Na Sharon Sauwa, Mwananchi
Dodoma. Makundi ya urais ndani ya CCM ni miongoni mwa mambo ambayo yameuteka mjadala wa Akaunti ya Escrow katika Bunge.
Tangu kuanza kwa mjadala wa Akaunti ya Escrow Jumatano iliyopita kumekuwa na sintofahamu iliyotokana na baadhi ya wabunge wa CCM kujikita katika kuangalia urais zaidi.
Hali hiyo ilifanya kupunguza ushiriki mzuri wa baadhi ya wabunge kuhofia kuingizwa kwenye chuki ya makundi ya urais kupitia mjadala huo.
Baadhi yao walisikika wakishutumu hatua ya uchotaji wa fedha hizo, kiasi cha Sh321 bilioni katika makundi madogo madogo nje ya Ukumbi wa Bunge, lakini hawakuonekana wakichangia ndani ya Bunge.
Hata hivyo, hatua ya vyama kupewa jukumu la kupeleka majina ya wachangiaji katika ofisi ya Katibu wa Bunge, nayo inaonekana kuwanyima fursa baadhi ya wabunge kuchangia katika mjadala huo.
Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimroad Mkono ni mmoja wa waathirika wa utaratibu huo, ambapo alilalamika bungeni kuhusu kutopewa nafasi ya kuchangia.
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu alimwambia aende kwenye chama chake akazungumze nao maana wao ndiyo walioleta majina ya wachangiaji.
“Mimi niliomba kuchangia, lakini nikapewa masharti kama ninataka kuipata nafasi hii niwasaidie (Serikali),” alisema mbunge mwingine wa CCM ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Makundi ya urais
Shinikizo la kutaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kujiuzulu katika nafasi hiyo linatajwa kuwa ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kuwa ni mbinu za kumchafua ili mbio zake za kusaka urais ziingie dosari.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira alisema kama kuna watu ambao wanataka urais kwa kuchafuana, hawafai kushika nafasi hiyo.
Mbinu hizo chafu zinatajwa kufanywa na wabunge walio ndani ya chama chake ambao wanatajwa kuyaunga mkono makundi mengine.Hofu hizi za makundi ya urais, yameufanya mdahalo huo kwa upande wa CCM kujikita katika kuhakikisha kuwa kila mmoja anajilinda ili asilichafue kundi alilomo.
Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, alisema ndani ya ukumbi huo wa Bunge kuna makundi manne. Alitaja kundi la kwanza ni wafanyabiashara, kundi la waliopewa fedha na wasiopewa na wale wanaotajwa kugombea urais.
Madhara ya kuwapo kwa makundi haya yamefanya mjadala huo kujikita katika malengo ya baadhi ya wabunge badala ya manufaa ya Taifa.
Hata hivyo, huwezi kuweka kando itikadi za vyama katika mjadala huo hasa kwa CCM ambapo baadhi ya wabunge walishindwa kuweka kando itikadi zao za vyama.
Staili ya mjadala
Kwa mara ya kwanza Bunge limeshuhudia mjadala ukienda hadi saa 5.00 usiku huku Serikali ikipewa muda wa zaidi ya saa 2.00 kujitetea.
Tofauti na mijadala mingine ambayo imewawajibisha mawaziri katika kashfa ya Richmond na Operesheni Tokomeza mjadala huu ulitoa nafasi ya wanaotuhumiwa kujieleza kabla ya michango ya wabunge. Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo, alipewa nafasi hiyo ya kuitetea Serikali kabla ya wabunge wengine kuanza kuchangia.
Serikali ilichapisha vitabu vilivyobeba maelezo ya Serikali ambayo yalitolewa na Profesa Muhungo.
Mbali na hilo, wakati wa kupitisha maazimio hayo serikali ilileta hoja za kubadili mapendekezo ya Kamati ya Bunge, Hesabu za Serikali (PAC).
Hali hiyo inawafanya wabunge akiwemo Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka na Lekule Laizer (Longido-CCM) kuhamaki kuhusiana na utaratibu huo huku wakitaka kama wahusika hawatawajibishwa basi mawaziri waliowahi kuwajibishwa waombwe radhi na wabunge.
Vikao vya wabunge wa CCM
Katika skendo zilizopita zilizowahi kujadiliwa bungeni kwa mara ya kwanza sakata hili limekuwa na vikao vingi vya wabunge wa CCM ambavyo vimelenga ama kuupoozesha mjadala ama kufanya jitihada za kuwasaidia mawaziri wasiwajibike.
Vikao hivi kwa nyakati tofauti viliwashirikisha Pinda, Makamu ya Rais Dk Gharib Bilal na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula. Hata vikao hivyo havikuweza kuwaleta pamoja wabunge wa CCM katika suala hilo licha ya kukutana wakati mwingine hadi usiku wa manane.
Hali hiyo imejionyesha katika mijadala iliyokuwa ikijitokeza bungeni, baadhi ya wabunge na mawaziri waligawanyika kwenye makundi mawili.
Makundi hayo ni wale waliotaka uwajibikaji wa wahusika na wale waliotaka kusiwapo na uwajibikaji kwa madai fedha hizo hazikuwa za umma.
Licha ya mjadala huo kutawaliwa na aina tofauti ya uchangiaji, lakini kitendo cha Serikali kutaka wanaotakiwa kuwajibika, kuchunguzwa na kuachiwa mamlaka za uteuzi kiliibua vurugu.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment