Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday 27 December 2014

WALIOPOKEA MGAWO WA ESCROW WATAKIWA KUKATWA KODI

Ole Naiko 
Dar es Salaam. Watu waliopokea mgawo wa fedha zilizochotwa kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) huenda wakalazimika kulipa mamilioni ya Shilingi ambayo ni kodi ya mapato ya fedha walizopewa, imefahamika.
Hata hivyo, habari zinasema malipo hayo ya kodi yatafanywa kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi wa vyombo vya dola ambao unawashirikisha maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu uhalali wa fedha walizolipwa.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema juzi kuwa wote waliopokea mgawo wa fedha zilizochotwa kutoka katika akaunti hiyo watapewa fomu za kuthibitisha mapato yao ili wakatwe kodi kutokana na fedha hizo ambazo pia zinapaswa kuhakikiwa na vyombo vya usalama kwamba ni mapato halali.
Alisema taratibu za kufuatilia fedha hizo zimekwishaanza na ifikapo Desemba 31 wahusika watapewa fomu ili kuthibitisha mapato yao ili hatua za kuwatoza kodi zianze.
Msingi wa maelezo ya Nchemba umejengwa kwenye Sheria ya Mapato ya Kodi (Income Tax Act) ya 2012 ambayo inaelekeza mlipaji wa kodi kuwasilisha ankara za hesabu za mapato yake kwa TRA kila ifikapo mwisho wa mwaka na hesabu hizo huiwezesha mamlaka hiyo kutathmini kiwango cha kodi inayopaswa kulipwa na mhusika.
“Hotuba ya Rais (Jakaya Kikwete) imetupa nguvu kuendelea na juhudi ambazo tayari tulikwishazianza tangu awali, maana amesisitiza kwamba lazima kodi ilipwe na sisi hilo ni jukumu letu, tutafuatilia ili kuhakikisha kwamba fedha za walipakodi zinarejeshwa,” alisema Nchemba.
Ikiwa wote waliotajwa watalazimika kukatwa asilimia 30 ya fedha walizopewa kama kodi ya mapato, TRA itakusanya zaidi ya Sh9.3 bilioni ambazo zinatokana na karibu Sh31 bilioni zilizotawanywa kwa watu na kampuni mbalimbali kutoka kwenye akaunti ya mmiliki wa VIP Engineering, James Rugemalira.
Miongoni mwa waliokiri kupokea fedha hizo ni aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye alipata mgawo wa Sh1.6 bilioni akisema fedha hizo zilikuwa ni za mchango wa kulipa mkopo wa shule anayoisimamia.
Hata hivyo, hatua yake hiyo tayari imemgharimu baada ya Rais Jakaya Kikwete kutengua uwaziri wake kutokana na kile alichokiita kuwapo kwa makosa ya kimaadili hasa ikizingatiwa kuwa fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti yake binafsi.
Taarifa ya PAC
Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ikiwasilisha taarifa yake bungeni kuhusu suala hilo mwezi uliopita, pia iliwataja wengine waliochukua fedha hizo kutoka VIP Engineering kuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge (Sh1.6 bilioni), aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye pia ni mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (Sh40.4 milioni) na Mbunge mstaafu wa Sumbawanga (CCM), Paul Kimiti (Sh40.4 milioni).
Wengine ni aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh40.4 milioni), aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk Enos Bukuku (Sh161.7 milioni), Majaji wa Mahakama Kuu, Profesa Eudes Ruhangisa (Sh404.25 milioni) na Jaji Aloysius K Mujulizi (Sh40.4 milioni) pamoja na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko (Sh40.4 milioni).
Pia wamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Daniel Ole Naiko (Sh40.4 milioni), Ofisa wa TRA, Lucy Appollo (Sh80.8 milioni), Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini (Sh80.9 milioni), Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzigirwa (Sh40.4 milioni) na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh40.4 milioni).
Wanastahili kulipa kodi?
Kumekuwa na hoja za kitaalamu kwamba waliopokea fedha hizo hawastahili kulipa kodi yoyote kutokana na madai kwamba hawabanwi na sheria za kodi kwa kuwa malipo waliyopokea hayaangukii katika maeneo matatu yanayopaswa kutozwa kodi ambayo ni uwekezaji, mishahara au biashara.
Akizungumzia hilo Nchemba alisema hata fedha za misaada kutoka kwa wafadhili hutozwa kodi, hivyo hakuna jinsi ambavyo watu waliopokea fedha hizo watakwepa wajibu wa kutozwa mapato ya Serikali.
“Hivi majuzi tu kuna shirika moja kutoka nje ya nchi lilitoa misaada ya vifaa vya uwindaji, tuliwatoza kodi kwa hicho kisingizio kwamba eti walipewa msaada, hakiwezi kusababisha wasitozwe kodi, mapato yoyote yanatozwa kodi, tofauti huwa ni kiwango kinachotozwa tu,” alisema Nchemba.
Kuhusu hoja kwamba fedha hizo ni chafu, naibu waziri huyo alisema madai hayo siyo ya kweli. “Fedha hizi ziliwekwa pale BoT kutoka Tanesco, tatizo ni jinsi zilivyotolewa pale, sasa unawezaje kusema fedha hizo ni chafu? Hizi ni fedha za hapa nchini na hazitokani na mapato ya bangi au dawa za kulevya,” alisema.
Hata hivyo, alisema kwa wale watakaofikishwa katika vyombo vya sheria na kufunguliwa mashtaka kuhusu mgawo waliopewa, Serikali haitachukua kodi kwani watakuwa wameingia katika mkondo tofauti wa kushughulikiwa kisheria.
Ufafanuzi wa TRA
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema hatua ya mamlaka yake kuwapelekea fomu waliopokea fedha hizo ni kuwapa fursa ya kueleza vyanzo vya mapato ya fedha zilizoingizwa kwenye akaunti zao.
“Hatuwezi kufahamu ni kiasi gani au ni kodi ya aina gani hawa watu wanaweza kutozwa, ndiyo maana tunawapelekea fomu ili waonyeshe vyanzo vya mapato yao na baada ya hapo wataalamu wetu watachunguza iwapo fedha zilizoingia kwenye akaunti zao zinapaswa kutozwa kodi na kama ni kodi basi ni ya aina gani,” alisema Kayombo na kuongeza:
“Kuna wale wanaosema kwamba fedha walizopewa ni mchango au msaada, hayo yote yatafuatiliwa na ikumbukwe kwamba kazi hii inafanywa na vyombo vya dola na sisi maofisa wetu wanachukua taarifa kusika kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi unaofanywa,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa sheria za kodi na sheria nyingine za nchi, mapato yanayotozwa kodi lazima yawe ni halali, hivyo TRA inachukua tahadhari ili kukwepa kuhalalisha mapato ambayo baadaye yanaweza kuja kuonekana kupatikana kwa njia zisizo halali.
“Leo hii ukikata kodi katika fedha fulani maana yake unaihalalisha, sasa baadaye ikija kubainika kuwa fedha hizo zilipatikana kwa njia haramu tunaweza kujikuta tunaharibu taratibu za kiuchunguzi. Hivyo, ndiyo maana wataalamu wetu wanafanya kazi kwa ukaribu na vyombo vingine,” alisisitiza Kayombo.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment