Baada ya kuamua kuleta mageuzi ya vyama vingi vya siasa, ilikuwa lazima kubadili baadhi ya vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Rais aIiteua Kamati ya kutazama Katiba yetu na kufanya mapendekezo yanayotakiwa. Kamati hiyo iliongozwa na Ndugu Mark Bomani.
Kati ya mapendekezo yake mengi,
moja lilihusu Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Kamati ilipendekeza kwamba
badala ya utaratibu wa sasa wa kuwa na Makamu wa Rais wawili, Waziri Mkuu wa
Serikali ya Muungano na Rais wa Zanzibar, inafaa tuwe na Makamu mmoja tu. Na
jinsi ya kumpata Kamati ilipendekeza tufuate utaratibu wa Kimarekani ambayo,
mtu aliyeteuliwa na Chama chake kuwa mgombea wa urais, atakuwa na mwenzake
wanamwita “Running Mate” na endapo
mgombea huyo atachaguliwa na wananchi kuwa rais basi huyo mgombea mwenzake ndiye
atakuwa Makamu wa Rais.
Lakini kamati ikapendekeza kwamba
kutokana na historia ya nchi yetu, itafaa Chama kikiteua Mgombea urais kutoka
upande mmoja wa Muungano, basi kiteue Mgombea mwenza kutoka upande wa pili wa
Muungano; na katiba iseme hivyo.
Watu wengi, mimi nikiwa miongoni
mwao, waliona kuwa mapendekezo haya ni mazuri. Lakini tukawa tukisikia
minong’ono kwamba “Wazanzibari” hawapendi pendekezo hili la kupata Makamu wa
Rais kwa njia ya kuwa na Mgombea Mwenza. Wanataka utaratibu wa sasa uendelee,
ambapo Rais wa Zanzibar akisha kuchaguliwa anakuwa moja kwa moja Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano.
Utaratibu huu hata sasa una
matatizo. Rais wa Zanzibar huchaguliwa na Wazanzibari watupu, ili awe Rais wao;
lakini anakuwa pia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano bila kuchaguliwa na
Watanzania wa Bara. Kama Rais wa Jamhuri ya Muungano hayupo kwa sababu yoyote
ile, huyu ataweza kushika nafasi yake, kwa mujibu wa Katiba, lakini bila
kuchaguliwa na wapiga kura wa Tanzania nzima. Ni dhahiri kwamba utaratibu huu
una walakini, na ingawa mpaka sasa haujatuletea matatizo makubwa, ni wazi
kwamba hata bila mfumo wa vyama vingi, siku moja tungelazimika kuubadili.
Lakini ni dhahiri zaidi kwamba
katika hali ya vyama vingi hatuwezi kuendelea na utaratibu wa sasa. Mkiwa na
vyama vingi vya siasa, na Serikali zaidi ya moja, hamna budi mkubali kwamba
inawezekana Chama kinachoongoza Serikali ya Muungano kinaweza kisiwe ndicho
kinachoongoza Serikali ya Zanzibar.
Kwa hiyo tukibaki na utaratibu wa
sasa, ambapo Rais wa Zanzibar anakuwa kwa moja ni Makamu wa Jamhuri ya Muungano
tunaweza kujikuta katika hali ambapo Rais wa Jamhuri anatoka katika chama cha
upinzani! Na endapo Rais hayupo kwa sababu yoyote huyu anaweza akashika nafasi
yake ingawa alikataliwa na wapiga kura katika uchaguzi uliopita!
Mapema mwezi Desemba 1992,
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ilikutana Dodoma kwa ajili ya kuzungumzia suala
hili pamoja na mengine. Viongozi wa chama na Serikali Waliniomba nami niende nikatoe
maoni yangu. Nikaenda.
Mkutano wa faragha: Tulikuwa na
kikao cha faragha cha viongozi wakuu wote wa Chama na Serikali, na wengine wa
nyongeza. Mambo yaliyokuwa yametayarishwa yakazungumzwe katika Halmashauri Kuu
yalikuwa ni hilo la utararibu wa kuchagua Makamu wa Rais na mengine. Lakini
Rais alieleza kuwa walikuwa wamezungumza pia suala la vipindi na muda wa kuwa
Rais wa Jamhuri ya Tanzania. Rais alieleza kuwa walikuwa wamekubaliana kwamba
vipindi vya kuwa Rais ni lazima vitamkwe, lakini walikuwa hawajafikia uamuzi
viwe vingapi - vingapi.
Awali baadhi ya Viongozi wa Chama
- walikuwa wameanza kampeni za kutaka Rais Mwinyi aongezewe vipindi vya muda wa
kuwa Rais. Nilipotambua hivyo nilikuwa nimekwenda mara moja kwa Rais na kumsihi
azizime kampeni hila; na viongozi wahusika nilitafuta nafasi nao nikawaomba
wasilifufue jambo hili. Nikadhani tumeelewana hivyo. Kwa hiyo nilishtuka
niliposikia kuwa kumbe suala hilo la vipindi vya urais- bado linazungumzwa, na
ati bado uamuzi wa vipindi vingapi haujafikiwa! Kwa hiyo nilirudia tena kueleza
umuhimu wa kukubali kwamba suala hili tumekwisha kuliamua, na hatari ya kuanza
kulizungumza upya.
Sababu ya kufanya muda ambao mtu
ye yote anaruhusiwa kuwa Rais utamkwe na uwe ni sehemu ya Katiba ilikuwa ni
kuutoa uamuzi huo mikononi mwa Rais mwenyewe, au kikundi cho chote cha Chama au
Dola. Si uamuzi mwepesi, kwa Rais wala kwa washauri wake.
Plato, Myunani wa kale,
alipendekeza kuwa mafilosofa ndio wanaofaa kuwa watawala wa nchi, maana wana
sifa mbili muhimu: kwanza, Wana uwezo wa kutawala, na pili, hawapendi kutawala.
Kwa hiyo, Jamhuri ya Plato itakuwa na sheria ya kuwalazimisha mafilosofa
kutawala kwa zamu; na mtu zamu yake ya kutawala ikiisha, atafurahi sana kurudia
shughuli zake za falsafa ambazo ndizo hasa anazozipenda.
Lakini nchi zetu hazitawaliwi na
mafilosofa wa Plato; watawala wetu ni wanasiasa wa kawaida ambao wanapenda sana
kutawala hata kama hawana uwezo wa kutawala; na ambao wako tayari hata kuhonga
ili wachaguliwe kuwa watawala, na wakisha kuchaguliwa hawatoki bila
kulazimishwa. Si busara kuwaachia wao wenyewe ndio wawe waamuzi wa lini waache
kuwa watawala.
Lakini hata kwa viongozi
wanaotambua kuwa uongozi ni wajibu, na ukisha kutimiza wajibu wako ni vizuri
kuondoka, si rahisi kuamua kama wajibu wako ni kuondoka au ni kuendelea. Na
sababu za kusita zinaweza zikawa nzuri kabisa. Na katika hali halisi ni vigumu
zaidi kwa washauri wa Rais kumwambia kuwa amekwisha kutimiza wajibu wake na kwa
maoni yao inafaa aondoke amwachie mtu mwingine. Wao wanazo sababu nyingi zaidi,
nzuri na mbaya, za kumtaka aendelee, na watamshauri hivyo. Kwa hiyo ni jambo la
busara kabisa uamuzi wa muda wa kuwa Rais ufanywe mara moja, na ukisha kufanywa
uwe ni sehemu ya Katiba ya Nchi na uheshimiwe.
Na hivyo ndivyo tulivyofanya.
Suala hili lilikwisha kuamuliwa zamani, na sasa ni sehemu ya Katiba yetu uamuzi
huo inafaa uheshimiwe. Rais Mwinyi ndiye Rais wa kwanza kuchaguliwa kwa mujibu
wa Katiba hiyo. Yeye akisema kuwa vipindi viwili havitoshi na akataka view
vitatu; rais wa pili atasema viindi vitatu havitoshi na atataka view vine; na
kadhalika na kadhalika mpaka tufiie Ngwazi wa Tanzania. Hilo si jambo la
kuzungumzwa, na limefanyiwa uamuzi wa mwisho. Kuhusu suala la utaratibu wa
kuchagua Makamu wa Rais, Kamati, Kuu ya CCM ilikuwa imeamua kupendekeza kwa
Halmashauri Kuu ya Taifa kwamba tuendelee na utaratibu wa sasa, kama
"Wazanzibari" wanavyopendelea! Bila maelezo ya kuridhisha. Katika
kutoa maoni yangu nilipendekeza na kusisitiza kuwa tukubali mapendekezo ya
Kamati ya Bomani.
Kikao cha Halmashauri Kuu:
Nilikuwa sikukusudia, wala niiikuwa sikusudiwi na wale walioniita, kuhudhuria
kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa. Nilitumaini kuwa baada ya mazungumzo yetu
ya faragha viongozi wetu watapenda kuutazama upya uamuzi wao wa kukataa rnapendekezo
ya Kamati ya Bomani.
Lakini nilipoambiwa asubuhi ya,
siku ya pili yake kwamba Kamati Kuu itayapeleka rnapendekezo yake katika
Halmashauri Kuu vile vile yalivyokuwa, niliomba nipatiwe nafasi nikatoe maoni
yangu mbele ya Halmashauri Kuu ya Taifa na kueleza kwa nini naamini kuwa
viongozi wetu watafanya makosa wakikataa mapendekezo ya Kamati ya Bomani.
Pamoja na mambo mengine,
nilieleza kuwa sehemu moja ya mapendekezo ya Kamati ya Bomani, ile inayosema
Mgombea akitoka upande mmoja mwenziwe atoke upande mwingine wa Muungano,
inakusudiwa kuisaidia Zanzibar. Maana ukiacha Mwenzi wa Mgombea urais
achaguliwe kutoka upande wo wote wa Muungano, uwezekano wa wote wawili, Rais na
Makamu, kutoka Tanzania Bara ni mkubwa sana. Mapendekezo ya Kamati ya Bomani
yalikuwa yanahakikisha kwamba mmoja wa viongozi wetu wakuu hao akitoka Bara
mwingine atatoka Visiwani. Kwa hiyo ni vigumu sana kuona kwa nini "Wazanzibari"
wanapinga utaratibu huu.
Na ukiuliza sababu unaambiwa kuwa
ni"nyeti"!.Nikaonya: ikiwa "Wazanzibari" wataendelea na
msimamo huu usioeleweka wala kuelezeka, maana ati ni "nyeti",
Watanzania Bara wataanza kununa. Nikasema nimeanza kusikia minong’ono ya
manung’uniko ‘mitaani’. Nilirudia tena kutoa maoni yangu kuhusu vipindi vya
urais.
Baada ya hapo niliondoka nikarudi
Butiama. Baadaye niliambiwa kwamba mjadala uliofuata haukuwa mzuri sana; na
viongozi wetu badala ya kulizungumzia suala la uchaguzi waziwazi kabisa na
kulifanyia uamuzi, waliondoka katika Halmashauri Kuu kwa “janjajanja",
wakalipeleka katika Bunge kuomba wapewe muda wa miaka miwili ya kulitafakari!
Na Bunge likakubali! Wabunge wakapitisha utaratibu wa kuchagua Rais na
kuahirisha utaratibu wa kuchagua Makamu wake mpaka hapo viongozi wetu
watakapopata ndoto nzuri zaidi - baada ya miaka miwili!
Baadaye viongozi wetu walinitumia
wajumbe kuja kunieleza upya msimamo wa Serikali, na kuniomba nielewe. Nakumbuka
vizuri sana mmoja wa wajumbe hao, mtu msema kweli sana, alinikosoa kwa kwenda
katika Halmashauri Kuu ya Taifa na kutaja minong'ono ya "mitaani"!
Nakumbuka pia kwamba nilisisitiza: Waambieni Viongozi wetu: Tatizo si mimi,
tatizo ni "Wazanzibari" na wale wanaounga mkono msimamo wao. Hao ndio
wanaofaa kutumiwa ujumbe; mimi ni mwelezaji tu wa tatizo lililopo ikiwa
tutaendelea na huu msimamo "nyeti" usiokuwa na maelezo.
Wazee hawa waliendelea kuja
kuniona au Msasani au Butiama. Baadaye suala la Zanzibar kuingia katika OIC
likazuka. Hili nalo viongozi wetu wakaliombea bungeni, na wakapewa muda wa
mwaka mmoja wa kulitafakali! Suala la kuvunja Katiba ya Nchi yetu!
REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI
WETU NA HATMA YA TANZANIA
No comments:
Post a Comment