TAASISI ya Utafiti ya Twaweza imetoa ripoti inayoonesha kuwa wananchi sita kati ya kumi (sawa na asilimia 60) wamesema upinzani utashinda urais mwaka 2025.
Pia, wananchi saba kati ya kumi (asilimia 68) wanafikiri kutakuwa na Rais mwanamke ifikapo mwaka mwaka huo, na wananchi sita kati ya kumi (asilimia 64) wanatabiri kukua kwa uzalishaji wa viwanda na kupungua kwa kilimo.
Mkuu wa Twaweza, Rakesh Rajani alitoa kauli hiyo jana na kubainisha kuwa asilimia 54 ya wananchi wa Tanzania wana matumaini kuwa maisha yao yatakuwa bora zaidi ifikapo mwaka huo.
Rakesh alisema
Katika kipindi cha mabadiliko muhimu ya kitaifa na ya kimataifa, wananchi wa matabaka yote kiuchumi, maeneo na jinsia zote, wana matumaini na siku zijazo nchini Tanzania.
"Changamoto kwa Serikali ya Tanzania, wasomi wa ndani pamoja na wananchi wenyewe, ni kuhakikisha kuwa matumaini haya yanaendelezwa kupitia utungaji sera na utekelezaji wenye ufanisi, kuhimiza maendeleo yenye usawa na kujenga mshikamano wa kijamii", alisisitiza Rakesh.
Alisema Chochote kitakachotokea ziku zijazo, wananchi wanaona mabadiliko makubwa, wananchi sita kati ya kumi wanatabiri kuwa upinzani utashinda urais, na tembo watapotea kabisa ifikapo 2025.
Awali, Meneja Mawasiliano wa Twaweza, Risha Chande alisema asilimia 54 ya wananchi wa Tanzania wanafikiri kuwa maisha yao yatakuwa bora zaidi ifikapo mwaka 2025, ikiwa ni mtazamo wa wananchi hao wakiwa katika makundi yote- vijana kwa wazee, wanaume kwa wanawake na wakazi wa vijijini na mijini.
Mtazamo huo ni tofauti na ule wa nchi za Marekani na Ulaya ambapo karibu wananchi saba kati ya kumi sawa na asilimia 65 wanafikiri kuwa watoto wao watakuwa na hali mbaya zaidi kifedha kuliko walivyo sasa.
Matokeo hayo yalitolewa na Twaweza na Society for International Development (SID) kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina la Tanzania ifikapo mwaka 2025: Je, Watanzania wana matarajio gani na maisha yao ya baadaye?.
Alisema muhtasari huo umetokana na takwimu za sauti za wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika kwa njia ya simu za mkononi.
Utafiti huo hufanyika katika maeneo yote Tanzania Bara (Zanzibar haimo kwenye matokeo haya). Matokeo hayo yametokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,408 Agosti mwaka huu.
"Wakiangalia nchi kwa ujumla, wananchi wawili kati ya watatu wanaamini kuwa Tanzania itakuwa mahali pazuri pa kuishi mwaka 2025.
Chanzo: Habari Leo.
No comments:
Post a Comment