Ikulu ya Tanzania
Na Mkimbu Lukule
Tangu kuanza harakati za uchaguzi
Tanzania kumekuwa na tambo nyingi za kuwanadi wagombea. Kila kundi likitaka mgombea wao ang’ae
dhidi ya mwenzake. Zimekuwepo
mbinu na hadaa nyingi katika kufanikisha malengo haya ya kisiasa.
Wapo ambao wamekuwa wakifanya
kampeni zao kwa kutoa ahadi lukuki ambazo zinalenga katika kuwaaminisha
wananchi kuwa wakichaguliwa wataibadilisha nchi kwa haraka na kuifanya ifike
katika kilele cha maendeleo.
Kampeni hizi zimeshuhudia pia
kupakana matope, kusifiana na kupondana baina ya wapambe wa wagombea
Urais. Ni wazi kuwa kila
upande unajaribu kuonyesha kuwa wapinzani wao hawajui, hawafai na
hawawezi. Kwamba ili
maendeleo yapatikane ni lazima mgombea wanayemnadi achaguliwe kuwa Rais.
Mitaani nako kumeibuka hali ya
sintofahamu na ushabiki. Zimekuwepo
kauli kuwa huu ni wakati wa ‘mabadiliko’. Kwamba iwe isiwe ni zamu yetu
kuingia ikulu. Kwamba hata
likiwekwa jiwe au mbuzi na chama fulani, sisi tutalichagua jiwe au tutampigia
kura mbuzi.
Ushabiki wa aina hii umeibua
maswali kwa wadau mbalimbali wa demokrasia. Tumeona wachambuzi wa kisiasa
wakijitokeza kwenye vyombo vya habari na kujadili kuhusu hali hiyo. Miongoni mwa wachambuzi hao yupo
Johnson Mbwambo wa gazeti la Raia Mwema.
Mwambo amekuwa akiandika uchambuzi
wa mara kwa mara kuhoji uhalali wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)
kumchagua Edward Lowassa, mtu
ambaye wapinzani wao yaani Chama Cha Mapinduzi, walimuengua kwa kigezo cha
kukosa maadili na kuwa na kashfa nyingi za ufisadi.
Ukiachilia mbali Mwambo, Mchungaji
Christopher Mtikila wa Chama cha Demokrasia (DP), mchambuzi wa kwenye mtandao
wa Jamii Forums, Mwanakijiji, aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, Dkt. Wilbroad Slaa na
aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba nao
wametoa kauli ambazo zimekinzana na uamuzi wa UKAWA kumsimamisha Lowassa.
Miongoni mwa sababu ambazo wadau
hao wamezitoa ni kuwa, kabla ya Lowassa kujiunga UKAWA, ajenda kubwa ya vyama
vya upinzani ilikuwa ni ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma, lakini
kujiunga kwa Lowassa kunasababisha wabadilishe ajenda.
Katika mazingira haya, viongozi
hawa waliojitoa wameeleza kuwa hapo awali wakati wanaitengeneza UKAWA
waliijenga kwa kanuni na misingi lakini lilipokuja suala la kumkaribisha
Lowassa walijikuta wakivunja misingi waliyojiwekea.
Mosi, Lipumba anasema kuwa Lowassa
alikuwemo katika Bunge Maalum la Katiba lililobariki muungano wa Serikali mbili
ambao UKAWA waliupinga na alikaa hadi mwisho wa bunge hilo. Pili, Dkt. Slaa alisema kuwa CHADEMA
walimtaja Lowassa katika orodha ya mafisadi wakubwa waliofilisi nchi na
ameendelea kumshtumu Lowassa, kwa nyakati tofauti, kuwa amejihusisha na vitendo
vya ufisadi mahala mbalimbali kwa nyakati tofauti.
Wote hawa wanaompinga Lowassa,
wanasema kuwa haikuwa tatizo kwa UKAWA kumpokea Lowassa ila kitendo cha
kumpokea na moja kwa moja kumkaribisha na kumpa nafasi ya kuwa mgombea Urais,
kimeibua udhaifu mkubwa wa wapinzani hao. Kwamba hadi kufikia hatua wapinzani
wao wanafanya mchakato wa kumpata mgombea Urais wao walikuwa bado hawajaweza
kuwa na mtu ambaye alikuwa na vigezo stahiki vya kusimama katika nafasi hiyo
kubwa ya Urais.
Jambo la kushangaza UKAWA inaundwa
na vyama vya kisiasa vyenye nguvu ambavyo baadhi ya wagombea wake kwa nyakati
tofauti wamesimama dhidi ya CCM na kusababisha ushindani mkali. Aliweza kufanya hivyo Prof. Lipumba,
aliweza kufanya hivyo Dkt. Slaa na walipata kura nyingi.
Kutokana na sintofahamu hii ndipo
inapoibuliwa hoja ya kuwa Je, kuna baadhi ya wanasiasa wanaounda UKAWA
walipokea fedha ili kufanikisha Lowassa awe mgombea Urais? Ama ni ushawishi
gani wa kisera na kimkakati, mgombea huyo aliingia nao Ukawa na kusababisha
apewe dhamana hiyo?
Kwa upande wa wana mabadiliko
wanatetea ujio huo wa Lowassa kwenda UKAWA wakisema kuwa kutokana na mzingira
yaliyopo, ujio wa Lowassa ukawa na kuteuliwa kwake katika nafasi ya kugombea
Urais ni vitu ambavyo visingeweza kuepukika.
Hoja yao ni kuwa CCM imekuwepo
madarakani miaka mingi na imefanya mabaya mengi na kwamba imefika wakati kuwa
wapumzishwe kwa njia yoyote ile. Katika
hili wapo wengi miongoni mwao yupo Freeman Mbowe-Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa,
Peter Msigwa- mbunge wa Chadema Iringa mjini, Tundu Lissu-mbunge wa CHADEMA
Singida, Jenerali Ulimwengu – mchambuzi wa gazeti la Raia Mwema na wengineo.
Watoa hoja hii ya mabadiliko
wanaeleza kuwa kwa hali ya nchi ilivyo sasa wanaamini kuwa ni wakati pekee wa
kuing’oa CCM kwasababu imegawanyika. Ni
wazi maelezo yao yanarejea kujiengua kwa waliowahi kuwa mawaziri wakuu wawili
Tanzania kupitia CCM, Lowassa na Frederick Sumaye ambao wamejiunga Ukawa.
Ukiyapitia maelezo ya
‘wanamabadiliko’ ni kama vile wanasema kuwa kabla ya kuja kwa Lowassa UKAWA na
vyama vilivyoungana havikuwa na uwezo wa kusimamisha mgombea mwenye nguvu ya
kushinda katika ngazi ya Urais.
‘Wanamabadiliko’ wameamua kuachana
na ajenda ya ufisadi na badala yake wameeneza falsafa mpya kuwa nchi imechoshwa
na utawala wa chama kimoja kwa maana hiyo inahitaji mbadala wa fikra. Hata hivyo, wanashindwa kujibu swali
la Je, kuwachukua wagombea walioshindwa kura za maoni kwenye vyama vyao ndiyo
kuleta fikra mpya?
Kutokana na hali hiyo nchi
imeingia katika sintofahamu kubwa ambapo vijana na wananchi wa kawaida
wamejikuta wakiburuzwa na falsafa na misemo ambayo hawaielewi. Watu wanalishwa neno ‘mabadiliko’
lakini hawaelewi mapana ya dhana ya neno hilo la mabadiliko. Wanaenda kulingana na upepo wa kisiasa
ambao hawaujui hatma yake.
Wakati huu nadhani kwa wanasiasa
ni wakati wa kuvuna walichopanda, kama mtu alipanda bangi atavuna
bangi. Kiongozi tunayemtaka ni yule ambaye uwajibikaji wake na uadilifu
wake utakuwa chachu kwa Watanzania wenyewe kujiletea maendeleo, kwani nchi
haiendelezwi kwa hela za mtu binafsi.
Mwandishi wa makala hii ni msomaji wa blog hii, anapatikana kwa barua pepe mkimbulukule70@gmail.com
No comments:
Post a Comment