Benson Kigaila
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimelitaka Jeshi la Polisi mkoani Iringa kuwakamata na kuwafungulia mashitaka ya uhalifu, watu watatu inachodai kuwa ni majambazi sugu ambao wameingia mkoani hapa wakitokea jijini Mwanza baada ya kukodiwa na mahasimu wao kisiasa kwa ajili ya kutekeleza matukio ya uhalifu kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga zinaoendelea.
Madai hayo yalitolewa na Mkuu wa chama hicho wa Operesheni ya Uchaguzi Jimbo la Kalenga, Benson Kigaila, wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Iringa jana.
Alidai kuwa, watu hao wamekodiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoka wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza na kupelekwa katika jimbo hilo wakitumia gari dogo aina ya Toyota Noah.
“Pamoja na mambo mengine, wameletwa katika uchaguzi huu kwa ajili ya kufanya uhalifu, ikiwemo kujeruhi, kuzusha ghasia na ikiwezekana kuua baadhi ya wafuasi wanaokiunga mkono Chadema katika kampeni hizo” alidai na kuongeza:
“Hali ni mbaya kwa sasa katika kampeni hizi za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga kwa sababu wenzetu wameleta watu wa kukodi ambao wana rekodi mbaya za uhalifu katika mikoa ya Mwanza, Arusha na Dodoma.
Baadhi yao wameshafika Kalenga, lakini pia wamo wengine waliokodiwa wanafanya mazoezi ya vitendo katika kijiji cha Ihanga na kambi ya CCM kule Ihemi.”
Kigaila aliyekuwa amefuatana na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare na Meneja kampeni, Alphonce Mawazo, alidai kikundi cha ulinzi cha chama hicho (Red Brigade) kimemkamata mtu mmoja ambaye ni mmoja wa watu waliokodiwa na mahasimu wao kuiteketeza kambi yao katika kijiji cha Wasa.
”Huyu (anataja jina) tumemkamata alfajiri ya leo (jana) saa 10:36 baada ya wenzake kufanikiwa kukimbia, lakini tumemhoji atueleze ametumwa na nani na wenzake ni akina nani. Amekiri kwamba walitaka kuichoma ngome yetu ya Wasa na kwamba yeye ni mkazi wa kijiji cha Iringa-Mvumi katika Jimbo la Mtera, mkoa wa Dodoma,” alisema.
Alipoulizwa na NIPASHE kuhusiana na madai hayo ya Chadema, Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga, alisema kamwe chama hicho hakiwezi kukodi majambazi au watu wenye rekodi mbaya za uhalifu ili kutekeleza madai hayo isipokuwa wanachokifanya Chadema ni kutaka kuhatarisha amani.
”Sisi tutaendelea kutunza amani na katika hili ninawaonya Chadema wasijaribu kutaka kuvuruga amani ya Jimbo la Kalenga na kwa sababu hiyo wakibipu, sisi tutawapigia. Wao wamewaleta watu na Fuso zipatazo 14 wanafikiri hatujui halafu wanasema sisi ndio tunaleta majambazi,” alisema Mtenga.
Kamanda wa Polisi Mkoani Iringa, Ramadhan Mungi, aliiambia NIPASHE kuwa mambo yanayojitokeza hivi sasa katika uchaguzi huo ni kutokana na kupanda kwa joto la uchaguzi ikiwamo matumizi ya propaganda ambazo vyama vote vya siasa zinazihusisha moja kwa moja na tetesi ili kubomoana kwa wapiga kura.
”Hali halisi ya usalama katika Jimbo la Kalenga na mkoa wetu kwa ujumla ni salama kwa kiasi kikubwa na kimsingi, vyama vyote vimekuwa vikitoa tetesi mbalimbali ambazo mara nyingi zinakuwa ni mtu amezitengeneza na akishazitengeneza anakuwa amezipa uzito na kusambaa kwa haraka” alisema na kuongeza:
“Nimewaeleza watu wa vyama vyote kwamba tetesi ni hatari kwa kuwa jambo hilo hupokelewa na makundi matatu ya Watu, wamo wenye uwezo mkubwa wa kuchambua mambo, wapo ambao hawana uwezo mkubwa sana wa kuchambua mambo na wapo wenye kupokea na kusambaza kile walichoambiwa bila ya kutafiti na ndo maana haya yanatokea.”
Hata hivyo, Kamanda Mungi alisema kwa kuwa hayo ni malalamiko ambayo yanapaswa kuripotiwa polisi na kufanyiwa kazi, polisi mkoa wa Iringa watachunguza kwa umakini na kwamba anawahakikishia amani wananchi wa Kalenga na mji wa Iringa kwa ujumla.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment