Na Boniface Meena na Sharon Sauwa, Mwananchi
Dodoma. Bunge limehitimisha mjadala wa Kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow kwa kupitisha maazimio manane, likiwamo la kuwawajibisha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Wengine waliowajibishwa pamoja na mawaziri hao ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) na kuwavua nyazifa zao wenyeviti watatu wa kamati za kudumu za Bunge.
Wenyeviti waliovuliwa nyadhifa zao ni Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja na Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge. Viongozi hao wamevuliwa nyadhifa zao chini ya azimio la Bunge namba mbili.
Maazimio hayo mapya manane yalisomwa bungeni jana jioni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe.
Akizungumza bungeni Zitto alisema, mabilioni ya fedha yaliyotolewa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow yametumika kuwapa kile kinachoonekana kuwa ni rushwa.
Zitto alisema baadhi ya watu waliochukua fedha hizo ni viongozi wa umma na maofisa wa Serikali kama mawaziri, majaji, wabunge, wenyeviti wa kamati za Bunge, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu binafsi.
“Vitendo vilivyofanywa na watu hawa vinaashiria uzembe na makosa mbalimbali ya jinai kama vile wizi, ubadhilifu kutakatisha fedha haramu, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na kupokea mali ya wizi,” alisema.
Alitaja azimio la kwanza la Bunge ni kulitaka Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.
Zitto alisema watu wote waliotajwa na taarifa maalumu ya kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Escrow na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea kuhusika katika vitendo hivyo vya jinai, watachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Azimio la tatu ni kuzitaka Kamati husika za kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya mkutano wa 18 wa Bunge kuwavua nyazifa zao za wenyeviti wa kamati husika za Bunge. Zitto alitaja azimio la nne ni la kumuomba Rais auende Tume ya kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Alisema utaratibu wa kushughulikia nidhamu za majaji kwa mujibu wa Katiba unamtaka Rais kuunda Tume ya Uchunguzi ya Kijaji, kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji.
Pia azimio la tano ni mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Benki ya Stanbic na benki nyingine yoyote itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow, kuwa taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.
Azimio la sita alilitaja Zitto kuwa ni kuiomba Serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria iliyounda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahususi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisasa.
Alisema azimio la saba la Bunge ni kuitaka Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za shirika hilo.
Katika azimio lake la nane Bunge liliazimia kwamba Serikali itekeleze azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge la Bajeti Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme.
Mbowe, Filikunjombe, Wassira
Wakichangia mapendekezo hayo mapya yaliyosomwa na Zitto, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe alisema wamekubaliana na mapendekezo hayo mapya manane yanayotosha kufikisha ujumbe.
Alisema ni muhimu viongozi wa Serikali wakalinda rasilimali za nchi kwa kutekeleza wajibu wao wakijua Watanzania wengi masikini wanawategemea wao kuwatoa kwenye umaskini.
“Niombe tu Waziri Mkuu awe mkali ili tusifike kwenye mshike mshike kama huu tuliofikia kwa sasa,” alisema Mbowe na kuongeza: “Waziri Mkuu uwe mkali kwa kweli.”
Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) alilishukuru Bunge kwa kufanya kazi yake akieleza kuwa limeweka maslahi ya nchi kwa kushikana pamoja.
“Kumekuwa na makosa yamefanyika kwenye baadhi ya maeneo, hivyo hatua zimechukuliwa,” alisema Filikunjombe.
Alisema anafurahi kwamba hatua stahiki zimechukuliwa kwa waliohusika.
“Sasa hatua stahiki zitachukuliwa kwa kila mmoja kwa nafasi yake,” alisema.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu, Stephen Wasira alisema juzi hali ilikuwa mbaya, lakini wameweza kuridhiana kwa kuwa wote ni binadamu.
Alisema mtafaruku uliotokea umewafundisha kwamba wanaweza kukubaliana wakijadiliana.
“Kazi haikuwa rahisi, lakini tumeelewana na aliyosema Zitto ndiyo tuliyokubaliana kwa kuwa CCM haina sera ya kukubali jambo lolote ambalo linaminya maendeleo ya wananchi,” alisema.
Alisema Serikali ina wajibu wa kutekeleza maazimio ya Bunge hivyo yanayowagusa wenzao ndani ya Serikali watawajibika kwa kuwa ndiyo wajibu.
“Sasa hivi kila mhimili umeguswa hivyo tutatekeleza,” alisema Wasira.
Spika Anne Makinda aliwaonya wabunge kuachana na watu wenye fedha wanaotoa kwa lengo la kuwahonga, kwani zitawaweke pabaya kwa kuwa hawana kinga za makosa ya jinai.
Bunge laendelea jana asubuhi
Baada ya juzi Spika Makinda kuahirisha Bunge kwa kushindwa kufikia mwafaka, jana Bunge liliendelea asubuhi, lakini baada ya wabunge kuingia Spika alitangaza kuahirisha Bunge hadi saa tano asubuhi ili vyama vikafanye vikao kwa ajili ya kutafuta suluhu ni maneno gani yatumike katika mapendekezo ya Kamati ya PAC yanayotaka kuwang’oa vigogo wote wa Serikali wanaotuhumiwa kuhusika na sakata hilo.
Wakati Spika akitoa maelekezo hayo tayari asubuhi na mapema wabunge wa Kambi ya Upinzani walioungana wote walikuwa wameshakutana kwenye Ukumbi wa Msekwa kuweka msimamo kuhusu mapendekezo hayo.
Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema) Mchungaji Peter Msigwa walisema kuwa kikao chao kiliamua kuwa wasimamie mapendekezo yote yaliyopendekezwa na kamati kama yalivyo na lisibadilishwe hata moja.
Selasini alisema wabunge wa CCM wanachotaka kufanya ni kuwaokoa watuhumiwa, lakini wao wanaingia bungeni na msimamo mmoja wa kutaka mapendekezo yote ya PAC yapite kama yalivyo.
“Wakikataa tutamalizana pale ndani,” alisema Selasini huku Msigwa akisema, “Wanataka kutufanyia uhuni, sisi tunataka mapendekezo yote ya kamati yapite kama yalivyo.”
Wakati upinzani ukiwa na msimamo huo na kuendelea na shughuli zao Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alionekana akizunguka kuwaomba wabunge wa CCM waelekee White House (Makao Makuu ya CCM Dodoma) kwa ajili ya kikao chao.
Hata hivyo, wabunge wengine wa CCM walionekana kutojali kikao hicho huku wakiendelea mazungumzo na wabunge wa upinzani huku wakipongezana na wengine wakikandiana kutokana na jambo lililotokea juzi.
Bunge larejea saa tano na kuahirishwa
Kikao cha Bunge kilirejea jana saa tano baada ya kuahirishwa asubuhi na Spika alimpa nafasi Lukuvi ambaye alitoa hoja ya kuomba Bunge liridhie kuongeza muda wa saa moja kwa ajili ya pande zote mbili kufanya mashauriano na kurudi na kauli moja kama Bunge. “Nilikuwa naomba tuahirishe Bunge kwa saa moja ili tuendelee na mashauriano na kuja na kauli moja,” alisema Lukuvi.
Hoja hiyo ilipingwa na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika aliyesema kuwa haiwezekani wakatoka nje kwenda kwenye mashauriano ya kukubaliana na msimamo wa CCM na kusema ni kauli moja ya Bunge. “Haiwezekani tukatoka na kauli moja kwa kuweka msimamo wa misimamo ya kichama,” alisema Mnyika.
Lukuvi alisimama tena na kusema; “Tumeomba saa moja tuendelee na mashauriano ili tutoke pamoja na siyo suala la vyama hapa. Tunataka tushauriane kama Bunge.”
Baada ya Lukuvi kumaliza, Spika Makinda alisema anatoa muda hadi saa kumi jioni ili viongozi wa upinzani na CCM wakakae ili kushauriana jinsi gani ya kuweza kuja na maneno yanayofaa kwenye mapendekezo yanayofuatia.
Hoja hiyo ilionekana kupingwa na wabunge wakieleza kwamba saa kumi jioni ni mbali hivyo Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe alisimama na kusema kuwa masaa mawili yanatosha kwa mashauriano lakini siyo saa moja kama Serikali ilivyoomba.
Spika alimpa nafasi Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia ambaye yeye alipendekeza masaa matatu ili kamati ikae na kuona jinsi gani wataweza kufikia mashauriano yao.
Spika Makinda alisema ni lazima wabunge waelewe kwamba mabunge ya kisasa yakifikia katika hali kama ya jana na juzi, lazima wakutane pande zote na kufanya mashauriano.
“Tuwe Bunge la kisasa lazima tushauriane tunapofika kwenye suala kama hili na hivyo mkutane wote na kukubaliana. Hivyo tukubaliane wakija na kauli moja tunapitisha,” alisema Spika Makinda.
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka aligomea kauli hiyo ya Spika na kueleza kuwa anakubali pande zote kutoa watu, lakini hakubaliani kwamba wakija na kauli moja ndiyo ipitishwe.
Kabla Ole Sendeka hajakaa Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekiel Wenje alisimama na kusema watu wapewe muda wa kushauriana, hivyo timu iundwe na ikae kwa muda mrefu ili wengine ambao hawatakuwa kwenye kamati hiyo wapate nafasi ya kutaarifiwa juu ya nini kinachoendelea.
“Kwa hiyo Spika mimi nakubali turudi saa kumi ili hiyo timu ikakae na sisi kwenye vikao vyetu tupewe taarifa tukifika hapa baadaye tumalizane tu,” alisema Wenje na hoja yake iliungwa mkono na wabunge hivyo Spika Makinda akasema viongozi wote wakae na kuja na kauli moja.
Pia, akitaka Zitto awe na wawakilishi kwa kuwa ndiye mwenye hoja, lakini wale wanaotuhumiwa wasiingie kwenye kamati hiyo. Hivyo akaahirisha Bunge.
Bunge laahirishwa tena saa kumi
Bunge lilirejea tena saa kumi jioni na kuahirishwa baada ya Spika kupewa taarifa kwamba kamati iliyoteuliwa kwa ajili ya mashauriano haijamaliza kazi.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenister Muhagama alisimama kwa upande wa CCM na kumweleza Spika kuwa corcus yao imeambiwa kwamba bado majadiliano yanaendelea.
“Spika sisi tulituma wawakilishi sita na mpaka sasa tumeambiwa kazi inaendelea lakini sijui kwa wenzetu imekuwaje lakini hadi sasa bado,” alisema Muhagama.
Spika Makinda alipokea taarifa hiyo na kuhoji upande wa upinzani una taarifa gani ambapo Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisimama na kusema, “Na sisi tumeelezwa kwamba bado.”
Kwa kauli hiyo Spika Makinda aliamua kuahirisha Bunge hadi saa moja jioni na kuwaeleza wabunge kwamba suala hilo lazima limalizike ifikapo saa mbili na robo usiku.
Wabunge walitoka nje na kuendelea na shughuli zao huku wengine wakijikusanya vikundi vikundi wakijadiliana. Wengine waliamua kukaa Kanteen ya Bunge kusikiliza hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ambaye amerejea nchini jana akitokea nchini Marekani alikokuwa kwa matibabu ya tezi dume.
Kilichotokea juzi usiku
Juzi Spika Makinda alilazimika kuahirisha Bunge kutokana na wabunge wa Kambi ya Upinzani kugoma kukubali marekebisho ya Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge kwamba uamuzi wa kumng’oa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo uachiwe mamlaka iliyomteua.
Chenge alifanya marekebisho akieleza pendekezo la kumng’oa Profesa Muhongo lisomeke kama lile la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi ambalo Bunge lilipitisha kwamba: “Bunge linaazimia kulifikisha suala hili kwa mamlaka ya uteuzi kwa hatua zaidi.”
Kipengele hicho kilikataliwa na upinzani na kuamua kusimama wakitaka Profesa Muhongo achukuliwe hatua lakini CCM waligoma ndipo Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliposimama na kusema kuwa haiwezekani kamati imependekeza mambo halafu Bunge linataka kuwalinda watuhumiwa.
Mbowe alisema kama Bunge linaamua hivyo wao hawawezi kuwa upande wa uamuzi huo kauli iliyowanyanyua wabunge wote wa upinzani vitini kutaka waondoke, ingawa Spika alimsihi Mbowe kuwatuliza, ilishindikana na Spika kuamua kisitisha Bunge hadi jana.
Jitihada kubwa zilifanyika kuwasihi wabunge wa upinzani kutulia lakini walianza kupiga kelele wakieleza kuwa hawawezi kulinda wezi.
Spika Makinda kabla ya kuahirisha aliwaeleza wabunge kuwa anapata wakati mgumu kwa kuwa Bunge limekuwa likiingilia shughuli za mihimili mingine na kwamba tayari ana kesi mahakamani kutokana na kuelezwa kuingilia shughuli za mahakama hivyo aliwaomba wabunge waache kutoa maamuzi ambayo yanaingilia mhimili wa Serikali.
“Tayari mimi nina kesi huko katika mhimili mwingine sasa mnataka nigombane tena na Executive (Serikali) itakuwaje jamani naomba tutafute maneno ya kutokuingilia mhimili mwingine,” alisema Spika Makinda.
Maneno yake hayo yalionekana kupuuzwa na wabunge wa upinzani na wengine wa CCM huku wakipiga kelele kuwa ni lazima watuhumiwa waliohusika kwenye sakata la escrow washughulikiwe kama ilivyokuwa kwenye sakata la Operesheni Tokomeza Ujangili.
No comments:
Post a Comment