Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday, 6 December 2014

KAFULILA AMNG'ANG'ANIA MMILIKI WA IPTL

David Kafulila akizungumza jana jijini Dar es Salaam.

Mbunge wa Kigoma Kusini kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi, David Kafulila, amezidi kumng’ang’ania mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme (IPTL), Harbinder Sethi (pichani), akidai ameiweka serikali mfukoni ndiyo maana inamkingia kifua licha ya kuidhalilisha nchi kimataifa.


Kafulila alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ziara ya chama chake mkoani Kigoma inayotarajia kuanza leo.

Ziara hiyo, pamoja na mambo mengine imelenga kuwaeleza Watanzania kuhusu ufisadi huo uliofanywa kwenye akaunti ya Escrow.Aidha, kuwashawishi wananchi kutoichagua CCM kwa kushindwa kusimamia serikali yake dhidi ya sakata hilo.

KAFULILA AMJIBU SETHI
Kuhusu hoja aliyotoa juzi Sethi ambaye pia ni mmiliki wa Kampuni ya Pan African Power Solutions (PAP), kuwa anafikiria upya uamuzi wake wa kuendelea kuwekeza Tanzania, Kafulila alisema mfanyabiashara huyo sio mwekezaji bali ni tapeli ambaye anapaswa kutiwa nguvuni.

Alisema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imebainisha wazi kuwa mfanyabiashara huyo alinunua IPTL kwa nyaraka za kughushi ambapo ni kosa la jinai.

“Rais anapaswa kuchukua hatua kuondoa aibu na fedheha hii inayofanya nchi yetu kuonekana imewekwa mfukoni mwa mfanyabiashara huyu tapeli, tumesitishiwa ufadhili kwa sababu ya sakata hili, kwa nini tumkumbatie tapeli huyu,” alisema na kuongeza:

“Huyu ni tapeli amepora fedha zetu, afadhali wawekezaji matapeli tuwakose kuliko waidhalilishe nchi yetu kimataifa, mfikishieni taarifa kuwa yeye sio mwekezaji bali dhaifu, ana bahati amekutana na serikali dhaifu, angekuwa anazungumzia jela maneno hayo,” alisema.

Aidha, alidai mfanyabiashara huyo amekuwa jeuri kwa kuwa anajua mchezo alioucheza umeshirikisha watu wakubwa serikalini.

WALIOKULA FEDHA
Kafulila alisema jeuri ya vigogo wa serikali kukataa kujiuzulu tofauti na kawaida ni mtego kwa Rais Jakaya Kikwete. Alidai kuwa, ushahidi unaonyesha baadhi ya maofisa wa Ikulu kuhusika katika sakata hili na ndiyo maana inawapa jeuri wahusika kuona kuwa hawapo peke yao kwenye sakata hilo.

“Rais anapaswa kusafisha kuanzia Ikulu ili kuipa ofisi yake uhalali kwani watendaji wake wasio waadilifu kama hawa wanaotakiwa kujiuzulu na kugoma,” alisema.
Alihoji kuwa CCM kama hakina mamlaka ya kuwachukulia hatua vigogo hao, kinapataje uhalali kuendelea kuchaguliwa.

“Viongozi wa CCM, kina Kinana, Mangula wametamka watu hao wachukuliwe hatua, Bunge nalo limetamka hilo, iweje Ikulu iwabebe, wananchi sasa mnatakiwa mpime wenyewe, hakuna sababu ya kuichagua CCM kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kuanza wiki ijayo na chaguzi nyingine,” alisema.

Aidha, alimtaka Rais Kikwete kuchukua hatua dhidi ya sakata hilo kabla ya wananchi hawajafanya hivyo. Kadhalika, alisema katika utoaji wa fedha kwenye akaunti ya Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu, Baraza la Mawaziri halikujulishwa zaidi ya kujadili suala hilo baada ya sakata hilo kutokea. Alisema huo ni ushahidi tosha kuwa Ikulu inahusika kwenye suala hilo.

Aliongeza kuwa, kufuatia sakata hilo, wangekuwa na Spika wa Bunge anayejua anaongoza muhimili wa mwisho, ilitosha nchi kuingia katika uchaguzi mkuu lakini maamuzi yaliyofikiwa ni madogo ambayo hata hivyo, Kafulila amesema hayatatekelezwa kama yale ya Richmond.

MAASKOFU
Kuhusu viongozi wa dini waliopata mgao wa fedha kutoka kwa Mkurugenzi wa VIP Engeering, James Rugemalira, alisema anaona hawana tatizo kwa kuwa, mamlaka zao haziwezi kushinikiza au kusaidia fedha hizo zitoke.

“Rushwa lazima iwe na vishawishi ambavyo vinasababisha mtu/watu wafanye kitu fulani, watu wa mamlaka kwa sababu mamlaka zao kwa namna moja au nyingine zilihusika kwa mfano jaji, waziri, viongozi wa dini hakuna sheria ambayo wao wanaweza kuipindisha ili fedha ziweze kutoka,” alisema.

HOFU YA RIPOTI KUTOTOKA
Alisema ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) dhidi ya IPTL iliyojaa jinai za wahusika kama ilivyofichwa ya mwaka 2000, anaamini  ya sasa itafanyiwa hivyo kwa kuwa Ikulu ina uzoefu wa hilo.

Alisema katika kongamano la Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi Kusini mwa Bara la Afrika (SADC) kuhusu rushwa lililofanyika mjini Mwanza Novemba 3, mwaka huu, Mkurugenzi wa Takukuru Dk. Edward Hosea, alisema  ripoti yake ameshamkabidhi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ingawa alikana.

“Ndiyo maana nasema hii siyo mara kwanza Ikulu kuficha ripoti za Takukuru kuhusu ufisadi wa IPTL, mwaka 2000 ilichunguza kuhusu vigogo waliohusika katika mkataba huu na namna rushwa ilivyotumika lakini haikutoka,” alisema.

BUNGE LIJALO
Kafulila alisema atahakikisha bunge linapata mrejesho na majibu ya yale yaliyoazimiwa kwenye sakata hilo ikiwa hayatafanyiwa maamuzi.NCCR-Mageuzi ni miongoni mwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi(UKAWA). Vyama vingine nChadema, CUF,na NLD.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment