Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday, 27 December 2014

SUMAYE ASEMA, UTAWALA MBOVU HUSABABISHA UVUNJIFU WA AMANI

Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye
Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema Tanzania inastahili kuongozwa na utawala unaomuogopa Mungu ili kuondokana na vyanzo vinavyohatarisha kuondoka kwa amani nchini.


Sumaye aliyasema hayo jana wakati akihutubia katika tamasha la uimbaji na kuliombea  lililofanyika jana kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Katika hotuba yake iliyopatikana jijini Dar es Salaam kwa njia ya barua pepe, Sumaye alisema masuala ya amani yanapojadiliwa nchini, ni lazima kujikumbusha ni nini hasa kinachoharibu hali iliyopo sasa.

 “Kwanza, ni lazima tupambane na mambo yale ambayo ni chukizo mbele za Mungu na tuweke madarakani utawala unaomwogopa Mungu. Wapo watu wanaodhani tukipiga tu magoti Mungu atatuhesabia haki,” alisema.

Alitoa mfano wa Israeli likiwa taifa teule la Mungu, jinsi wafalme wao walipoacha njia za haki na kufanya matendo maovu na Mungu aliwaadhibu, akawaangamiza kwa kuuawa na maadui wao kama Wafilisti au Wakaldiyo.

 “Hivyo ni lazima tuwe tunatenda matendo mema ndipo Mungu tukimwomba atatujalia amani,” alisema na kukumbusha kuwa Waisrael mara zote walipoharibikiwa, walikuwa na mtawala mbovu.

“Hata katika nyakati zetu nchi nyingi zinazopoteza amani mchango mkubwa unatokana na kiongozi mkuu wa nchi husika,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, Watanzania wanapaswa kujiandaa kumpata Rais bora katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Alisema yapo mambo muhimu ya kuangalia katika uchaguzi huo, akitoa mfano wa kukemea maovu na kumpata kiongozi bora, mambo yanayohitaji umakini mkubwa.

Kwa mujibu wa Sumaye, Rais ajaye anapaswa kuwa mzalendo kwa nchi na wananchi wake, mwenye upeo, kutii utawala wa sheria na demokrasia, kuweka madarakani serikali inayowajibika kwa umma, kupambana na umasikini na ukosefu wa ajira.

Pia, alisema Rais ajaye anapaswa kuwa na utashi wa kuboresha huduma za jamii, kupambana na rushwa, ufisadi, dawa za kulevya na maovu mengine kama ujambazi, mauaji na ubakaji.

Sumaye aliongeza kuwa Rais atakayechukua nafasi ya Rais Jakaya Kikwete, anastahili kuwa na uwezo wa kukuza uchumi imara, kusimamia mapato na matumizi ya fedha za umma.

Alisema kwa hali hiyo, Uchaguzi Mkuu wa mwakani ni kigezo muhimu cha kulinda amani na utulivu na akaongeza, “tunaiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) vyombo vyote vinavyosimamia uchaguzi watende haki bila kupinda hata kidogo.”

Alisema haki ikitendeka pasipo kutia shaka, uchaguzi huo utakuwa wa amani na utulivu utadumu nchini.

Aidha, Sumaye aliviasa vyama vya siasa kuwasimamia wanachama na washabiki wao ili washiriki kuilinda amani wakati wa uchaguzi huo.

Sumaye ni mmoja wa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotajwa kutia nia ya kuwania urais kupitia chama hicho.

Hata hivyo, Sumaye alishaweka wazi kuwa ikiwa CCM italipitisha jina na mgombea anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi wa aina tofauti, hatakuwa tayari kumuunga mkono ikibidi hatakuwa pamoja na waliomo katika chama hicho.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment