakini Mheshimiwa suala ni hilo la bure. Kwa sababu tayari tunajua walimu wamekuwa wakilalamika sana, mishahara yenyewe ni midogo. Hizo fedha zitatoka wapi, za mpaka watu waende bure?
Lowassa: Mbona wanazoendeshea mashangingi zinatoka wapi? Kuna mashangingi makubwa sana ya (shilingi) milioni 230 mtu mmoja. Utakosa hela za kugawa kwa ajili ya wanafunzi? Au kwa mfano, pesa za gesi, tuna gesi nyingi tu kutoka Kusini sasa hivi.
Zuhura: Kwa hiyo nahisi tukitegemea gesi kwa sasa haitakuwa sawa. Kuna namna nyingine?
Lowassa: Kwanza kwamba gesi haitokuwa sawa si kweli. Ghana walikuwa na mgogoro kama hivi hivi, lakini wakaruhusiwa kukopa Gas Reserves. Unakopa Gas Reserve kwamba itakapofika mwaka fulani nita... nitawalipeni kodi yenu. Ingawa wanasema mpaka 2020, tunaweza kuanza kutumia kwa kukopa... kuwekeza katika miundombinu na rasilimali zinazostahili.
Zuhura: Kitu gani kimefanya mpaka sasa hivi isiwezekane (elimu) kuwa bure? Maana’ke unasema inawezekana lakini kwa nini mpaka sasa?
Lowassa: Waulize walionitangulia.
Zuhura: Mheshimiwa, wewe umekuwa ukilizungumzia suala hilo la waliokutangulia, umekuwa katika chama cha CCM kwa takribani miaka 35, kwa hiyo ulikuwa katika serikali hiyo, bila shaka ulikuwa na uwezo wa kutekeleza hayo ya elimu bure, lakini...
Lowassa: Ukitaka kutekeleza ni yule mwenye mamlaka. Ama ni waziri, ama ni waziri mkuu ama ni rais. Lakini vilevile, nilipokuwa waziri mkuu nimesimamia elimu. Tulijenga shule za sekondari kwenye kila kata ya nchi hii.
Zuhura: Hilo ni jambo jema wote kupata elimu lakini si ya bure. Na ambapo ulikuwa katika nafasi ya uwaziri mkuu ambayo ulikuwa na uwezo wa kupendekeza hilo la elimu bure…
Lowassa: Mimi sioni kwa nini unaugua habari ya (elimu ya) bure! Inawezekana. Hivi huko Ulaya wanatoza shule kodi?
Zuhura: Sikatai mheshimiwa kwamba inawezekana, lakini nani atatekeleza? Kwa sababu kila mtu anaahidi, kila mtu anasema, lakini watekelezaji?
Lowassa: Watanzania wanipe mandate tarehe 25 Oktoba utaona nitakavyoitekeleza.
Zuhura: Lakini ulikuwa na nafasi hiyo zaidi. Umechukua nafasi nyingi za uwaziri mheshimiwa, mpaka waziri mkuu si jambo dogo hilo.
Lowassa: Nisikilize basi. Ndiyo maana naomba nafasi hiyo sasa. Tarehe 25 Oktoba wakinipa mandate hiyo utaona utekelezaji wake. Na mimi nakuahidi, wallah itakuwa maajabu!
Zuhura: Kwa hiyo unatakiwa uwe rais ndiyo uweze kutekeleza hayo siyo? Huwezi kuwa waziri tu, waziri mkuu, mbunge..
Lowassa: Kuna mambo ambayo waziri huna mamlaka nayo.
Zuhura: Kwa hiyo uliwahi kushauri suala hilo likakataliwa?
Lowassa: Nina hiyari ya kukataa na kukubali, kusema kwamba nilishauri au sijashauri siwezi kusema!
Zuhura: Ufisadi: Una mkakati gani wa kupambana nao? Mana’ke ufisadi huo uko katika ngazi ya juu mpaka ya chini.
Lowassa: Hilo ni swali gumu, refu na lingetaka mjadala wake peke yake. Mimi nimetafakari, kwa kuanzia tu, tuanze na One stop center. Ambako huko huduma za serikali zinapatikana. Kwa hiyo nikija, dirisha hili linapata hiki, dirisha hili linapata kile, nikiondoka nimemaliza kazi. Tupunguze kidogo urasimu.
Zuhura: Na katika ngazi ya juu? Hizo ni katika ngazi za chini lakini kuna viongozi.
Lowassa: Ngazi ya juu ningetaka kulitafakari kidogo. Wametoa taarifa juzi ya PPA ya hali ya ufisadi ulivyo nchini na kuorodhesha wizara zile ambazo zinaongoza.
Zuhura: Unajinadi mabadiliko. Ni mabadiliko gani hasa?
Lowassa: Baada ya miaka 50 ya kujitawala, tunataka mabadiliko katika nchi yetu.
Zuhura: Mabadiliko hayo unahisi kwa upande wa Ukawa ndiyo yanaweza yakafanyika?
Lowassa: Siyo nahisi tu, naamini hivyo.
Zuhura: Kuna tofauti gani ambayo unahisi kule ulishindwa kufanya, utaweza kufanya wakati ukiwa Ukawa?
Lowassa: Miaka ya nyuma kabisa Mwalimu (Nyerere) alisema, akitambua kwamba ndani ya CCM huwezi kupata mabadiliko, nje ya CCM ndiyo unaweza kubadilika kwa sababu ni mfumo. Nahitaji kubadilisha mfumo mzima.
Zuhura: Lakini Mheshimiwa ukisema sera za CCM.. Una kama miezi kadhaa tu ulikuwa humo humo. Na bila shaka kama usingekatwa ungebaki na mfumo na sera hizo hizo za CCM, si ndiyo?
Lowassa: Unanionea! Mimi nimekuwa mbunge wa kawaida toka miaka nane iliyopita, sikuwa na madaraka yoyote katika nchi, nilikuwa mjumbe wa vikao lakini sikuwa na madaraka katika nchi.
Zuhura: Baadhi ya wapinzani wanasema kutokana na nafasi hii kubwa ya urais, wamekuwa wakizungumzia afya yako. Wewe unawaambiaje?
Lowassa: Afya yangu nzuri kabisa!
Zuhura: Kwa mfano, ikatokea hukufanikiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nini mipango yako?



Lowassa: Nitakuja kuchunga ng’ombe. Nina ng’ombe, nitakaa na ng’ombe wangu kijijini na kuendelea na maisha.

CREDIT: GPL

No comments:

Post a Comment