Steven Wassira - Nje
Abbas Mtemvu - Nje
Zitto Kabwe - Ndani
Bonna Kaluwa - Ndani
Na Daniel Mbega
UCHAGUZI
mkuu umekwishapita, matokeo yametangazwa na tunashuhudia vilio na vicheko
kutoka sehemu mbalimbali nchini – iwe kwenye udiwani, ubunge na hata urais.
Ingawa
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda viti vingi vya udiwani na ubunge, lakini
binafsi nasema kimeshindwa vibaya kwa sababu safari hii tumeshuhudia ikipoteza
halmashauri takriban 19 huku wapinzani wakizoa viti vingi vya ubunge kuliko
ilivyowahi kutokea tangu kuanza kwa uchaguzi mkuu wa vyama vingi mwaka 1995.
Hili
ni funzo kubwa kwa CCM, ambayo kama ilikuwa inadhani inaendelea kutawala kwa
mfumo ule wa kizamani, inaweza ikapotea kabisa mwaka 2020 ikiwa haitafanya
jitihada za makusudi kujikosoa, kujisahihisha na kutekeleza ahadi zake kwa
vitendo.
Kinyume
chake, chama hiki ambacho ni kikongwe kabisa barani Afrika, kinaweza kujikuta
kikisukumwa pembeni kwa sababu Watanzania wameamka kidemokrasia na zaidi
wanataka serikali inayowatumikia.
Najaribu
kuangalia tu katika orodha ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
waliotangazwa baada ya uchaguzi wa Oktoba 25, 2015.
Vilio na vicheko
Ingawa
CCM inachekelea kuyakomboa majimbo kadhaa yaliyokuwa yanashikiliwa na upinzani,
hususan ya jijini Mwanza (Ilemela na Nyamagana), Kigoma Kusini, Kasulu na Lindi
Mjini, lakini inalia kwa sababu imepoteza majimbo muhimu kabisa hasa ya mkoani
Dar es Salaam.
Chama
hicho kimepoteza jimbo jipya la Kibamba, lakini pia majimbo ya zamani ya
Ukonga, Temeke na Kionondoni, huku ikishindwa kulikomboa Jimbo la Kawe ambalo
limeendelea kushikiliwa na Halima Mdee wa Chadema wakati Jimbo la Ubungo
limetua tena Chadema, safari hii chini ya mwanahabari-mwanaharakati Saed
Kubenea.
Majimbo
ya Kinondoni na Temeke yamenyakuliwa na CUF wakati majimbo ya Ukonga, Ubungo,
Kawe na Kibamba yamechukuliwa na Chadema, huku CCM yenyewe ikichukua majimbo ya
Kigamboni, Ilala, Mbagala na Segerea pekee.
Zaidi
ya hayo, CCM imepoteza Jimbo la Same Mashariki, Moshi Vijijini, Siha, Babati
Mjini, Arumeru Magharibi, Longido, Monduli, Iringa Mjini, Muleba Kaskazini,
Buyungu, Kigoma Mjini, Bukoba Mjini na mengineyo.
Kwa
ujumla, mpaka tunakwenda mitamboni, CCM ilikuwa imepoteza majimbo 42 Tanzania
Bara, wakati ambapo mwaka 2010 ilipoteza majimbo 27 tu.
Wanaolia mmoja mmoja kwa CCM ni Namelock Edward Sokoine, Abasi Zuberi Mtemvu, Iddi Azzan, Mwakalebela
Fredrick Wilfred, Balozi Khamis Sued Kagasheki, Christopher Chiza, Aggrey
Mwanri, Anne Kilango Malecela, Dk. Cyril Chami, Said Mtanda, Murtaza Ally
Mangungu, Steven Wasira, Dk. Steven Kebwe, Kisyeri Chambiri, Christopher
Olonyhokie Ole Sendeka, Weston Godfrey Zambi.
Lakini
kwa upande mwingine, wapinzani wanachekelea huku wakijifuta machozi, kwa sababu
licha ya kuongeza majimbo, imejikuta ikipoteza majimbo mengine muhimu kabisa.
CUF
imeongeza majimbo manne mwaka huu na kufikisha matano, lakini jambo baya ni
kwamba, imepoteza Jimbo la Lindi Mjini ambalo limerejea CCM, huku ikishangilia
kupata majimbo matatu katika mikoa muhimu ya Tanga na Dar es Salaam. Chama
hicho kimeshinda ubunge Tanga Mjini, Kinondoni na Temeke, huku pia kikipata
viti vipya Mtwara Mjini, Tandahimba, Kilwa Kaskazini, na Mchinga.
Chadema
wamenufaika zaidi na ujio wa Edward Lowassa kwani wamepata viti 35
ukilinganisha na viti 22 vya mwaka 2010. Hii maana yake ni kwamba, bado
kitaendelea kuwa chama kikuu cha upinzani bungeni, kwani kikipata na wabunge wa
kuteuliwa kinaweza kufikisha wabunge 55.
Ikiwa
Ukawa wataendelea na mshikamano wao huo wa sasa, basi wanaweza kutengeneza
ngome imara bungeni kwa sababu watakuwa na wabunge pengine 100 hivi kutokana na
ukweli kwamba, mpaka sasa wana wabunge 62 wa majimbo (Chadema 35, CUF 26 na
NCCR 1).
Sura ngeni tupu
Bunge
la 11 linatarajiwa kutumia muda kwa wajumbe wake kuzoeana, kwani takwimu
zinaonyesha kwamba, walio wengi ni wageni kabisa japokuwa wapo baadhi ambao
wamerejea.
Kwa
kuangalia takwimu, inaonysha kwamba 95 ya wabunge wa mwaka huu ni wapya kabisa,
ambao watahitaji muda kidogo wa kujifunza Kanuni za Bunge wakati wenzao wengine
tayari wamekwishazielewa na watakuwa wakijikumbusha tu.
Uwiano
Bunge
la safari hii halina ule uwiano wa jinsi katika nafasi za uchaguzi, kwani
takwimu zinaonyesha kwamba, kuna wabunge 19 tu wanawake walioshinda kwenye
majimbo, ambapo kati yao 13 ni wa CCM na waliobaki wa Chadema.
Kama
Katiba Mpya hasa Rasimu ya Pili ingepitishwa, maana yake Bunge la 11 lingekuwa
na wanawake wachache zaidi, lakini sasa kwa kutumia Katiba ya Mwaka 1977, bado
wataongezeka wabunge 72 ambapo kati yao 62 ni wa Viti Maalum na 10 wa ‘Kapu la
Rais’.
Matokeo ya ajabu
Katika
uchaguzi wa mwaka huu, kumekuwepo na matokeo ya ajabu kwenye ubunge, hasa baada
ya kushuhudia wanasiasa kama Wasira, Dk. Didas Masaburi, Mwanri, Dk. Chami,
Abbass Mtemvu, Christopher Chiza na Hezekiah Wenje waking’olewa katika nafasi
zao.
Lakini
pia ni uchaguzi ulioshuhudia wanasiasa wapya wakiibuka kutoka kusikojulikana na
kufanya vizuri zaidi.
Wengi
kati yao ni kutoka upinzani, baadhi yao ni pamoja na Gibson Ole Mesiyeki (Arumeru
Magharibi), Wille Qambalo (Karatu), Saed Kubenea (Ubungo), Bonna Mosse Kaluwa
(Segerea), Abdallah Mtolea (Temeke), Maulid Mtulia (Kinondoni), Antony Mavunde
(Dodoma Mjini), Sanda Edwin (Kondoa Mjini), Cosato Chumi (Mafinga Mjini), Bilago
Samson (Buyungu), Dk. Godwin Mollel (Siha), Nangejwa Kaboyoka (Same Mashariki),
Hassan Bobali (Mchinga) na Emmanuel Papiani (Kiteto).
Hii
inaonyesha kwamba demokrasia imekua na Watanzania wanazidi kukomaa kisiasa hasa
katika kipindi hiki ambacho serikali ya awamu ya nne imejitahidi kuweka uwazi
katika masuala mengi ikiwemo utawala bora.
Kwa
mantiki hiyo, ni dhahiri siasa zikifanywa kwa uadilifu, uwazi na uaminifu
wananchi wanaweza kushuhudia maendeleo katika huduma mbalimbali za kijamii.
CREDIT: UWAZI MIZENGWE
No comments:
Post a Comment