Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wamemaliza ‘mnyukano’ wa muda mrefu wa vigogo wa kuwania
uenyekiti wa kudumu wa Bunge hilo, baada ya kutoa baraka zote kwa
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kugombea nafasi
hiyo.
Wakati Waziri Sitta akipewa baraka hizo na wajumbe hao kupitia Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM, Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, ameripotiwa kuamua kutogombea nafasi hiyo.
Pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Hassan Suluhu, amepitishwa na kamati hiyo kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Kudumu wa Bunge hilo kutokea Zanzibar.
NIPASHE lilimtafuta Sitta jana kueleza kupitishwa na chama chake, lakini alisema kuwa hakuwa kwenye mkutano huo hadi mwisho. “Niliingia kwenye kikao na kutoka mapema, sijui kama uamuzi huo umefikiwa,” alisema.
Vyanzo mbalimbali vya NIPASHE kutoka ndani ya kikao hicho vinaeleza kuwa, uamuzi wa kamati hiyo ulifikiwa baada ya kuwaita viongozi hao na kuwahoji kwa nyakati tofauti iwapo wana nia ya kugombea nafasi hizo au la.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Waziri Sitta na Waziri Suluhu, walipitishwa kwa kauli moja kuwania nafasi hizo, baada ya kamati hiyo kujiridhisha kwamba, wamekidhi sifa.
Mbali na Sitta, Suluhu na Chenge, chanzo hicho kilieleza kuwa mwingine, ambaye aliitwa na kuhojiwa na kamati hiyo ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, aliyefahamika kwa majina la Mwajuma Mgeni, ambaye hata hivyo, naye kama Chenge aliamua kutogombea nafasi hiyo.
Kabla ya kamati hiyo kutoa baraka hizo, kiongozi pekee aliyejitokeza hadharani na kutangaza azma ya kuwania nafasi hiyo ni Sitta pekee.
Sitta alisema anataka kuwania nafasi hiyo ili apate fursa ya kutimiza kwa vitendo ndoto ya Rais Jakaya Kikwete ya kuhakikisha Tanzania inapata katiba bora.
Imeelezwa kuwa wajumbe kadhaa walipendekeza jina la Sitta lipitishwe pasipo kuwapo mgombea mwingine, kwa maelezo kuwa wana-CCM wengine waliokuwa wanatajwa, wanaonekana kutokuwa na uwezo wa kulimudu Bunge hilo.
“Tumetoka kwenye kikao cha wajumbe wa CCM na kwa namna ya pekee, imekubalika kwamba Sitta ndiye anayefaa kwa uenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba,” kilieleza chanzo kimojawapo kwa sharti la kutokutajwa jina lake gazetini.
“Kama chama kimeonyesha imani yake kwa Sitta, na kwa mujibu wa Sheria, Makamu wake anatakiwa kutoka Zanzibar ambapo jina la Samia Suluhu limepitishwa ndani kwa wajumbe wa CCM,” kilieleza chanzo hicho.
Sitta amekuwa akitajwa ndani na nje ya Bunge Maalum la Katiba, kwamba anafaa kuchukua nafasi hiyo kutokana na rekodi nzuri aliyoiacha alipokuwa Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
ZENGWE LA SERIKALI TATU
Hata hivyo, waliokuwa wanampinga Sitta waliibua hoja kwamba mwanasiasa huyo mkongwe, amekuwa na mwelekeo wa kutaka kuwapo kwa serikali tatu, hoja aliyoipinga mara kadhaa akisema uamuzi wowote kuhusu hatima ya Katiba Mpya na hususani mfumo wa utawala utakavyokuwa, vitaamriwa na Watanzania.
HAKUNA MARIDHIANO
Katika hatua nyingine, matumaini ya kufikia maridhiano yatakayowezesha kupatikana kwa katiba mpya, yamezidi kufifia.
Hiyo ni baada ya wajumbe wa Bunge hilo kutoka vyama vya upinzani na makundi ya kijamii na wale wanaotoka CCM kuendelea kuvutana kuhusu utaratibu utakaotumiwa kupata uamuzi katika vikao vya Bunge hilo.
Katika mvutano huo, wajumbe wa CCM wanataka utaratibu utakaotumiwa kupata uamuzi katika vikao vya Bunge hilo uwe wa kura ya wazi, huku wale wanaotoka katika vyama vya upinzani na wa baadhi wanaotoka katika makundi ya kijamii wakitaka utumike wa kura ya siri.
Msimamo wa wajumbe kutoka vyama vya upinzani na makundi ya kijamii, ulifikiwa kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika kikao chake kilichofanyika juzi.
Chanzo chetu kutoka ndani ya kikao cha wajumbe wa CCM zinaeleza kuwa baadhi ya wajumbe walilalamikia kile walichokiita mjadala wa Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalumu kuachwa kuhodhiwa na wapinzani bungeni.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, baadhi ya wajumbe katika kikao hicho walitoa mfano wakisema uundwaji wa Kamati ya Kanuni za Bunge Maalumu, ambao walidai kuwa imeachiwa kuhodhiwa na wapinzani.
Mbunge huyo alieleza pia kuwa wajumbe wengine katika kikao hicho walidai kwamba hata Rasimu ya Kanuni ya Bunge Maalumu ya Mwaka 2014 zimetungwa kwa kuwabeba wapinzani.
Alieleza kuwa kuwa baadhi ya wajumbe katika mjadala huo, walitaka kumjua waliyemuita “mchawi” aliyesababisha hali hiyo.
MKAKATI WA KUTEKA BUNGE
Mtoa taarifa wetu alieleza kuwa baada ya majadiliano yaliyochukua takriban saa sita, hatimaye kikao kilifikia maamuzi mbalimbali, ikiwamo namna wajumbe watahakikisha utaratibu wa kupata uamuzi katika Bunge hilo kwa kura ya siri unadhibitiwa.
Alieleza kuwa jambo lingine, ambalo lilitolewa uamuzi na kikao hicho, linahusu namna ya kumdhibiti mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho.
Chanzo hicho kilisema udhibiti huo utalenga zaidi katika maelekezo yoyote yatakayotolewa na mwenyekiti huyo wakati wa kusimamia mjadala wa rasimu ya kanuni hizo hadi azimio la kuzipitisha litakapotolewa na Bunge hilo.
Kilisema kuwa maamuzi hayo pia yalipinga ushauri uliotolewa na Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela, wakati akichangia mjadala wa rasimu ya kanuni hizo wiki iliyopita, kwamba ushauri huo hauna maslahi na chama.
Chanzo hicho kilieleza kuwa kikao hicho pia kilipitisha maamuzi ya kujengwa mazingira ya kuahirishwa makusudi kikao cha Bunge cha jana asubuhi, kama ilivyotokea.
Kilieleza kuwa uamuzi huo ulipitishwa ili kuwapa fursa wajumbe wa CCM kuifanya marekebisho rasimu ya kanuni hizo kama wanavyotaka.
NDIYO DHIDI YA SIRI
Chanzo hicho kilieleza pia kuwa uamuzi mwingine uliofikiwa na kikao hicho ulitaka lazima mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo ahakikishe upitishaji wa vifungu vya rasimu ya kanuni hizo unafanyika kwa kura za wajumbe kupaza sauti za ndiyo au hapana.
Katibu wa wajumbe wa CCM, Jenista Mhagama, hakupatikana jana kuzungumzia yaliyojiri katika kikao chao cha juzi na hata alipopigiwa, simu yake ilikuwa inaita bila majibu.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment