Wanahabari wakichukua tukio hilo.
Georgia Mtikila akisoma taarifa yake pembeni yake ni baadhi ya viongozi wa chama cha DP aliokuwa ameambatana nao.
MKE wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, Georgia Mtikila amejitokeza mbele ya wanahabari jijini Dar es Salaam, mapema leo na kumuomba Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kuunda tume ili ichunguze kifo cha mumewe kwa kuwa kina utata mkubwa ndani yake.
Hayo ameyasema leo katika Idara ya Habari (maelezo) alipokuwa akizungumza na wanahabari na kusema kuwa marehemu alikuwa na maadui wengi kwa miaka yote ya harakati zake za kisiasa na kusema kuwa baada ya kifo hicho alishangaa kutoonekana kwa mlinzi wake (bodyguard) wa Mtikila aliyemtaja kwa jina la Patrick na kudai kuwa hajui amuweke fungu gani kwa kuwa hata kwenye msiba hakufika japokuwa yupo hapa (Dar).
Vilevile amedai kuwa mumewe aliuawa na maadui waliopinga kauli zake za kulitetea taifa na pia amekanusha ripoti ya polisi ya kifo cha Mtikila kwa madai kuwa hana imani na ripoti ya uchunguzi iliyotolewa na polisi kwa kuwa nao wanaweza kutumiwa na watu wabaya.
“Ninaomba mheshimiwa rais aingilie kati kifo cha marehemu mume wangu kwa kuunda tume isiyohusisha polisi kwa kuwa sina imani nao,” alisema Bi. Georgia huku akiitaka mamlaka ya mawasiliano, TCRA isaidie kujua nani aliyeweka picha, mapema alfajiri kwa kile alichodai kuwa mtu huyo alifanya hivyo kuwaonesha mabosi zake jinsi alivyoikamilisha kazi ya kumuua Mchungaji Mtikila.
CREDIT: GPL/DENIS MTIMA
No comments:
Post a Comment