Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday, 20 December 2014

MWEKEZAJI KAPUNGA AKODISHA SHULE

Na Daniel Mbega, Mbarali

MWEKEZAJI katika Shamba la Mpunga la Kapunga wilayani Mbarali, kampuni ya Kapunga Rice Project Limited (KRPL), ameikodisha Serikali ya Kijiji shule aliyoijenga.

Wakati mwekezaji anaikodisha shule hiyo, hatma ya shule ya umma iliyojengwa na serikali mwaka 1991 katika eneo la mradi ambayo mwekezaji huyo ameifunga tangu mwezi Mei 2013 mpaka sasa bado haijajulikana.
Mwekezaji huyo aliifunga shule hiyo kwa maelezo kwamba iko kwenye eneo lake alilouziwa na serikali mwaka 2006.
Hata hivyo, shule iliyojengwa na mwekezaji kwenye eneo lake lenye ukubwa wa hekta 3.5 jirani na kitongoji cha Site One badala ya lile aliloelekezwa na wanakijiji, imekodishwa kwa kipindi cha miezi 30 tu (miaka miwili na nusu) kuanzia Julai 8, 2013 hadi Desemba 31, 2015 huku serikali ya kijiji ikitakiwa kulipa Shs. 1 kwa mwaka kama gharama ya ukodishwaji huo.
Mkataba wa maridhiano ya ukodishaji uliosainiwa na mwekezaji Wally Vermaak, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kapunga Ramadhan Nyoni na Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mikidadi Athumani siku ya Ijumaa Julai 5, 2013 unaonyesha mkanganyiko wa maelezo yake.
Miongoni mwa vipengele vinavyokanganya ni kile kinachoeleza kwamba mkataba huo utakoma Desemba 31, 2015 wakati kingine kinasema ni mkataba wa kudumu hadi pale serikali itakapotoa hati tofauti za ardhi, ambapo kimsingi mwekezaji huyo kwa miaka nane sasa anasema eneo lote ni lake na kuwataka wanakijiji wa Kapunga waondoke.
Aidha, ili kupata haki ya kumiliki eneo hilo la shule, mkataba huo unasema Halmashauri ya Kijiji cha Kapunga na Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali ndio washughulikie mgawanyo huo wa hati miliki.
Emmanuel Kasekwa, mkazi wa Kapunga, ameshangazwa na taarifa kwamba mwekezaji amewakodisha shule bila kujua hatma ya fidia ya shule ya umma.
“Kama alitaka kufidia shule baada ya kuifunga ile ya umma kwenye eneo lake, kwa nini atukodishe hii? Tena kwa nini alikataa kuja kujenga hapa kijijini akaijenga kwenye eneo lake? Serikali ituambie kuhusu ile shule ya umma inafidiwaje.” alisema.

Mkuu wa Wilaya hajui
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Gullamhussein Kifu, alikanusha taarifa kwamba mwekezaji huyo ameifunga shule ya msingi na akasema mwenye uwezo wa kufanya hivyo ni serikali.
Kifu alisema hana taarifa ya mwekezaji kuikodisha kwa serikali ya kijiji shule ya msingi aliyoijenga ndani ya eneo lake, lakini alipoulizwa inakuwaje anashindwa kujua hilo wakati mkataba umesainiwa na Mwanasheria wa Halmashauri, alisema: “Kama hamna ushahidi msipende kuwazushia watu, inaweza kuleta matatizo makubwa.”
Uchunguzi unaonyesha kwamba, mwekazaji aliikabidhi shule hiyo Julai 5, 2013 ambapo Mkuu wa Wilaya akiwa ameongozana na Mwanasheria wa Wilaya ndiye aliyepokea funguo za shule na kumkabidhi mwenyekiti wa Kijiji cha Kapunga.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ramadhan Nyoni, alikiri kwamba aliyepokea funguo hizo ni Mkuu wa Wilaya, Gullamhussein Kifu na akamkabidhi yeye.
“Baada ya kunikabidhi akaniambie niende nikasaini mkataba huo kwa niaba ya serikali. Nikasaini tukiwa pamoja na Mwanasheria wa Wilaya, lakini sikujua vipengele vilikuwa vinasemaje kwa sababu mkaataba umeandikwa kwa lugha ya Kiingereza,” alisema mwenyekiti huyo.

Walitaka sekondari
Aidha, inaelezwa kwamba, baada ya kukabidhiwa shule hiyo, Halmashauri ya Kijiji iliitisha mkutano Julai 18, 2013 na suala la shule hiyo lilikuwa agenda ya tatu ambapo walipendekeza itumike kama shule ya sekondari ya Kata ili kuwasaidia wanafunzi kutoka vijiji vya Kata ya Itamboleo.
“Imeazimiwa kuwa shule aliyokabidhi mwekezaji iwe shule ya sekondari ambayo itanufaisha Kata ya Itamboleo ambayo ina vijiji vya Kapunga, Itamboleo, Mbalino na Matebete, hata hivyo (wananchi) wameona haiwezi kuwa shule ya msingi kwa kuwa eneo lake ni hatari kwa watoto wadogo kiusalama kwani kuna mfereji wa maji,” yalisema maazimio ya kikao hicho, ambayo nakala yake ilipelekwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya kwa Kumb. Na. MB/KIJ/936/DED/Vol. 1/06.

Mgogoro wa shule
Mgogoro kuhusu shule ya msingi Kapunga unakwenda sanjari na mgogoro wa ardhi ya kijiji hicho tangu serikali ilipouza lililokuwa Shamba la NAFCO Kapunga mwaka 2006 kwa Kampuni ya Export Trading Co. Ltd.
Taarifa za uchunguzi zinaeleza kwamba, baada ya mwekezaji kuuziwa shamba hilo kwa thamani ya Shs. 2.311 bilioni, aliwafukuza walimu wote waliokuwa wakiishi katika nyumba zilizojengwa na shirika.
Hali hiyo iliwafanya walimu hao kwenda kupanga Chimala, umbali wa kilometa 26 kutoka shuleni na kulazimika kutembea kwa miguu ama kukodi bodaboda kila siku.
Williard Sengele (58) ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kapunga, anasema yeye na familia yake ya watu sita walilazimika kuishi kwenye chumba cha darasa tangu Desemba 6, 2006 hadi Januari 6, 2007 kutokana na kukosa mahali pengine pa kuishi kabla ya kupata nyumba ya kupanga Chimala.
Anasema tangu wakati huo, walimu karibu wote wamekuwa wakitembea umbali wa kilometa 52 kila siku kwenda na kurudi shule, hali ambayo imeleta changamoto kwa baadhi ya vipindi kutofundishwa ipasavyo.
“Walimu wengi wamekuwa wakichelewa kwa sababu wanaishi Chimala, ambako walihamia baada ya kufukuzwa mwaka 2006 kutoka kwenye nyumba walizokuwa wakiishi wakati NAFCO ikimiliki shamba la mpunga la Kapunga,” anasema Sengele.
Shule hiyo ilijengwa na NAFCO mwaka 1991 baada ya kuanza uzalishaji kwenye shamba hilo.  Shirika hilo liliihamisha shule hiyo iliyosajiliwa rasmi mwaka 1977 ikiwa na Hati Na. MB 08/1/022 kutoka kijijini hadi kwenye eneo la shirika ikiwa ni njia ya kuwapatia makazi bora walimu ambao walikuwa wakiishi kwenye nyumba zilizoezekwa kwa nyasi kijijini. Kufuatia uhamisho huo, majengo ya zamani ya shule pamoja na nyumba za walimu yakabomolewa.

Mwekezaji agoma
Wakati alipoifunga shule ya umma kwenye eneo lake, mwekezaji huyo aligoma kusikiliza ushauri wa viongozi wa kijiji wa kwenda kujenga shule hiyo mahali ilipokuwepo awali kabla ya kuhamishiwa kwenye eneo la mradi kwa maelezo kwamba hata wanakijiji wanatakiwa kuhama.
Hali hiyo iliwakasirisha wanakijiji hao ambao waliamua kuchanga fedha na nguvukazi na kujenga vyumba 9 vya madarasa, ofisi mbili za walimu, vyoo pamoja na nyumba mbili za walimu.
Tayari shule hiyo inafanya kazi tangu ilipofunguliwa Julai 8, 2013.

Mgogoro uliopo
Tangu kuuzwa kwa shamba hilo, mgogoro wa ardhi unaendelea kufuatia mwekezaji kusema hata Kijiji cha Kapunga kimo ndani ya eneo lake ambalo amekabidhiwa hati yenye namba 6249 ikionyesha kwamba eneo hilo lina ukubwa wa hekta 7,850.
Hata hivyo, wananchi wanapinga madai hayo na kuilaumu serikali kwamba iliuza shamba, kijiji na huduma za jamii kwa makosa kwa vile shamba lililokuwa linamilikiwa na NAFCO ni hekta 5,500 tu ambazo Halmashauri ya Kijiji iliridhia kulitoa kwa serikali katika kikao kilichofanyika Novemba 14, 1985.
Inaelezwa kwamba, mradi huo uliofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) ulilenga kujenga miundombinu ya shamba la NAFCO la hekta 5,500 na shamba la wakulima wadogo lenye ukubwa wa hekta 800, wakati ambapo eneo la kijiji ni hekta 1,070.
Kwa kuwa mradi wote ulikuwa ukijulikana kama Mradi wa Umwagiliaji Kapunga (KRIP) ukiwa na hati moja tu, serikali ilipouza shamba la NAFCO haikujishughulisha kutengeneza hatimiliki ya shamba hilo na badala yake kutoa hatimiliki ya jumla, ambayo ilihusisha kijiji, shamba la wakulima wadogo na lile la NAFCO.
“Hali hii ikafanya kijiji kiuzwe pamoja na huduma zote za jamii, mwekezaji hataki kuamini ukweli kwamba hata eneo ambalo lilitangazwa kwenye zabuni ni hekta 5,500 na siyo 7,850 kama anavyong’ang’ania,” anasema Brighton Ngella, mkazi wa Kapunga.
Sera ya Taifa ya Uwekezaji inaelekeza kwamba, mwekezaji anapaswa kuendeleza huduma za jamii kama shule na zahanati katika maeneo yanayozunguka mradi wake.
Sergei Bekker, meneja uzalishaji wa Kapunga Rice Project Limited, aliwahi kumweleza mwandishi wa habari hizi kwamba wangejenga shule katika eneo la Site One na kuihamisha ya sasa katika eneo hilo ili kuisaidia jamii.
“Hatuwezi kujenga shule kwenye Kijiji cha Kapunga kwa sababu ni ardhi yetu. Tulitaka kujenga kule Matebete, lakini serikali imesema wananchi wale wanapaswa kuhamishwa kwani ni eneo la TANAPA. Wakazi wa Kapunga hawataki kututambua kama wawekezaji na hili ndilo tatizo linalochelewesha mradi wa ujenzi wa shule,” alisema.
Katika ziara yake ya Januari 2014, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alisema mwekezaji huyo anapaswa kurejesha hekta 1,870 kwa wananchi bila masharti yoyote.

No comments:

Post a Comment