Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amejiuzulu nafasi yake hiyo kuanzia jana kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Katika barua yake kwa Rais Jakaya Kikwete, Jaji Werema alisema ameomba kujiuzulu kwa sababu; “ushauri wake kuhusiana na suala la Escrow hakueleweka na umechafua hali ya hewa.”
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilisema jana kuwa Rais Kikwete amekubali ombi hilo la kujiuzulu na amemshukuru Jaji Werema kwa; “utumishi wake ulioongozwa na uaminifu na uadilifu.”
Jaji Werema ambaye mara kwa mara amekuwa akitetea ushauri katika sakata hilo, amechukua uamuzi huo katika siku ya mwisho ya wiki moja iliyoahidiwa na Rais Kikwete kukamilisha uchambuzi wa taarifa za Bunge na kutoa uamuzi dhidi ya wahusika wa sakata hilo.
Uamuzi wa Werema unatokana na mazimio ya Bunge ya kutaka yeye na baadhi ya vigogo wachukuliwe hatua kutokana na madai ya kuhusika kwenye sakata la uchotwaji fedha katika akaunti hiyo.
Mwanasheria huyo alilalamikia maazimio hayo akisema hayakuwa ya haki kwa wote waliotuhumiwa na uamuzi huo ulifanywa kwa hasira na kufuata mkumbo.
Bunge liliazimia Jaji Werema kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria kutokana na kuipotosha Serikali kuhusu malipo ya Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow, akishauri fedha hizo zilipwe kwa Kampuni ya IPTL iliyo na mkataba wa ufuaji umeme na Tanesco bila ya kukata kodi.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment