Na Mwandishi Wetu
HATIMAYE Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions ya
jijini Dar es Salaam, Alex Msama ameibuka na kutamka yeye si Meneja wa malkia
wa nyimbo za Injili nchini, Rose Muhando akisema amekuwa akishirikiana naye
katika mazingira ya kawaida kama ilivyo kwa waimbaji wengine.
Kwa mujibu wa taarifa ya Msama kwa vyombo vya habari
aliyoitoa juzi, yeye akiwa mlezi wa waimbaji wote wa muziki wa Injili, amekuwa
akishirikana nao kwa karibu kutokana na nafasi yake katika huduma hiyo ya
uimbaji kwa kipindi cha miaka 15.
Msama aliyechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya muziki wa
injili nchini kutokana na kuandaa matukio ya muziki huo kama Tamasha la Pasaka,
uzinduzi wa albamu na Tamasha la Krismasi, alisema ameamua kutoa tamko hilo
kutokana na malalamiko ya muda mrefu ambayo amekuwa akipata juu ya Rose.
“Nimekuwa nikipokea malalamiko mengi ikiwemo kutoka kwa
viongozi wa kiroho wakiwemo Wachungaji na Maaskofu kwamba pengine nimekuwa
nikimzuia Rose (Muhando) katika matamasha wanayomualika na kushindwa kutokea.
“Lakini, naomba watumishi wa Mungu wanielewe katika hili,
sipokei mialiko wala simzuii Rose. Mimi ninapokuwa na matamasha, nimekuwa
nikimualika kama wafanyavyo wengine.
“Nimekuwa nikimlipa kiasi cha fedha anachotaka na hakuna
zaidi, hivyo mimi sio Meneja wake,” alisema Msama katika taarifa hiyo na
kuongeza:
“Agosti mwaka huu, kampuni yangu ilidhamini uzinduzi wa
albamu yake ya Kamata Pindo la Yesu, haikuwa na maana kwamba ni Meneja wake.
“Nilimualika uzinduzi wa albamu ya Uko Hapa ya msanii John
Lissu Oktoba mwaka huu, nilimlipa fedha, lakini hakutokea kama
ambavyo amekuwa akifanya kwa wengine ambao wamekuwa wakilalamikia tabia hiyo,”
alisema Msama.
“Pia wiki iliyopita nilikuwa na Tamasha la Krismasi
tulikubaliana aje katika maonesho hayo, lakini hakutokea na tulishamlipa,”
alisema Msama kwa masikitiko na kuongeza kuwa amemsamehe na anamuombea kwa
Mungu aweze kubadilika.
Alieleza kuwa hana tatizo na mwimbaji huyo, wala hana
ugomvi naye, lakini amekuwa akipata taabu kutoka kwa baadhi ya wachungaji pale
Rose anapoalikwa halafu hatokei na inaonekana yeye ndiye amemzuia.
“Sijawahi kupokea mialiko kwa niaba ya Rose, kila kitu
anafanya mwenyewe, hivyo ni vyema wadau wakafahamu hilo ,” alisema Msama na kusema angekuwa
mwepesi wa kulalamika, angeshafanya hivyo muda mrefu dhidi ya Rose.
Aidha, Msama amekana kuhusiana na madai ya Rose kutumia
dawa za kulevya na kusisitiza kuwa hajawahi kumuona ‘akijidunga’ kama ambavyo
baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti na kuongeza kama ikiwa ni
kweli, hilo pia ni suala binafsi.
“Baadhi ya vyombo vya habari vinaandika ni mjamzito,
nafikiri pia hayo ni mambo yake binafsi na hakuna mtu mwenye haki au uhalali wa
kuhoji hilo.Yule ni mtu mzima na mwenye kujielewa,” alisema Msama.
Rose ni mwimbaji mahiri wa muziki wa injili nchini
aliyejipatia sifa ndani na nje ya ukanda wa Afrika Mashariki ambaye mwishoni
mwa mwaka 2013, alisaini mkataba wa kufanya kazi na kampuni ya muziki ya Sony
ya Afrika Kusini.
Miongoni mwa albamu zilizompa umaarufu Rose kiasi cha kuwa
alama ya mafanikio ya muziki wa injili nchini ni ‘Uwe Macho,’ Nyota ya Ajabu
(Zawadi ya Krismasi), 'Jipange Sawasawa', 'Kitimutimu', ‘Mungu Anacheka’ na 'Wololo' na 'Kamata Pindo la Yesu' aliyoachia hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment