Dk. John Magufuli (CCM) .
Na Daniel Mbega
ILIKUWA miezi, wiki na sasa zimesalia siku tu kabla Watanzania hawajaamua kumchagua rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Oktoba 25, 2015.
Jumla ya wagombea nane wa vyama mbalimbali wanawania nafasi hiyo adhimu ya kupokea kijiti kutoka kwa Jakaya Kikwete wa CCM.
Wananchi wakimshangilia Magufuli hayupo pichani.
Wagombea hao ni Fahmi Dovutwa (UPDP), Maxmillian Lyimo (TLP), Hashimu Rugwe (Chaumma), Chief Lutasola Yemba (ADC), Anna Maghwira (ACT-Tanzania), Janken Kasambala (NRA), Dk. John Magufuli (CCM) na Edward Lowassa wa Chadema anayegombea kwa mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Ushindani mkali uko kwa wagombea wawili – Lowassa na Magufuli, ambao wamezua gumzo kubwa miongoni mwa Watanzania, huku wakichuana kuwania kura 23,533,050 za Tanzania Bara na 720,491 za Zanzibar.
Hata hivyo, licha ya mchuano huo, kuna sababu nyingi za kumfanya Magufuli achaguliwe mwaka huu, lakini tano ni hizi:
Hana makundi
Ukiangalia mwenendo mzima wa mchakato wa kumsaka mteule wa CCM katika kuwania urais, utagundua kwamba karibu watia nia wengi kati ya 42 waliojitokeza awali, na hata 38 waliorejesha fomu, walikuwa na makundi yao.
Wengi walikwenda kuchukua fomu kwa mbwembwe na wakarejesha kwa madoido huku baadhi yao wakitumia runinga kutangaza nia yao na nini ambacho watakifanya ikiwa watateuliwa na hata kushika Ikulu.
Lakini Magufuli alipojitokeza Mei 29, 2015 hakuna aliyetegemea na kwa hakika aliitetemesha CCM na kuyumbisha ngome za wagombea wengi. Hii ni kwa sababu hana makundi katika chama hicho au hata nje ya chama.
Alikwenda kimya kimya akachukua fomu. Wanahabari walipomuuliza kwa nini hataki kuzungumzia atakachokifanya kama wenzake walivyokuwa wanafanya, yeye alisema atainadi Ilani ya CCM kwa sababu ndiyo yenye mwongozo wote. Wakati wa kurudisha pia hakuwa na mbwembwe.
Ingawa alinufaika na vita ya makundi ndani ya chama hicho ndiyo maana akashinda kwa kura 2,104 kati ya kura 2,416 zilizopigwa, lakini bado ukweli uko wazi kwamba, hata waliomchagua waliamini huyo ni “Simba wa Kazi”, kama rais mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi alivyomwita.
Kutokana na kutambua ubaya wa makundi ndani ya chama, ambayo yameiathiri hata serikali katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, na kwa kuzingatia kwamba yeye si mtu wa makundi, ni wazi kwamba atakaposhinda urais na kukabidhiwa pia uenyekiti wa chama, hatakubali kuona kuna makundi.
Kwa mantiki hiyo, kuna kila dalili kwamba heshima na misingi ya CCM iliyorithiwa kutoka Tanu inaweza kurudi huku miiko ya viongozi na utawala bora vikizingatiwa.
Mchapakazi
Hata wapinzani wanaamini kwamba Dk. Magufuli ni mchapakakazi, si kwa maneno, bali kwa vitendo.
Mwenyewe amesikika mara kadhaa kwenye mikutano yake ya kampeni akisema si mwanasiasa na hapendi ‘siasa siasa’ na anachoangalia zaidi ni utendaji, hivyo kila mtu anategemea kuwa serikali yake itakuwa ya watendaji wasiochoka kuwajibika kwa wananchi.
“Kwenye serikali yangu sitaki kusikia mwananchi anakwenda kwenye ofisi ya umma halafu anaambiwa ‘njoo kesho…’. Hakuna haja ya kuwazungusha wananchi katika mambo yanayotekelezeka na kama kuna mtumishi yeyote mwenye tabia hiyo aanze kubadilika sasa,” amekuwa akisikika akisema.
Katika wizara zote alizopitia, Magufuli amekuwa akichapa kazi pengine kuliko mawaziri wote waliobahatika kufanya kazi katika Serikali ya Benjamin Mkapa na hata hii ya Jakaya Kikwete.
Katika kipindi ambacho wananchi wanakabiliwa na kero nyingi pamoja na malalamiko ya uzembe wa baadhi ya watendaji, Magufuli ndiye hasa anayefaa ‘kuwanyorosha’ na kusimamia misingi ya utawala bora na uwajibikaji.
Ana msimamo usioyumba
Jambo jingine linaloweza kumvusha Magufuli katika uchaguzi wa Oktoba ni msimamo. Huyu jamaa ana misimamo isiyotia mashaka na hajui kumung’unya maneno. Daima anajua anachokisimamia. Hii ni tabia ambayo alikuwa nayo Mwalimu Julius Nyerere, kwamba akishaamua jambo fulani na kama anajua njia yake, kamwe huwezi kumyumbisha.
Wakati akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alithubutu hata kumtaja Naibu wake kwamba anahodhi viwanja.
Mwaka 2013, aliwashangaza watu wakati alipopishana hadharani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kuhusu suala la magari ya mizigo kupita katika barabara yakiwa yamezidisha uzito. Licha ya malori kugoma na kusababisha kero kubwa, lakini kamwe hakuweza kubadili msimamo wake.
Uwezo wa kuchambua nyaraka
Elimu siyo kila kitu katika uongozi, lakini kiongozi mwenye elimu pamoja na sifa nyingine anafaa zaidi kuliko asiye na elimu. Magufuli ni Profesa wa Kemia – amesomea wala hakupewa kama ‘asante’ – hivyo ni msomi mwenye uwezo pia wa kuongoza.
Lakini uwezo wake wa kusoma na kuchambua nyaraka nao unampa sifa nyingine kubwa kwamba Watanzania wategemee mtendaji anayefuatilia na hata kama kuna nyaraka zitatua mezani kwake, basi waamini kwamba atazipitia na kuzitolea uamuzi bila shida.
Magufuli anajiuza mwenyewe
Wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea urais kupitia CCM mwaka 1995, Mwalimu Nyerere aliwashangaza wengi wakati alipoingilia kati na ‘kupangua mipango michafu ya wabaya wa chama waliokwenda na mgombea wao’ huku akiwatuhumu kwamba walikuwa wanatumia fedha za bhangi kuhakikisha ‘mtu wao’ anaingia Ikulu.
Hatimaye akateuliwa Benjamin Mkapa, ambaye alikuwa ‘hafahamiki’, lakini Mwalimu Nyerere akasema angemnadi mgombea huyo wa CCM kwa vile “anauzika”.
Mwaka 2005 CCM haikutumia nguvu kubwa kumnadi Jakaya Kikwete ambaye alikuwa kipenzi cha watu, japokuwa ndani ya chama kakikundi kadogo kalikojiita ‘Wanamtandao’ kalikuwa kameibuka na kuweka matabaka ambayo baadaye ndiyo yalisababisha kuvurugika kwa maadili ndani ya chama na serikali.
Lakini safari hii, licha ya kuwepo upinzani mkubwa kutoka kwa mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, bado kuna matumaini makubwa kwa CCM kukamata Dola kwa vile Dk. Magufuli anafahamika na anajiuza mwenyewe!
Wanaoibeza CCM kwamba ‘imefilisika ndiyo maana Magufuli mwenyewe anajinadi’ wanakosea, kwa sababu hata mchuuzi wa samaki, pamoja na kubeba kapu kubwa, wakati mwingine anapofika kwa wateja huwa anawatoa samaki wake kuwaonyesha wateja!
Kwa hiyo basi, hakuna ubaya wowote kwao kutumia jina la Magufuli, kwani ni sawa na kusema “Nauza migebuka” bila kutaja kwamba wako kwenye tenga ama kikapu!
Ukweli huu hata wapinzani wenyewe wanaujua.
0656-331974
CREDIT: UWAZI MIZENGWE
No comments:
Post a Comment