Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Aboud Mohamed Aboud.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 2:00 usiku wakati askari hao wakilinda hoteli ya kitalii ya Bongwe Bay Resort iliyopo wilaya ya Kati katika mkoa wa Kusini Unguja.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Zanzibar (SACP), Agostino Ollomi, alisema wakati askari hao wakiwa katika shughuli zao za ulinzi hotelini hapo, lilitokea kundi la watu wanaodaiwa kuwa majambazi na kuvamia hoteli hiyo.
Alimtaja aliyeuawa kwa kupigwa risasi kuwa ni Koplo (E560) Muhammed Mjombo (44) na kwamba Koplo (F 6198) Ibrahim Juma alijeruhiwa.
Alisema kuwa majambazi hayo yalitumia bunduki aina ya SMG au SRA na kwamba baada ya tukio hilo walitoweka na bunduki ya SMG ikiwa na risasi 30 mali ya Jeshi la Polisi.
Bunduki hiyo iliporwa na majambazi hayo kutoka kwa Koplo Ibrahim pamoja na simu ya mkononi, mali ya raia wa Italia, Suzan.
Alisema hoteli hiyo inamilikiwa na Jiovanne Rundo, raia wa Italia na kwamba watu hao hawakufanikiwa kupora wala kudhuru wageni hotelini hapo.
Ollomi alisema kuwa askari aliyefariki tayari mwili wake umeshakabidhiwa kwa jamaa zake na kuzikwa kwa heshima zote za kijeshi na kuongeza kuwa ameacha wajane wawili na watoto watano.
Alisema Koplo Ibrahim alipata majeraha katika bega na amelazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mnazi Mmoja na hali yake inaendelea vizuri.
Hata hivyo, alisema hadi sasa watu watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
NIPASHE lilipofika katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, mwandishi hakuruhusiwa kuonana na Koplo Ibrahim hadi jioni wakati wa kuwaona wagonjwa.
Hata hivyo, Katibu wa hospitali hiyo, Hassan Makame, alisema hali ya majeruhi huyo ilikuwa inaendelea vizuri.
Kutokana na matukio kadhaa ya kuwapora watalii, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) mwaka jana ilianzisha mikakati ya kudhibiti hali hiyo kwa kuanzisha utaratibu wa kuvitumia vikosi vyake vya ulinzi na usalama kulinda maeneo mbalimbali ya kitalii zikiwamo hoteli.
Utaratibu huo ulitangazwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Aboud Mohamed Aboud na Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo, Said Ali Mbalu.
SMZ ilielekeza kwamba vikosi vyake vikiwamo Polisi, Valantia, JKU, KMKM na Magereza vitatumika kulinda maeneo hayo zikiwamo hoteli baada ya kushauriana na wamiliki wake.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment