Mwalimu Julius Nyerere akimsikiliza Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine enzi ya uhai wao.
Na Daniel Mbega
KAMA kuna
kitu ambacho Mwalimu Nyerere alikiabudu – mbali ya Mungu kupitia katika imani
yake ya Kikatoliki – ni Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea iliyozaliwa ndani ya
Azimio la Arusha, ambayo aliendelea kuihubiri na kuitetea kwa nguvu zake zote
hadi kikomo cha uhai wake.
Kila
alikokwenda daima alitembea na Biblia pamoja na Azimio la Arusha, akiamini
kwamba misingi ambayo chama cha Tanu kiliiweka kwenye azimio hilo Februari 5,
1967 pale Arusha ilikuwa mizuri na ingeendelea kuwa mizuri ikiwa tu Watanzania
wangemwelewa dhamira yake.
Azimio la
Arusha lililohimiza Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea bado liko katika maandiko,
ikiwemo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ingawa kwa sasa ni nadharia
tu na si vitendo.
Hii
inatokana na azimio hilo ‘kuuawa’ na Azimio la Zanzibar la mwaka 1991, ambalo
lilileta ‘Uliberali Mamboleo’ (Neo-Liberalism)
ambao kimsingi ni ubepari.
Wenyewe
wanauita ‘Soko Huria’ na ndio ulitoa ruksa kwa kila kitu, zikiwemo nguo za
mitumba (maarufu wakati huo kama ‘kafa Ulaya mazishi Bongo’).
Soko huria
hili likatafsiriwa vibaya na watu wengi, wakiwemo watumishi wa umma ambao enzi
zile za Mwalimu na siasa yake ya ujamaa na kujitegemea walijiona wameminywa,
sasa wakaachana hata na misingi ya utawala bora na maadili ya uongozi wa umma,
pamoja na miiko ya viongozi, na kuamua kujilimbikizia mali kadiri walivyotaka
kwa kutumia nyadhifa zao, jambo ambalo Tanu, na baadaye CCM, ililikemea kwa
nguvu zote.
Soko huria
hili, lililotokana na shinikizo la ‘wakubwa’ kama Benki ya Dunia na Shirika la
Fedha Duniani, likabinafsisha mashirika ya umma, likabidhaifisha huduma muhimu
za jamii kama elimu, afya na hata usafiri, na ndio ukawa mwanzo wa upunguzwaji
wa watumishi wa umma (retrenchment).
Kwa miaka
23 chini ya utawala wa Mwalimu Nyerere, Tanzania iliishi chini ya mfumo wa
Ujamaa, siasa ambayo iliweka njia zote kuu za uchumi chini ya umiliki wa umma, ingawa
wengi wanasema hali hiyo ndiyo ilichelewesha maendeleo kwa Tanzania.
Rais
mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi, alikaririwa Julai 2008 akisema kwamba Ujamaa
ulikuwa hautekelezeki.
Ujamaa ni
siasa nzuri lakini unapingana na uasili wa binadamu. Watu, wakati wote
wanapenda kuwa matajiri. Hawataki kuwa maskini kwa maisha yao yote. Msingi
mmoja wa ujamaa ni kwamba kusiwepo na pengo kubwa kati ya matajiri na maskini,
pengo ambalo sasa tunalishuhudia huku wachache wakiwa wamejilimbikizia mali
kinyume cha utaratibu na wakitamani kuendelea kuchota mali za umma na hata
kununua uongozi au madaraka ili waendelee kuifaidi keki ya fursa za kiuchumi
huku walio wengi wakiendelea kuogelea katika ufukara wa kutisha.
Alhaji
Mwinyi alisema, wakati anashika uongozi wa juu katika miaka ya 1980 bidhaa
mbalimbali muhimu zikiwemo sukari, dawa za meno na hata sabuni zilikuwa adimu.
“Tungeweza
kuendelea na sera ile au kufanya mabadiliko? Ujamaa kweli ulikuwa unafanya kazi
1980? Lakini ukiniuliza kama ujamaa ulikuwa mbaya? Nitakwambia, ni siasa nzuri
duniani. Tatizo lake ni kama ndoto,” alikaririwa akisema siku hiyo ya uzinduzi
wa kitabu chenye maoni ya wakuu 13 wa nchi za Afrika akiwemo yeye mwenyewe na
Rais aliyemfuata Benjamin Mkapa ambapo wanaeleza uzoefu wao.
Ndani ya
kitabu hicho, Mwinyi anasema alikuwa mkuu wa nchi ambaye alitaka kufanya mabadiliko
lakini wakati huo makamu mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), chama ambacho
wakati huo mwenyekiti wake alikuwa ndiye muasisi wa Azimio la Arusha, Mwalimu
Nyerere.
Itakumbukwa
kwamba, sera na mipango aliyoianzisha Mwinyi ikafuatiwa kwa kasi kubwa na Rais
Mkapa aliyemfuatia, hali ambayo ilidhihirisha kuuzika kabisa ujamaa.
Ingawa
hili lilikuwa dhahiri, lakini hakuna aliyewahi kuthubutu kutoa kauli kwamba
ujamaa umeshindikana wakati Mwalimu Nyerere akiwa hai, hadi baada ya kifo chake
mwaka 1999 ndipo tunazisikia kauli hizi kwa uwazi zaidi. Wengi enzi hizo
walipenda kusema chini chini, kwa usiri pengine kwa kuhofia kukemewa na
‘Mchonga Meno’.
Lakini
nakumbuka vyema Mwalimu Nyerere aliwahi kukaririwa na jarida la New
Internationalist, toleo namba 309 la Januari-Februari 1999 (wakati huo akiwa
msuluhishi mkuu wa mgogoro wa Burundi) akisema kwamba Ujamaa haukushindwa
duniani, bali haukuwahi kujaribiwa!
Ndiyo!
Alikuwa na kila sababu ya kusema hivyo, kwa sababu hadi wakati huo mataifa
makubwa yaliyoasisi Ujamaa yalikuwa yamegeukia ubepari. Sera za Ujamaa katika
Poland zilikuwa zimeshindikana, Cuba iliendelea kukabiliwa na upinzani mkubwa
na vikwazo vingi kutoka Mataifa ya Magharibi, Urusi (USSR) ilikuwa
imesambaratishwa mwaka 1991 chini ya Rais Mikhail Gorbachev, Ujerumani
Mashariki nayo ilikuwa imeungana na Magharibi mwaka 1990 na ‘kuuvunja Ukuta wa
Berlin’ uliodumu kwa miaka mingi, huku Czechoslovakia ikigawanyika na kuzaliwa
kwa mataifa mawili – Jamhuri ya Czech na Slovakia, kama ilivyokuwa kwa
Yugoslavia ya zamani iliyozaa Yugoslavia na Serbia!
Mwalimu
Nyerere alikuwa na lengo zuri tu (kwa maoni yangu) katika kuanzisha Azimio la
Arusha, kama alivyokaririwa akisema; “Bado naendelea kulibeba (Azimio) kila
niendako. Kila wakati nasoma tena na tena kuona nini ambacho naweza kukibadili.
Labda nitaboresha katika Kiswahili kilichotumiwa lakini Azimio hili bado
linafaa: Siwezi kubadili chochote. Tanzania ilikuwa imepata uhuru muda mfupi tu
lakini tayari tulikuwa tumeshuhudia pengo kubwa kati ya wenye-nacho na wasio-nacho.
Matajiri walikuwa wameibuka kutoka katika kundi la wanasiasa na maofisa ambao
walikuwa maskini wakati ule wa utawala wa wakoloni, lakini sasa walikuwa
wanatumia madaraka yao ndani ya chama na serikali kujinufaisha. Maendeleo ya
aina hii yangewanyang’anya wananchi madaraka (kama ilivyo sasa). Kwa hiyo
tukaanzisha chombo kipya: tukasema maendeleo ni kwa watu wote na si kikundi
kidogo cha watu,” alisema.
“Azimio la
Arusha ndicho kitu kilichoifanya leo Tanzania iwe Tanzania. Tulisema kile
tulichokisimamia, tukaweka miiko ya uongozi kwa viongozi wetu na tukafanya
juhudi kufikia malengo yetu. Hili lilikuwa dhahiri kwa kila mmoja, hata kama
tulifanya makosa – na mtu anapojaribu kitu fulani kipya na kigeni lazima kuwepo
na makosa.
“Azimio la
Arusha na mfumo wetu wa demokrasia ya chama kimoja, pamoja na lugha yetu ya
taifa, Kiswahili, na jeshi la taifa lililonolewa kisiasa na lenye nidhamu,
liliweza kuyaunganisha makabila zaidi ya 126 katika taifa imara.
“Hata
hivyo, pamoja na mafanikio yote haya, bado wanasema tulishindwa katika
Tanzania, kwamba ‘tulichemka’. Lakini ni kweli tulishindwa? Lazima tuseme
hapana. Hatuwezi kukanusha kila jambo tulilofanikiwa. Kuna rafiki zangu ambao
hatukuwaruhusu wawe matajiri; sasa wametajirika na wanasema “Unaona, tunatajirika
sasa, kwa hiyo hukuwa sahihi”. Lakini hilo ni jibu la aina gani? Kusuasua kwa
Ujamaa kumekuwa ni kwa dunia nzima. Hili ndilo linalopaswa kutolewa maelezo,
siyo tu upande wa Tanzania. George Bernard Shaw, ambaye alikuwa anapinga kuwepo
kwa Mungu, alipata kusema: “Huwezi kusema Ukristo umeshindikana kwa sababu
haujajaribiwa”. Hivyo ndivyo ilivyo hata kwa Ujamaa: huwezi kusema Ujamaa
umeshindwa eti kwa sababu haukujaribiwa,” alifafanua.
Lakini leo
hii tunapokumbuka miaka 16 ya kifo chake tunapaswa kujiuliza: Hivi ni kweli
Ujamaa ulishindwa au haukujaribiwa? Inavyoonekana ni kwamba viongozi wetu ndio
wanaotufanya tuamini kwamba Ujamaa kweli ulishindwa, wakati wananchi wa kawaida
wanaelewa tofauti.
Itakumbukwa
kwamba, enzi zile wakati Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ikiimbwa kila kona,
hata wanafunzi walijifunza kujitegemea, kwa kuzingatia Azimio la Musoma
lililopitishwa na Halmashauri Kuu ya Tanu Novemba 1974 mjini Musoma
likisisitiza kwamba ‘Elimu ni Kazi’.
Enzi zile
kila shule, hasa za vijijini, zilikuwa na mashamba zikijishughulisha na kilimo,
ikiwa ni elimu mojawapo ya kumwandaa mtoto aje ajitegemee baada ya kumaliza
elimu yake ya msingi. Kilimo bora kilionekana hata katika Mashamba ya Ujamaa ya
Vijiji ambapo kila kaya ilitakiwa kuwa na walau ekari moja na mazao yaliyovunwa
humo yaliwekwa katika akiba ya kijiji ili kupambana na baa la njaa endapo
lingetokea.
Wananchi
walikuwa tayari kushiriki, lakini ukweli ni kwamba, viongozi wetu – wengi wao –
hawakuwa tayari kuijaribu Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kwa sababu iliwanyima
fursa za kuchuma na kujilimbikizia mali.
Leo hii
watoto hawajui hata mche wa mahindi ukoje, hawajui hata jembe linashikwaje,
wakimaliza elimu ya msingi wanaambiwa ni wadogo, watafanya kazi gani. Lakini
watu hawajiulizi kuhusu wale watoto waliokosa fursa za elimu ambao wengi ni
wadogo kuliko hata hawa wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari, ambao
wanachunga na kulima. Hawasemi kama ni wadogo, badala yake wanapiga kelele
kwamba serikali imeshindwa kazi. Hivi ni kweli?
Tutafakari
katika kipindi hiki na tuone tunawezaje kuinusuru nchi yetu na kongwa hili.
Nakaribisha maoni ya kizalendo.
0656-331974
Makala haya yamechapishwa kwenye gazeti la Risasi, Jumatano, Oktoba 14, 2015.
No comments:
Post a Comment